UJASIRIA-VIJANA NA UKABURU WA KIUMRI

 

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

 

Sehemu mbalimbali za dunia hii zimewahi kutawaliwa na viongozi wenye sifa na tabia
tofauti, na waliofanya mambo makubwa ya kuziendeleza nchi zao, na hata
kuzibomoa. Afrika pia ilizalisha viongozi wa aina hiyo. Uwatajapo Kwame Nkrumah
au Julius Nyerere unataja viongozi waliokuwa na ndoto za kujenga jamii zenye
utu. Uwatajapo Bokassa, Mobutu, Idi Amin au Kamuzu Banda, unakuwa umetaja
viongozi wakatili, vibaraka wa mabeberu, waliopora nchi zao na kuwatesa wananchi
wao.

 

Lakini
utu wa Nkrumah na Nyerere haukutokana na dini zao au makabila yao. Ulitokana na
itikadi ilizowaongoza katika mapambano yao. Wote waliongozwa na itikadi ya
Umajumui wa Afrika (pan-Africanism),
itikadi ambayo ililenga kulikomboa bara la Afrika toka katika utawala wa
kikoloni, na hatimaye kuliunganisha ili kuunda dola moja lenye nguvu. Uundwaji
wa dola hilo ndio ungekuwa salama ya Afrika katika mfumo katili na wa kinyonyaji
wa ubepari wa kimataifa (global
capitalist system
). Hivyo, kati ya nguzo kuu za Umajumui wa Afrika ni
upingaji wa ubeberu. Sina hakika kama mtu anaweza kuwa mmajumui mzuri bila kuwa
mpinga ubepari, na mpiganiaji wa mfumo mbadala wa uzalishaji mali na ugawanaji
ziada. Ndio maana Nkrumah na Nyerere walikuwa pia wajamaa.

 

Kusema
kwamba wote walikuwa wakiongozwa na itikadi ya Kijamaa na dira ya Umajumui wa
Afrika hakumaanishi kuwa magwiji hawa hawakutofautiana. Ndani ya itikadi hizo
mbili kuna tofauti nyingi. Lakini tofauti hizo zilikuwa ni za njia (means) za kufikia lengo (end). Lengo ni kuiunganisha Afrika,
kujenga mfumo mbadala, na kupambana na kila aina ya unyonyaji, ubaguzi na
ukandamizaji. Hivyo, mara kwa mara walipokutana, hasa katika mikutano ya nchi
za Umoja wa Afrika walibishana juu ya namna ya kujenga dola huru la Afrika.
Kamwe hawakutofautiana juu ya haja ya kuwa na Afrika iliyoungana.

Kwa
bahati mbaya kizazi hicho cha viongozi wenye dira, na wanaoongozwa na itikadi
pana kimeondoka. Tumebaki na watawala vibaraka, wanaopigania fursa za kupendwa
na mataifa ya mabeberu na wanaoshindania kinyang’anyiro cha kuzirudisha nchi
zao utumwani kwa kuvutia makampuni ya kimataifa kuwekeza katika nchi zao.
Miongoni mwa vivutio hivyo vikiwa kutoa misamaha ya kodi, kuruhusu utoroshaji
wa mitaji na faida, na kuwalazimisha wanyonge kuwapisha wawekezaji-papa hata
ikibidi kwa mtutu wa bunduki. Taifa letu la Tanzania haliko nyuma katika hilo.

 

Nimetaja
neno taifa. Je, ni sahihi kuiita Tanzania taifa (nation)? Kuelekea uchaguzi wa mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alitumia
jitihada kubwa sana kusisitiza kuwa sisi bado ni taifa changa. Na kwa kweli
hatukuwa taifa. Tulikuwa mkusanyiko wa makabila mbalimbali. Vikabila hivi
ndivyo vitaifa vyetu. Mwalimu alitolea mfano wa George Kahama alipokuwa katika
ndege. Ndege ilipopata msukosuko akasema “My God!
 Lakini ilipotikisika mara ya
pili akasema “Mungu wangu!
” Ilipotikisika zaidi Akasema “Mawee”! Kwa jinsi
kataifa ketu kalivyo kachanga, alisisitiza Mwalimu, mtu akipatwa na msukosuko
atasema, “Mawee”! Bado tuna damu ya makabila ndani yetu.

