Na Isaack Mdindile

@isaac29g

Ni saa 11 kamili alfajiri hapa Brazil, mida inaenda kasi ya korona. Mikono inawasha, inataka kunawa ili iandike. Nachapa “korona” kwa kompyuta, wala haishtuki tena kwa kuchora mstari mwekundu kama mwanzo. 

Sasa neno korona limepata uraia, limeingia kwenye kamusi yetu. Misamiati ya kiswahili imepata nduguye. Kumbe, lugha nazo huazimana mawazo, aleluiya. Eneweyi, tuache hayo….

Tukiacha hayo tutaongea nini? Na suala sio kuongea, bali unaongea nini na vipi? Maana, kuna kuongea na kufungua mdomo! Pia, chaguo ni lako, kutumia ulimi kuzungumza au kuhesabia meno.

Basi leo naamsha gumzo kwa kuzungumza yale ambayo wengi hatupendi kuyagusa. Ni kuhusu imani, dini, jinsi(a), itikadi na misimamo yetu. Binafsi, imenichukua kitambo kuanza kujikubali na kukubali kukosolewa, na bado safari ni changa.

Kisa cha kweli…

Nakumbuka, kipindi tunaishi kijijini Mapogoro (asili ya ubini wake ni miti fulani) kumkosoa mtemi wetu, Mwami Sabuni, ilikuwa kama kujitakia laana. Ila kuna nyakati ilibidi kumkalisha chini maana badala ya kuwa sehemu ya suluhisho alikuwa ni tatizo.

Mzee alichukuliwa kama mungu-mtu, na hii nadharia bado ipo kwa baadhi ya viongozi wetu hapa. Hata kama hazina hoja, kauli zao hawataki zihojiwe.

Mfano hai ….

Wakati wa kampeni za uchaguzi hapa Rio de Janeiro, kuna wachungaji na maaskofu walidiriki kusema kwamba mgombea Jair Messias Bolsonaro ni chaguo (Messia) la Mungu. Walienda zaidi kwa kumtengenezea kaulimbiu; “Brasil acima de tudo, Deus acima de todos” (Brazil juu ya kila kitu; Mungu juu ya kila mtu). Mfano wa huu wa kaulimbiu au motto ni kama ule wa Ujerumani kipindi cha Hitler. Moto wake hapo baadae, ni historia tu, inaweza simulia bila kupindisha. 

Historia ina tabia ya kujikwaa, na kuturudisha nyuma, ili tuelewe somo. Hivyo, ukitaka kuelewa vizuri hizi ndoa za siri kati ya baadhi ya wachungaji, wanasiasa, na wafanyabiashara, angalia filamu halisia ya The family huko Netflix. Hapo utapata pia ufunuo mzuri wa hawa Marais Trumph na huyu Bolsonaro. It’s phenomenal.

Sasa wiki ya jana, huyu Rais wa Brazil, akiwa na wakereketwa, pamoja na wachungaji wake waliitisha mkusanyiko wa maombi kwa taifa, wakafanya maandamano ya kupinga karantini, pamoja na kugoma kufunga ibada makanisani. Baada ya kushinikizwa, wamerudi nyuma. Na mpaka naandika hii shajara vifo kutokana na hii korona vimeshafika karibu elfu mbili na vituo vya afya vimejaa. Mbaya zaidi, Raisi amemfukuza waziri wa afya, Bwana Luiz Henrique Mandetta.

Ila nilishanga, hili la Raisi anaitisha maandamano kupinga maamuzi ya serikali, ulishaona wapi? Ni danganya toto, kutufanya sisi wajinga. Ni dhahiri, kwamba wanajificha nyuma ya mwamvuli na soli ya dini, kuhalalisha agenda zao. Ni utume wa mfumo dume. Isingekuwa vyombo vya sheria kuingilia kati, sijui tungekuwa wapi.

Kimya kimya, na-miss, maandamano, ile kukutana tu kama wananchi na kuzungumza yetu, bila sababu za kiitikadi wala madai. Napanga, kuwakilisha hoja bungeni kwamba baada ya kupita hili janga, wananchi turuhusiwe kuandamana, sababu yake ni ya kiafya zaidi.

Kila uchao, Rais anakemewa kuhusu kauli zake za kuwavunjia heshima wanawake, kudharau wapinzani na kubagua watu wa asili wa Brazil na kukandamiza haki za wafanyakazi. “Watawala kama hawa ni kama ng’e wanatembea kimadaha huku wanatema sumu njiani” alisema babu yangu mzee Msawasi.

Turudi kwenye kesi yangu kijijini….

Mzee Mwami alikuwa “mao de vaca” yaani mbana matumizi hasa kama wanenavyo wabrazil. Sio tu kubana matumizi ya madafu, hata majibu yake, kimkato sana. Wakati anaongea, ilibidi kusikiliza zaidi yale ambayo haongei.

Akina mama ndio walitufunda namna na wakati wa kuongea na mtemi. Halafu, nasikia maraisi na mawaziri wanawake (sio jinsia bali jinsi) ndio wanalikabili vizuri hili janga la korona. Sio fake news! Ni ukweli hata kama mtasema huu ni uchochezi na ni habari za kibepari.

