Dondoo kutoka katika Kitabu cha “CHACHAGE: Uchambuzi wa Sera, Uongozi na Maslahi ya Watanzania” kitakachozinduliwa Mwaka 2010

Wakati wingu la mkanganyiko wa dhana ya utandawazi likiwa bado limeigubika nchi yetu, kuna mjadala mkali katika vyombo vya habari kuhusu lugha ambayo inafaa itumike katika taasisi mbalimbali za elimu. Kuna baadhi ya watu ambao wanaamini kabisa kuwa Kiswahili si lugha ambayo inastahili kutumika katika taasisi hizo kwa kuwa tunaishi katika enzi za sayansi na teknolojia – enzi za utandawazi! Hivyo Kiswahili hakitatusaidia duniani. Kwa maana hiyo basi, Kiingereza si lugha ya kigeni, bali ni lugha ya mataifa yote. Hapa, ukweli kwamba lugha ndiyo kioo cha utamaduni wa umma na ainisho kuu la taifa na watu wa popote pale duniani umesahauliwa kabisa. Hapa ikumbukwe kwamba, utamaduni, kwa ujumla ni mfumo wa maisha ya watu katika umoja wao katika muktadha wa kuyajenga maisha yao na kutokana na mazingira wanayojikuta wanaishi nayo. Vitu kama sanaa, sayansi na taasisi mbalimbali, pamoja na imani na mila ni sehemu ya utamaduni wao. Katika kupambana na maisha na kuyasaka maendeleo, watu wanaibua maarifa na uelewa ambao unawafanya wao watambulike kama watu wa aina fulani. Hivyo hujitokeza katika nyimbo zao, aina aya muziki, hadithi na ngano na muhimu zaidi katika aina ya lugha waitumiayo.

Katika hotuba ya uzinduzi wa Jamhuri ya Tanganyika Bungeni Tarehe 09.12.1962, Mwalimu Julius Nyerere,[1] pamoja na masuala mengine, aliongelea kuhusu historia ya utamaduni wa Tanganyika . Naye alitamka kwamba nchi isiyokuwa na utamaduni wake haina tofauti na mkusanyiko wa watu ambao hawana roho iwawezeshayo kuwa taifa. Alivilaani vitendo vya wakoloni vya au kuwafanya Waafrika waamini kwamba hawana utamaduni wao wenyewe; ama kuufanya utamaduni wa Kiafrika uonekane kitu cha ovyo. Kutokana na hili, wengi wa waliokuwa wamesoma na kupata elimu ya Kizungu walijiona kuwa ni “wastaarabu” na walijifunza kuwaiga Wazungu kiasi kwamba kuwa Mwafrika msomi kulimaanisha kuwa Mzungu Mweusi. Na hili ndilo ambalo taifa letu linashuhudia leo kutokana na huu mjadala wa ikiwa ni lugha ipi inabidi itumike katika taasisi za elimu. Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, hadi leo kuna watu wanaoamini kwamba cha wengine ni bora zaidi kuliko chao. Na hili ndilo dhara kuu la huu ukoloni mpya uitwao utandawazi. Hili linadhihirisha kwamba, kutokana na kutawaliwa kiuchumi na kisiasa, watu wameukubali hata huo utamaduni wa watawala.

Hayo mataifa makubwa ambayo yamekuwa yakizitawala nchi za Kiafrika kiuchumi na kisiasa yanaelewa fika kuwa lugha ni kioo cha utamaduni fulani, na ndiyo maana yamekuwa yakipigania ufundishaji wa lugha zao hususan Kiingereza na Kifaransa. Hawa wanadai kuwa kuna zile ambazo zinaitwa lugha kuu za dunia – na wakati huo huo wanasahau kuwa hata Kiswahili ni moja wapo ya lugh kuu 10 za dunia! Haiyumkiniki kama hayo mataifa yenye kutawala dunia hii yanawaonaje Waafrika ambao wanapiga vita lugha zao wenyewe, wakati mataifa hayo hayo yanaongea na kufundisha kwa lugha zao. Wafaransa, Waingereza, Wareno, Wajerumani, Waswidi, Wafini, Wanorway, Wadenishi, Warusi, Wajapani, Wakorea, Waarabu, Wahabeshi, Wahispania, Wakorea, Wamalay, na mataifa mengi duniani (mengi yao yakiwa na wazungumzaji wachache maradufu ya wale wanaozungumza Kiswahili) hutumia lugha zao katika masomo na nyanja zote kwa ujumla. Israeli ni nchi ndogo sana , kadhalika Wafini hawazidi milioni nane: wote hawa wanatumia lugha zao katika kila nyanja ikiwa ni pamoja na katika taasisi za elimu, bila kuacha kujifunza lugha za wengine. Lakini Watanzania na Waafrika wengi hawaoni kuwa wana haki ya kutumia lugha yao . Watanzania wanaodai kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa dogo na si ya kisasa, ni watu wenye kasumba ya kikoloni ambayo leo hii imejificha nyuma ya pazia la itikadi ya utandawazi.

