Yafuatayo ni majibu ya Tundu Lissu kuhusu makala ya Mambo ya Msingi ambayo hayazungumzwi katika Madai ya Katiba Mpya yaliyoandikwa na Nassoro Kitunda.
Hoja kwamba mjadala wa Katiba Mpya haujagusa maslahi ya walalahoi
Huu ni utetezi mwepesi sana wa Samia Suluhu Hassan na CCM yake, ambao wanasema Katiba Mpya sio muhimu kwa sasa; kwamba haitawaletea wananchi ugali mezani, na kadhalika. Nianze na hii hoja ya kwamba mjadala wa Katiba Mpya haujagusa maslahi ya walalahoi. Kama yeyote aliyewahi kuangalia Rasimu ya Warioba au Katiba Inayopendekezwa, hata kwa juu juu tu, anavyoweza kuthibitisha, kulikuwa na mjadala mkubwa sana juu ya haki za kisiasa, kiuchumi, na kijamii za wananchi wetu wakati wa nyaraka hizo.
Matokeo ya mjadala huo ni kwamba nyaraka hizo mbili zimefafanua haki hizo kwa namna ambayo ni pana kuliko waraka mwingine wowote wa kikatiba uliowahi kutolewa hapa nchini katika historia yetu yote. Tunaodai Katiba Mpya tunadai Katiba Mpya yenye mambo haya pia, sio Katiba Mpya inayofafanua haki za kisiasa tu. Kwa hiyo, yeyote anayedai, kama mleta mada hii, kwamba mambo haya muhimu hayazungumzwi kwenye mjadala wa Katiba Mpya ni kwamba hajaufuatilia mjadala wenyewe au anapotosha kwa sababu na makusudi mengine.
Kile kisichosemwa na mleta mada na wenye hoja za aina hii (sub-text), ni kwamba Katiba Mpya na ya kidemokrasia haina maslahi yoyote na walalahoi bali inaangalia maslahi ya ‘walalaheri.’ Kwa ufupi, madai ya demokrasia hayana maana yoyote kwa wasiokuwa nacho, n.k. Hoja hii haina ukweli wowote kihistoria mahali popote duniani na hata hapa kwetu Tanzania.
Kama ambavyo historia ya mapambano ya walalahoi imethibitisha kila mahali, demokrasia na haki nyingine za kisiasa ni muhimu sana katika mapambano hayo. Bila kudai haki za kisiasa za kuanzisha au kujiunga na vyama vya siasa, kupiga na kupigiwa kura, kugoma, n.k., matabaka ya walalahoi wa Ulaya Magharibi na kwingineko katika nchi zilizoendelea yasingeweza kupata mafanikio makubwa katika madai yao ya haki za kiuchumi na kijamii. Haki za kisiasa, yaani Katiba Mpya, ndio ziliwezesha mapambano ya haki nyingine za matabaka ya walalahoi. Ndio maana historia ya mapambano ya walalahoi wa nchi zote zilizoendelea, tangu Enlightenment(Kipindi cha Mwamko wa Kifikra Barani Ulaya) mpaka sasa, ni mapambano ya kupanua wigo wa haki za kikatiba za walalahoi hao.
Mara nyingi mapambano hayo yalitumia lugha ya kudai nafuu ya maisha na maslahi ya wafanyakazi. Mara nyingine yalitumia lugha ya kikatiba au kisheria. Lakini mara zote yalichukua sura ya kisiasa na matokeo yake yalionekana kwenye mabadiliko ya kikatiba, kisheria, na kitaasisi. Mfumo wote wa afya ya jamii, social security (hifadhi ya jamii), elimu n.k., katika nchi za Magharibi ni mfano mzuri na halisi wa hili.
Kwa hakika, Katiba Mpya inaweka utaratibu na utamaduni mpya wa kushughulikia changamoto ambazo tunaweza tusizijue kwa sasa kwa sababu ya upeo wetu mdogo wa ufahamu. Katiba Mpya ya Marekani ya 1787 haikusema chochote juu ya watumwa, au Watu wa Asili wa Marekani (Native Americans) au wanawake, weusi au weupe (black or white). Na kwa hakika, haikuweka haki za binadamu kabisa (Hiyo ilifanywa katika Mabadiliko ya Kwanza [First Amendment] baada ya Katiba Mpya kuwa imepitishwa).