Mara paap Cuba wamegundua chanjo ya korona…

Hamuishiwi mate, bado mtachonga visa na vitasa kufungia vichwa. Najaribu kuwaza, iwapo wapinzani wetu hapa wakaja na suluhisho mbadala kukabiliana na hili janga katika mazingira yetu, je, serikali ya zamu hii itakuwa tayari kuazima?

Tuongee tu bila kuoneana wala kuona aibu…

Ila karantini inachosha na kukosha bwana. Mitandao pia inaboa. Nimekumbuka, kuna maswali nilitumiwa huko fesibuki; “Eti, kama shule, vyuo, ligi za michezo, makongamano, madarasa vimefungwa, kwanini nyumba za ibada zisifungwe? Ni Mungu gani huyo ambaye, anajifunua tu kwenye nyumba za ibada, hawezi kufanya hivyo majumbani na mitaani kwetu? Mbona tunamfukarisha Mungu kiasi hiki! Hakika ni kuwafanya waumini kama watoto, yaani hawawezi kusali pekee yao”! Eeh, watu wana maswali, aisee.

Natema hizi cheche na kutetea hadi kwa kucha zote, sio tu uhuru wa kujieleza, bali tisa kumi, nafasi ya fikra mbadala, lakini sio rahisi kama tunavyofikiria. Ni safari ya nyakati za jua na mvua, bara na visiwani.

Moja ya tukio ambalo linaweza kuwa kioo kwetu, ni msimamo wa pamoja wa jinsi ya kukabiliana na hili janga kutoka kwa taasisi/asasi mbalimbali hapa Brazil. Licha ya fujo na figisu za Rais, ambaye kwake kila tatizo linatatuliwa na wanajeshi na kupiga magoti, ukomavu na umoja wa hizi taasisi ulinijaza povu la wivu.

Nawamegea kipande cha ujumbe wa maaskofu, wawakilishi wa wasio na dini, wachungaji na mamufti:

“Sisi tutakuwa, mstari wa mbele kusaidia maskini, wasio na makazi na chakula kipindi hiki cha korona. Serikali iandae mpango na bajeti ya dharura kunusuru familia masikini, mambo ya ibada ituachie sisi. Tunarudia, hakuna ibada makanisani wala dua misikitini. Tusali nyumbani, tukumbuke kwamba sisi ni hekalu takatifu na nyumba zetu ni kanisa pia. Tusiogope, Mungu hapungukiwi, anaendelea kuwa mkubwa kuliko korona,” ndivyo ujumbe ulivyoishia.

Kama manabii, bila woga walitoa huu waraka mapema kabla hata ya ule wa serikali. Au kama wasemavyo Watanzania; “hawakusubiri maagizo kutoka juu.” Nilivuta pumzi la tabasamu, kuona uhuru na ukomavu wa taasisi zilizo mstari wa mbele kulinda haki na ustawi wa jamii.

Na zaidi, baadhi ya maaskofu/wachungaji wameruhusu mahekalu yao kuwa hospitali, maana vituo vya afya zimezidiwa. Na baadhi ya wachungaji wanatoa huduma huko huko mahospitalini.

“Kwa kanisa langu kuhudumia wagonjwa wa hivi virusi ni baraka na heshima kubwa sana” Mchungaji Magdalena de Souza, alisisitiza.

Kipindi hiki kimenikumbusha maana ya ubatizo wangu. Nilibatizwa katika dini ya asili ya kiafrika, baadae ukristo na kuishi na waislamu vizuri tu. Mie ni mwingi, kama ambavyo Watanzania wengi tumejaliwa. Sivumilii na kustahimili tu, bali naheshimu na kustawisha imani za wengine.

“Mungu hana jinsia wala dini, haja yake ni moyo mkunjufu na rehema” misahafu inaandika. Lakini, kusoma tu hii misahafu bila historia ya nyakati, wala kujua lengo la mwandishi ni kuhujumu ujumbe kamili. Misahafu na mapokeo yake, lazima yasomwe kwa jicho la fikra tunduizi kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira yetu. Sayansi ya Mungu (theology) inafundisha hayo. Ndio maana, sishangai, kwa mfano, Biblia ya wakristo kuwa na maswali zaidi kuliko majibu. Lengo ni kututafakarisha, sio kumezeshwa tu imla na mila fulani.

Na ibada sio njia pekee ya kumwabudu Mungu. Ibada ya kweli na hukumu itatoka katika matendo ya huruma kama kuwasaidia wazee, maskini, wagonjwa, kupigania haki za kijamii na maendeleo, uhifadhi wa mazingira na kulinda maisha kwa ujumla. Yaani kufuata sayansi, kukuza tafiti na kusaidia wataalamu wa afya ni tendo la kiimani zaidi kuliko unavyofikiria.

Dini au kikundi fulani kuona kina hatimiliki ya kusali kwa sauti kubwa bila kuzingatia afya za majirani, kuuza maji ya baraka, kuona ni kawaida na kukaa kimya, bila kuonesha kwa vitendo njia mbadala kuhusu uchafuzi wa mazingira na ongezeko la umaskini nchini, kwa mfano, basi hili kundi ni janga la taifa, zaidi ya hivi virusi. Inabidi kurekebisha mapema. Sio ustaarabu wala utaratibu kibinadamu.

Wino umeisha kwa leo, usisahau kunawa mikono!