 

Lakini
kwa Mwalimu, ukabila haukuwa usukuma, uzanaki au uhaya peke yake. Hata utaifa
[kwa maana ya nationalism] pia ni
ukabila. Mwalimu alisisitiza kuwa utaifa [nationalism]
usioongozwa na itikadi pana ya Umajumui, ni sawa na ukabila katika ngazi ya
bara la Afrika [Nationalism outside
pan-Africanism is equivalent to tribalism at the continental scale
]. Ndio
maana Mwalimu alipinga vikali ukabila wa Utanganyika na Uzanzibari.

 

Leo
hii Mwalimu angefufuka angeomba arudi huko aliko. Asingeamini kuwa kale kataifa
kachanga sasa kameshakufa. Hakuna Tanzania tena: tunaimba nyimbo za Utanganyika
na Uzanzibari. Labda angepigwa butwaa zaidi kuona nyimbo za Utanganyika
zinapigwa zaidi, na safari hii madijei wakiwa wale “vijana wake” aliowakabidhi
kuendesha taasisi yake, huku wacheza dansi wakuu wakiwa wanasiasa na
wanaharakati toka asasi za kiraia. 

 

Udini, alioupinga kwa nguvu zote, sasa ndio
umekolea. Bila shaka hata yeye angepokea ujumbe wa simu ya kiganjani toka
kwa  wakristo wakiwabeza waislamu, au
waislamu wakiwabeza wakristo. Ambacho kingemchefua ni kuona jinsi wanasiasa
wanavyotumia madhehebu na misikiti kupandikiza udini ili wapate urahisi wa
kuingia Ikulu!

 

Yumkini
hayo yangemsikitisha na kumsononesha, lakini yasingemshangaza. Alikuwa ameyaona
na kushiriki kuyakemea kikamilifu katika miaka ya tisini. Labda ambalo
lingemshangaza lingekuwa ni aina mpya ya Ukaburu. Hii sio ile ya “Uzawa”,
ambayo pia Mwalimu aliita “Ukaburu”! Hii ni aina mpya ya Ukaburu, na bila shaka
Mwalimu angeiita “Ukaburu wa Kiumri”. 

 

Katika miaka ya mwanzo ya Uhuru, Mwalimu
alipambana kwa dhati na Ukaburu wa Uzawa, uliolenga kutoa uraia na nafasi za
uongozi na fursa za kiuchumi kwa watu wenye ngozi nyeusi peke yake. Akiwa
Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mwalimu alikemea hilo, katika Bunge la Tanganyika
tarehe 18 Oktoba 1961:

 

Kama sisi Watanganyika tutaanza kusema kuwa
watu wote wa Tanganyika ni sawa isipokuwa Wahindi, na Waarabu na Wazungu, na
Wachina, wanaoishi Tanganyika tutakuwa tumevunja kanuni. Kanuni hiyo
haitaturuhusu tuishie hapo. Kama uraia wetu utakuwa si jambo la utii wa nchi
bali jambo la rangi, hatutaishia hapo. Tutaendela kuivunja kanuni hiyo, na
nimeshasikia watu hapa wakifanya hivyo tayari. Nimesikia mara kadhaa… maneno ‘Waafrika
Wazawa’. Wameanza kuwatofautisha Waafrika pia… ipo siku ambayo tutasema watu
wote ni sawa isipokuwa Wagogo, isipokuwa Waha, isipokuwa waliooa zaidi ya mke
mmoja, isipokuwa Waislam, n.k. Tutaendelea kuzivunja kanuni hizi”

“Unajua nini kinachotokea pale watu
wanapoanza kuleweshwa na madaraka na kuanza kutukuza rangi zao, akina Hitler, ndicho
wafanyacho. Unajua wananakopeleka ubinadamu, akina Verwoerds wa Afrika Kusini,
ndicho wafanyacho… Hawa watu wanatuambia tubaguane kwa sababu ’ya mazingira
maalum ya Tanganyika.’ Hiki ndicho Verwoerd anachosema ‘Mazingira ya Afrika
Kusini ni tofauti’. Hoja hii hutumiwa na wabaguzi wa rangi/Makaburu
”!