Sheikh Shaaban Robert aliyewahi kukitetea Kiswahili kwa kughani katika shairi lake maarufu liitwalo “Kiswahili” (Tazama Pambo la Lugha) kwamba “Titi la mama liatamu, hata likiwa la mbwa”, aliandika katika Kielelezo cha Insha (Lugha ya Watu wote Afrika Mashariki) kuwa “Lugha ni alama ya umoja wa taifa”. Hakuishia hapo: “Umoja wa taifa hutaka sana lugha ya watu wote iwe kiungo cha kufahamiana na chombo cha kuchukua watu katika elimu na mapatano.” Alitamka wazi kwamba, japo kuwa kulishawahi kuwepo Kiarabu na Kidachi Tanganyika , lakini lugha zote hizi mbili zilishindwa kuwa lugha za watu wote. Kuhusu Kiswahili na Kiingereza, alikuwa na haya ya kusema:

Kwa bahati mbaya lugha hizi mbili zinakafiliwa sasa kupigana kama chongowe na nyangumi. Wasio Waafrika wanadai Kiingereza kuwa bora nacho kitumike katika halmashauri. Waafrika wataka matumizi ya Kiswahili, kwa sababu kina usawa wa lugha mbali mbali za wenyeji ndani yake. Kwa hivi kina ubora wake ufaao kutumika katika halmashauri pia. Zaidi yake watu wa pande hizi hawana urithi mwingine wa haki kuliko Kiswahili. Katika kila pigano upande mmoja hushinda. Hapana shaka Kingereza kitashinda, lakini yatabiriwa kwamba ushinde wake utakuwa wa kitambo tu. Hayamkini kwamba wenyeji wenyeji wa mahali popote katika ulimwengu waweza kuridhika kuishi katika lugha ngeni milele.[2]

Kadhalika, Shaaban Robert alitamka wazi kwamba “watu wasemao kwamba mafundisho ya Kiswahili hayawezi kuongoza katika elimu na matafiti makubwa”, ni “dhana ya wageni. Wenyeji hawasemi hivi. Hasa wao wana imani kwamba kila mdharau chake ni mwizi. Kwa imani hii washikilia matumizi ya Kiswahili kwa hali iwayo yote. Acha elimu na matafiti makubwa yafasiriwe kwa Kiswahili.” Mbona misahafu na kazi nyingine kubwa kubwa zilikuwa zimefasiriwa? Alitaka Kiswahili kitumike katika kila nyanja. Akahitimisha: “Wakati tunapotumia Kiswahili twaweza kusitawisha uzuri wa lugha nyingine zitufae vile vile.”[3]

La muhimu kukumbuka hapa ni kwamba lugha ya kigeni si lugha ya usawa. Ni lugha ambayo wanaitumia wachache sana katika taifa lolote lile. Kukua na kusambaa kwa kasi kwa Kiswahili kulitokana na ukweli kwamba ilikuwa ni lugha ya ukombozi kwa watu wa Afrika ya Mashariki. Hata maasi ya vijana wa Soweto mwaka 1976 yaliibuka kutokana na kulazimishwa kutumia lugha ya Makaburu (Afrikaner), kwani lugha hiyo iliashiria itikadi na utamaduni wa kigandamizaji na ule wa kuwapendelea wachache. Lakini pia ikumbukwe kwamba tangu enzi za Shaaban Robert, wale waliopigania matumizi ya Kiswahili ni watu ambao hawakuzibeza lugha zingine. Katika “Kila Lugha” (Insha na Mashairi), ubeti wa mwisho unasema:

Lugha kitu kitukufu, hapana nichukiayo,
Kila lugha asharafu, kwangu kwa masaidio,
Lugha zenu nazisifu, yangu nachieni nayo.
Hapana lugha dhaifu, sitatii wabezao.
Lugha yangu taisifu mpaka kukoma moyo.
Ama mwili kuwa mfu, maisha tembe sinayo.