Lakini Katiba Mpya hiyo iliweka utaratibu wa kujadili na kutatua matatizo mbalimbali yaliyokuja kujitokeza kwa miaka 250 iliyofuatia ya historia ya Marekani. Inasemekana Benjamin Franklin, Baba wa Taifa mmojawapo (one of the Founding Fathers), alipoulizwa na mtu mmoja mmetuletea nini alisema: ‘tumewaletea Jamhuri, kama mnaweza kuilinda’! Katiba Mpya inaleta haki na mfumo mpya wa kujitawala ambao unahitaji kujengwa na kuimarishwa na kulindwa. Baba wa Taifa mwingine wa Marekani, Thomas Jefferson, naye alisema gharama ya uhuru ni kuwa macho milele (‘the price of freedom is eternal vigilance’).
Katiba Mpya ni mwanzo, sio mwisho, wa kazi ya kujitawala.
Kwa hiyo, hoja ya mleta mada – inayoonekana kijuujuu kama iliyoandikwa kwa kufuata misingi bora ya uchambuzi wa Ki-Marx wa matabaka (in the best traditions of Marxist class analysis) – kwamba demokrasia haina maana yoyote kwa walalahoi, kiukweli haina u-Marx wowote. Ni jaribio tu la kujificha kwenye pazia la Marxist class analysis ili kuficha hoja halisi: utetezi wa mfumo uliopo wa kikatiba na utawala ambao umekuwa madarakani tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru wetu.
Matumizi mabaya ya mfano wa Afrika Kusini na Kenya na hoja za Prof. Issa Shivji
Imekuwa ni kawaida kwa watetezi wa mfumo tawala (status quo) kudai kwamba Katiba Mpya sio mwarobaini wa matatizo yetu yote. Wenye hoja hii wanapenda kukimbilia mifano ya Katiba Mpya za Afrika Kusini na Kenya iliyotolewa kwa mara ya kwanza na Prof Issa Shivji miezi kadhaa iliyopita. Kwamba nchi hizo mbili zina Katiba Mpya bora kabisa lakini bado zina matatizo mengi na makubwa tu ya kisiasa na kijamii, n.k. Kilichojificha hapa (Left unsaid) ni dhana kwamba Katiba Mpya za nchi hizo hazijawasaidia wananchi wao kwa chochote kile.
Hoja hii ni dhaifu sana. Kwanza, hakuna yeyote ambaye amewahi kudai kwamba Katiba Mpya ndio dawa – mwarobaini – wa matatizo yetu yote ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, n.k. Katiba Mpya sio mwisho, bali ni mwanzo, wa safari ya kutatua matatizo hayo kwa njia za amani.
Katiba Mpya inaweka msingi au muundombinu (framework) wa kuyajadili matatizo hayo na kuyatatua. Ni kweli kwamba Afrika Kusini na Kenya bado zina matatizo mengi na makubwa. Lakini je, kuna yeyote Afrika Kusini anayetaka kurudi kwenye katiba za nyuma za mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid)? Je, ni nani Kenya anayetaka kurudi kwenye katiba za kiimla za Kenyatta wa Kwanza na Moi?
Ukweli ni kwamba, licha ya matatizo yao, nchi hizo zimepiga hatua kubwa katika mifumo yao ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii hasa kwa sababu ya kuwa na Katiba Mpya. Wote ni mashahidi wa jinsi mahakama za nchi hizo au mabunge yao yanavyofanya kazi kwa ufanisi ambao kwetu ni ndoto. Ni kwa sababu ya Katiba Mpya na utamaduni mpya uliozaliwa na Katiba Mpya hizo. Ndivyo tunavyotaka na sisi.