 

Leo
hii wameibuka wanasiasa ambao kwa kila namna ni makapuku wa kisiasa na
mbilikimo wa kiitikadi.  Wameona hoja
pekee ya wao kuteuliwa kugombea urais katika vyama vyao ni kupandikiza sumu ya
ubaguzi wa kiumri. Hoja hii haikuanza kama ubaguzi. Bali ilianza kama
ujasiria-vijana, yaani utumiaji wa kundi la vijana kama mtaji wa kisiasa. Hivyo
makaburu hawa walianza kupigania haki ya kupunguza umri wa kupiga kura hadi
miaka 16, na kugombea urais hadi miaka 35. 

 

Muda ulivyokwenda ndivyo sura halisi
ya ukaburu ilivyoibuka. Hoja ya umri wa kupiga kura ikafifia, ya umri wa urais
ikapaa. Taifa zima likaingia katika mjadala ili kumwezesha mtu mmoja kutimiza
ndoto ya kuwa atakuwa rais akiwa na umri chini ya miaka 40. Baada ya muda
ukaburu halisi ukajitokeza: sasa wenye hoja hiyo wakadai kuwa mwaka 2015 watu
wote waliozaliwa kabla ya 1961 wasiruhusiwe kugombea urais. Wanadai kuwa sasa ni wakati wa vijana. Wazee ndiyo
chanzo cha matatizo, waiachie nchi kwa vijana. Ndani ya UVCCM pia wapo vijana wamebeba
bango hilo: Rais awateue wao vijana kuwa wakuu wa wilaya na mikoa, na Chama
kiwateue kuwa makatibu wa wilaya na mikoa kwa sababu wazee wameshindwa!

 

Na
vijana wameimeza sumu hiyo. Wanakutana katika makundi yao na kupendekeza majina
ya “vijana” wenzao kugombea urais. Wanaopendekezwa ni wale wale waliobeba hoja
ya kupunguza umri na kuzuia waliozaliwa kabla ya 1961 kutogombea. Mmoja wao
sasa keshaanza pia kuzunguka makanisani!

 

Kwa namna yoyote kinachopandikizwa hapa ni sumu ya ubaguzi
– ubaguzi wa umri. Katika mfumo wa kandamizi na wa kinyonyaji tulionao,
uliowafanya watu kupoteza matumaini, ni rahisi sana kupandikiza sumu ya aina
hiyo na ikafanya kazi.
Kama hoja ya leo ni
umri, kesho itakuwa ni dini. 

 

Tuna hoja gani ya kumjibu atakayetushawishi kuwa
nchi hii imetawaliwa na wakatoliki wawili na waislam wawili katika kipindi cha
miaka 50 na hakujawahi kuwa matumaini? Kisha akituambia kuwa chanzo cha
matatizo yetu ni hizo dini mbili, na kwamba ni wakati sasa wa kuwajaribu
waprotestanti au wapagani, tutakataa? Akija mwingine akatuambia chanzo ni
makabila yaliyotawala na kwamba sasa ni wakati wa kuwajaribu wahaya, wasukuma,
wanyakyusa au wachagga tutakataa? 
Na, je atakayetuambia chanzo ni kutawaliwa na watu
wasio na Phd za darasani? Na, vipi atakayesema kuwa chanzo ni kuwa marais wote
walikuwa wanaume, na kwamba sasa ni wakati wa kumjaribu mwanamke?

 

Ukaburu wa kiumri, kama ulivyo udini, ukabila, ni
mjadala uliolenga kununua hisia za wanyonge na kuwafanya wasihoji chanzo cha
ufukara wao na kudadisi sababu za utajiri wa wenzao; waendelee kutawaliwa na
kunyonywa na kijitabaka kilekile ambacho kinazidi kujizalisha (tena sasa
kinajizalisha kinasaba); na wasiweze kujenga umoja ili kukipindua kijitabaka
hicho kinachokumbatia mfumo kandamizi wa uliberali mambo-leo. Ni mjadala
unaogusa hisia na kujaribu kuwafanya vijana wajione wao ni kundi moja, kundi
linalounganishwa na umri. 

 

Ni kipi kimfanyacho kijana mlalahoi wa Nyamitwebili
ajione kuwa yeye si sawa na walalahoi wenzake wenye umri wa zaidi ya miaka 40,
eti kisa ni wazee? Halafu ajione yuko sawa na jamaa fulani wanaopokea milioni
1o kwa mwezi, eti kisa ni vijana? Ni wakati sasa wa wanyonge kuamka na kukataa
itikadi na mirengo finyu inayokumbatia dini, kabila, nchi, chama.

 

Mwandishi
wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya
Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe sany7th@yahoo.com