Haya mawazo yalikitokea pia katika Almasi za Mwafrika na Mwafrika Aimba. Baadhi ya beti katika shairi la “Lugha Yetu” (Mwafrika Aimba) zilikuwa na haya:

Hapana lugha damiri, ana yake kila mtu;
Mimi hasa nafikiri, tunachekwa na wenzetu,
Tumo katika ngururi ya kutupa lugha yetu,
Hima pakutane watu au tutahasiri.
…..
Lugha ngeni nakiri, zina manufaa kwetu,
Tujifunze kwa dhamira, tuseme kama upatu,
Walakini tufikiri ubora wa lugha yetu,
Hima pakutane watu au tutahasiri.

Ni wazi kwamba vita dhidi ya lugha za Kiafrika ina historia ndefu. Kibaya kuliko vyote ni kwmba huu mjadala wa lugha inayofaa kutumika katika nyanja mbali mbali, hauzingatii masuala muhimu ya kihistoria na kitamaduni, kitu ambacho kingewezesha watu kumaizi nafasi ya nadharia, itikadi, teknolojia, sayansi, imani, n.k., vitu vianishwavyo na lugha ya watu. Katika mjadala huu, hakuna anayeibua masuala muhimu ya utaaalamu, maarifa, ujuzi, ufahamu na elimu. Bali sasa kujua Kingereza kunaoanishwa na kuwa na elimu, ujuzi na maarifa. Kwa maana hiyo basi, motto wa miaka mitano wa London ni mjuzi zaidi kuliko mzee wa miaka 50 wa China au Afrika asiyejua Kingereza!

Yanajitokeza madai, kwa mfano, kwamba viwango vya elimu nchini vinaporomoka kutokana na wanafunzi kutojua Kiingereza. Wengi wa wale wenye uwezo wanawapeleka watoto wao nchi za nje au katika haya ma academy ambayo yamechipuka kwa kasi ya uyoga nchini. Hapa suala zima la tabia ya usomaji halizingatiwi, kwani inaaminika kwamba mashule na vyuo ndivyo ambavyo hufundisha, na si mwanafunzi kujenga tabia ya kusoma na kujiendeleza. Lakini hata kama ni suala la lugha, ikumbukwe kuwa wataalamu wa mambo ya lugha wamebainisha wazi kwamba inachukua karibia masaa 18,000 mtu kujifunza na kuwa mahiri wa lugha kutoka utotoni hadi ukubwani. Hapa nchini kwetu, Kingereza kinafundishwa kwa masaa kama 800 hivi.

Haiyumkiniki vipi mtu anaweza kuwa na ujuzi wowote ule baada ya kufundishwa lugha kwa masaa hayo. Na huyu ni mtu ambaye amekua huku akiwa na lugha yake ambayo anaifahamu kwa kiasi kikubwa. Hatimaye, mtu kama huyu anaishia kuchanganyikiwa kwa vile anaishia kutokuwa mahiri katika lugha yake mwenyewe, na kadhalika hata ile nyingine anakuwa hajaifamu. Kibaya zaidi anaishia kutokuwa na elimu wala maarifa, kwa vile hana alichojifunza. Kujifunza kwa Kiswahili ni kupata elimu, lakini kujifunza kwa lugha ya kigeni ni kujifunza lugha. Hivi vitu viwili si rahisi kwenda pamoja. Na ndiyo maana wanafunzi huishia kukariri, kwani hawaelewi dhana wanazofundishwa. Mwadamu yeyote ajifunzapo lugha ngeni huanzia kuitafsiri ile lugha kwa lugha yake mwenyewe. Na kadri anavyojua zaidi kuityumia lugha yake, ndivyo anavyokuwa mwepesi kujifunza lugha za wengine. Vipi mtu aweze kuifahamu lugha ya kigeni ikiwa yake wake mwenyewe haifahamu?