Pili, kuhusu msimamo mpya wa Prof. Shivji. Pengine kuliko msomi mwingine yeyote wa nchi yetu, Prof. Shivji ndiye mtu ambaye, kwa maisha yake yote, ameandika na kutufundisha juu ya ubovu wa mfumo wetu wa kikatiba na wa kisiasa na umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya na ya kidemokrasia. Kutokea kitabu chake cha Law, State and the Working Class in Tanzania [‘Sheria, Dola, na Tabaka la Wafanyakazi Tanzania’] – tasnifu yake ya uzamivu (PhD thesis) ya mwaka 1982 juu ya mapambano ya wafanyakazi wa Tanzania tangu ukoloni hadi 1964 – mpaka Let the People Speak [‘Waache Watu Waongee’], mkusanyiko wa maandiko yake ya miaka ya ’90 juu ya Katiba Mpya na Mageuzi, msomi huyu maarufu barani Afrika ametufundisha umuhimu wa demokrasia na Katiba Mpya na ametushauri hata namna ya kuipata.
Kabla hata sisi wengine hatujaamka na kuanza kudai demokrasia na Katiba Mpya, Prof. Shivji alikuwa amekwishaianza kazi hiyo muda mrefu, akitumia kalamu yake ya kitaaluma. Kwa hakika, huyu ndiye baba wa kitaaluma wa madai haya. Kuanzia mchakato wa Katiba Mpya ulioanza mwaka 2011, msimamo wake ulianza kubadilika. Kutokea msomi aliyeonesha kwa ustadi mkubwa jinsi ambavyo Tanganyika iliichukua na kuikalia Zanzibar kisiasa kwa kutumia Muungano, aliishia kuwa mtetezi mkubwa wa Muungano kama ulivyo na kama ambavyo umekuwa miaka yote.
Na kutoka mwandishi wa Let the People Speak juu ya haja na namna ya kupata Katiba Mpya na ya kidemokrasia, sasa Prof. Shivji anasema – hata kama ni kwa kudhaniwa (even if impliedly) – kwamba Katiba Mpya haina maana yoyote kwa walalahoi na wananchi wa kawaida. Kitu gani kilichompata mpaka amebadili msimamo wake huu wa miaka yake yote? Mimi sijui.
Kwa sababu ya kazi yake kubwa ya kisomi kwenye masuala haya, Prof. Shivji alitazamiwa na wengi, kuwa sio tu mjumbe bali hata Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kama ilivyokuwa kwa mwalimu wake na msomi mwenzake wa kikatiba wa Kenya, Prof. Yash Ghai. Kwa ujumla, ukilinganisha na mchango wake wakati wa Tume ya Nyalali na baada ya kazi ya Tume hiyo, ushiriki na mchango wa Prof. Shivji katika mchakato wa Tume ya Warioba ulikuwa hafifu sana. Mara nyingi, kama sio zote, alipolazimika kutoa msimamo wake hadharani juu ya mchakato huo, msimamo huo ulikuwa ni wa kuponda zaidi, badala ya kufanya uchambuzi wa kitaaluma aliotuzoesha wakati wa mjadala wa Tume ya Nyalali na katika maisha yake yote ya kisomi.
Ndio maana mimi na rafiki yangu Ismail Jussa, wanafunzi (disciples) wake wa miaka mingi (Shivjites), tulishangazwa na msimamo wake wakati wa Bunge Maalum mwaka 2014 na tulimpinga hadharani. Na ndio maana nafikiri misimamo yake ya sasa juu ya Katiba Mpya inahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa. Kwa hakika, misimamo hiyo ya sasa inahitaji kupimwa na maandiko yake ya miaka mingi kuhusu masuala haya haya.
Hitimisho
Kwa kumalizia, mjadala wa Katiba Mpya unaoendelea haujapuuza maslahi ya walalahoi. Madai ya demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, uwajibikaji, n.k., ni madai muhimu ya walalahoi – na walalahai – kama ambavyo Rasimu ya Warioba na Katiba inayopendekezwa zinavyothibitisha. Wanaodai vinginevyo, kwa kujua au la, ni watetezi wa mfumo wa sasa wa kisiasa na kikatiba unaowakandamiza walalahoi na wananchi wengine wote.
Sisi tunaodai Katiba Mpya ni marafiki, sio maadui, wa maslahi mapana ya walalahoi. Tunataka na wao wawe na sauti katika masuala muhimu ya nchi yetu. Hatutaki waendelee kuitwa walalahoi; tunataka na wao wawe walalaheri!