Tulio wapenzi wa fasihi tumeupokea ujio wa jarida-mtandao la Umbu kwa furaha na faraja kubwa. Aidha kwa wapenda historia, Umbu limekuja kama sauti ya kuweka urari katika simulizi za ukombozi wa taifa letu.
Nimelisoma toleo lote la awali ndani ya muda mfupi sana, nikibugia uhondo wa uandishi na utunzi bora kabisa kutoka kwamkusanyo wa aina ya kipekee wa waandishi na washairi wanawake.
Naweza kusema bila kusita kwamba kazi ya ukusanyaji wa maandishi katika Umbu kwenye toleo la kwanza lililopewa jina la Titi imefanywa kwa umakini na umahiri uliopea. Ni kazi inayostahili pongezi.
Titi, jina la mmoja wa wapigania uhuru wa awali kabisa katika Tanganyika, ambayo ilikuja kuungana na Zanzibar kuunda taifa la Tanzania, limetumika vema kusawiri taswira nzima ya dhamira ya Umbu toleo la kwanza. Titi, kwa sadfa, ni moja katika viungo pacha vya mwanamke vikaavyo kifuani, vikisimama kama nembo mojawapo ya uzuri wa umbile la mwanamke, wenzo wa awali katika kuimarisha maisha na afya ya mtoto, na kwa maana hiyo jamii, na silaha katika mapambano ya haki kwa wanawake.
Uandishi wa kibunifu katika Umbu toleo hili la awali umeweza kuiteka nadhari ya msomaji kupitia mbinu za kihistoria, kishairi na hadithi fupi kuitumia nguzo ya Titi kama dhamira ya kuunganisha nguvu za udugu wa wanawake na kuidhihirisha nguvu yao katika jamii, nguvu ambayo imekuwa ama ikipuuzwa au ikifunikwa na ‘simulizi dume’ kwa matilaba ya mfumo wa kimazoea uliotamalaki kwa miongo mingi tangia Tanzania ipate uhuru wake. Na hii si kwa Tanzania pekee, simulizi za wanawake zimekuwa zikizimwa na kupata tabu kujulikana mahali pengi pengine.
Waandishi katika Umbu wamejidhihirisha kuwa wabunifu weledi na wapigania urari katika mitazamo ya kijamii hususan imhusuyo mwanamke. Kidonda na Umpendaye, japo zenye kusisimua na kuvutia sana usomaji, zimetungwa katika mfumo wa maumbu kufundana kuhusu maadili katika maisha ya mwanamke. Hali kadhalika Titi Furaha ya Kweli, Titi la Jirani na Matiti Yangu Wapenzi yana mvuto wa kipekee unaotukumbusha msemo maarufu wa kishairi wa Shaaban Robert kuwa Titi la Mama li Tamu. Ninavyomkumbuka Bibi Titi, Aliyoniambia Mama yangu kuhusu Bibi Titi, Kafara ya Talaka na Nibatize ni miangwi ya roho ya uanamapinduzi katika mwanamke. Nguvu ya Matiti na Matiti, Uwanja wa Mapambano na ni sauti ya upinzani dhidi ya uovu na dhulma za kimfumo kwa kutumia uanamke.
Ninavyomkumbuka Bibi Titi – Chemi Che-Mponda
Aliyoniambia Mama yangu kuhusu Bibi Titi – Saleha Sally Akhtar Qazi
Kafara ya Talaka – Rachel Maina
Titi Furaha ya Kweli – Dkt. Salma Omar Hamad
Titi la Jirani – Isabella Lucas
Matiti Yangu Wapenzi – Manka John
Matiti, Uwanja wa Mapambano –Neema Komba
Pamoja na mafanikio haya ya kimaudhui, natamani kufuatilia kwa umakini matoleo yajayo ya Umbu kuona uendelevu wa mkusanyo wa waandishi wanawake pekee au mabadiliko katika kujumuisha waandishi wanaume wenye mawazo au michango iendanayo na dhamira ya Umbu. Lakini nakiri kwamba mkusanyo wa waandishi hawa wanawake umekuwa na mvuto mithili ya matiti ya mwali ambayo hayachushi kuyatazama!
Nimefurahia namna dhana ya Titi ilivyotumiwa kiufundi kwa uandishi wa makala, ushairi, hadithi na insha katika kuileta taswira ya kwanza kabisa ya Umbu. Nasubiri kwa hamu matoleo yajayo.
Kongole kwa timu nzima ya Umbu!
Jarida la mtandaoni la Umbu ni hatua muhimu sana katika kuiweka fasihi ya Kiswahili mahali inapostahili. Natoa pongezi za dhati kwa hatua hii adhimu. Natoa rai kwa watu kutembelea jarida hili.