Tupende tusipende, Tanzania ni nchi ya Kiswahili katika kila hali. Hata hao wanaodai kwamba Kingereza ndiyo lugha inayofaa hulazimika kutumia Kiswahili wakati wakiomba kura ili wachaguliwe. Wataalamu mbalimbali vijijini na mijini, madaktari, wafanyabiashara,wenye mabenki, n.k. ambao inabidi wakutane na watu wa wakawaida hawana lugha nyingine ya kutumia isipokuwa Kiswahili. Na ni hili lilowafanya hata wamishionari kulazimika kutafsiri misahafu kwa Kiswahili, ama sivyo kusingekuwa na wafuasi wa Ukristo wengi kiasi hiki! Leo hii, Tanzania kuna magazeti mengi kuliko nchi nyingi za Kiafrika kusini mwa janga la Sahara (ukiachia Nigeria , ambako kuna magazeti mengi kwa kuwa hata lugha za Kiafrika zinatumika) kwa sababu ya lugha ya Kiswahili. Hata kampeni za elimu ya watu wazima mnamo miaka ya 1960-70 ziliwezekana kutoka na kuwepo kwa Kiswahili. Hakuna nchi duniani ambayo imeweza kupiga hatua kimaendeleo bila kuwa na lugha yake. Huu ni ukweli usiopingika duniani kote.

Kama ilivyooneshwa katika sehemu ya kwanza ya makala hii, maana halisi ya utandawazi ni kuimarishwa kwa mahusiano ambayo yanawapa nguvu, madaraka na utajiri wachache, wakati mamilioni ya watu wanabakia kufukarishwa, kugandamizwa, kudhalilishwa na kuonewa. Hivyo basi, utetezi wa lugha za kigeni kwa kisingizio cha utandawazi, kihalisia ni utetezi wa mahusiano kama hayo. Yaani wnatetea uendelezaji wa mfumo unawagawanya watu kati ya wafadhili na wafadhiki, waheshimiwa na waishiwa, wenye hisa (stockholders) na washika dau/wadau (stakeholders), walenga na walengwa, wawezeshaji na wawezeshwaji, walaji na walwaji, waelewa wa usasa na wasioelewa, wawekezaji na wawekezwao, wenye mali (mitaji au vitega uchumi) na wenye raslimali, na kadhalika.

Kwa kuhitimisha, ni wazi kwamba hatima ya Kiswahili katika nchi hii ni mbaya kutokana na kuukumbatia ugeni ambao tunakumbana nao usiku na mchana masebuleni na vyumbani mwetu, kwa masaada wa vyombo vya habari (TV, redio, n.k). Kuna nguvu za aina nyingi ambazo zinajaribu kukivunjilia mbali Kiswahili, ikiwa ni pamoja na dhima ya magazeti, majarida na vitabu katika nyanja ya ujengaji hulka ya watu na jumuia. Inasemekana, na baadhi ya watu, kwamba teknolojia ya televisheni inaua siku hadi siku tamaduni za nchi mbali mbali na hata tabia za watu kuyasaka maarifa, na ndiyo sababu hata viwango vya elimu vinaporomoka. Kadhalika, darasani si mahali ambapo wanafunzi hupatia tamaa ya upenzi wa kujifunza na kujisomea ili kupata yale yanayoweza kuujenga utu wao, bali huko hupata mbinu za kushinda mitihani.

Labda kuna ukweli katika madai hayo, kwa wale ambao wamesahau kwamba lugha, utamaduni na elimu ni haki za kimsingi ya binadamu. Labda huo ni ukweli kwa wale ambao wamemeza ndoana ya itikadi ya masoko huria yaliyohinikizwa kwa vipindi maalum na matangazo ya biashara (bia, sabuni, simu ya mkononi, n.k.) kwenye vyombo vya habari na ambayo yanasindikizwa na habari zihusuzo watu wanaokufa kwa njaa, magonjwa au vita. Labda ni kweli kwa wale wanaoamini kwamba hizi ni enzi za uteja na ulaji. Kwani kwa hawa wote, imani yao ni kuwa dunia imefikia enzi za masoko huria, na katika mfumo huu lugha, habari, elimu na maarifa lazima viwe vitu ambavyo ni vya “manufaa” moja kwa moja kwa mtu binafsi tu. Kwa mfano, mtu inambidi asome pale tu anapoona anafaidika—kupata kazi, kufaulu mitihani, kuzawadiwa au kufurahishwa. Kwa hiyo ndiyo sababu watu wengi hupendelea machapisho ya ngono, vitabu vya miongozo mbali mbali, kama vile jinsi ya kutajirika haraka, jinsi ya kufarijika au ufundi, upishi na kadhalika.

Lakini, kihalisia, huo ni uzushi mtupu. Ukweli ni kwamba taifa na dola vimepooza nguvu zake kwa sababu ya kuyaachia madaraka na nguvu masoko, na katika hali hiyo, hata uzalendo na utaifa umekufa[4] na uteja na ulaji ndivyo ambavyo vinashamiri. Sasa mteja na mwekezaji ni watu wa maana kuliko mtu wa kawaida. Leo inachukua nafasi ya jana na kesho. Hivyo historia imeuawa na watu wanaishi bila mbele wala nyuma. Matamanio ya maisha mema ya mwandamu na mitizamo ya maisha adilifu inabetuliwa pembeni, huku ndoto za watu binafsi zikitukuzwa. Na ni kwa sababu hii mifano ya watu mashuhuri—wale “walioukata”, matajiri, inatamanisha na kuvutia zaidi kuliko nadharia au mifano ya wasomi wanaojaribu kuwashawishi watu kwamba maarifa, elimu na kufikiri ni mambo ya msingi kabisa katika maisha.

Vyombo vya habari katika hali kama hii vinaugeuza hata utamaduni kuwa ni suala la matukio ya watu fulani fulani, badala ya kioo cha maisha ya watu katika mahusiano yao na mapambano ya kuyasaka maisha yaliyo bora na ya ufanisi. Kiu ya kupata elimu na maarifa inageuzwa kuwa ushabiki wa kuwafahamu watu maarufu. Leo hivi, ufadhili umegeuka kuwa sera, badala ya maadili na itikeli zilizojikita katika uwezo wa kujitegemea kifikra. Utawala bora umekuwa ndiyo mbadala wa uongozi bora na adilifu. Ni katika hali kama hiyo ndipo tunashuhudia hata kilicho chetu, kwa mfano lugha ya Kiswahili, ikipigwa vita na watu wa nje na wandani.

Lakini bado wako wale ambao wangali wakiamini kwamba utamaduni wa watu (pamoja na lugha kama Kiswahili) ni nyenzo muhimu ya binadamu. Toka enzi za akina Muyaka, akina Shabaan Robert, akina Mathias Mnyampala, akina Akilimali Snowhite na hata viongozi waliopigania uhuru wa nchi hii—mfano mzuri ukiwa ni ule wa Mwalimu Julius Nyerere, kumekuwepo walinzi wa Kiswahili na tamaduni zetu. Wamekuwa watu ambao wameutukuza umuhimu wa kufikiri, kama ainisho la ubinadamu wetu. Wamekuwa wapenzi wa maandishi mazuri yenye vionjo na busara, ambayo licha ya kuusifu ubinadamu wetu, kadhalika yameukosoa kwa nia ya ujenzi wa maadili na ya ujenzi wa ulimwengu usiokuwa na madhila, mazonge, unyonyaji na ugandamizaji. Kiswahili kitaimarika zaidi kwa kuziumbua mbinu mbali mbali za huu mfumo wa utandawazi, ambao unatishia kutokomeza historia ya upiganiaji wa haki za kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kisiasa. Kwa kujipambanua na matamanio ya walio wengi ambao ndio hasa watumiaji wa Kiswahili, lugha hii haitaangamizwa na hao wachache wanaoushabikia utandawazi na ugeni kwa ujumla.

——————————————————————————–

[1] J.K. Nyerere, Freedom and Unity, Oxford University Press, Dar es Salaam , 1967, uk . 186-7. [2] Oxford Univerity Press, Nairobi , 1966, uk . 101.[3] Kama juu, uk . 102.[4] Uzalendo na utaifa si vitu muhimu tena katika hizi enzi zetu, badala yake ni uraia (haijalishi kama unauza nchi au hujali maslahi yake!). Uzalendo na utaifa katika enzi zake viliweza kuwatambulisha Waafrika kama watu waliostahili heshima na haki.