CHUMBIA BINTI MPENDA VITABU
Hii ni kwa vijana wanaopenda kuoa! Ukitaka kuoa, chumbia Binti Mpenda Vitabu ( BMV)
Kwa nini? Wa kazi gani? Utampata wapi?
Unaweza kumpata Maktaba akihangaika na vitabu vyenye vumbi na harufu kali ichomayo puani; vitabu ambavyo vimeuvaa uajuza na ushaibu kwa kutofunuliwa siku nyingi. Waweza pia kumkuta kwenye maduka ya vitabu akinunua vitabu. Ukisikia kuna uzinduzi wa kitabu sehemu au mjadala wa Kitabu Nilichosoma, Jongea maeneo hayo kwa vile BMV hawezi kukosa! Nenda tu hata kama hupendi vitabu!
Ukibahatika kukutana naye kwenye daladala, yu nawe siti ya jirani, lazima atakuwa kashika kitabu. Usishangae kwa nini hakusemeshi; kitabu humtia mtu upofu asione cha jirani. Tafadhali, usimsemeshe mambo yasiyo na kichwa wala miguu; mara ‘dada habari’; ‘waitwa nani’? waenda wapi?. Hutopata mwitikio mzuri. Kama wataka kumnasa, msalimie kisha zungumza naye kuhusu kitabu; ’’Samahani, hii ni fiction au non-fiction?’ ‘’Yaelekea ni kizuri eeeh?’’ ‘’Kinahusu nini? ‘’ BMV hupenda kuulizwa mambo ya vitabu. Jitahidi kadiri ya uwezo wako mazungumzo yako yajikite kwenye vitabu. Tupa ndoano kwa kuazima kitabu; atakupa namba ya simu. BMV hupenda wapenda vitabu.
Endelea kuwasiliana naye. Nakusihi, kwenye mazungumzo yenu, habari ya vitabu iwe mbele. Mchunguze kuhusu vitabu avipendavyo. Aweza kuwa mpenzi wa fasihi. Naam, tuchukulie ni mpenzi wa fasihi. Basi jitahidi ujikite hapo.
Ni siku yake ya kuzaliwa. Unapanga kumfanyia nini? Keki? Kadi? Unasema unataka kumnunulia simu ya kisasa halafu umpeleke outing pale Samaki Samaki au Del Monte? Haya yote ni mazuri lakini hayataukosha vilivyo moyo wa BMV. Ngoja nikueleze. Unakifahamu kitabu kipya kilichotoka karibuni? Yaweza kuwa umekwisha msikia akikitaja kwamba kikiingia madukani atakinunua. BMV hutumia sehemu ya pesa yake kununua vitabu. Basi chunguza kama hajakinunua. Nenda kakinunue kisha kiweke kwenye bahasha nzuri.
Mwambie kwamba ungependa kutoka naye outing. BMV hupenda pahala tulivu. Mpeleke ufukweni au Soma Book Cafe kwa Demere Kitunga . Amini nakuambia, atafurahi mno kuliko unavyodhani. Zungumza naye. Kumbuka nilivyokuhusia, mazungumzo yenu yahusu vitabu. Kisha m-suprise kwa zawadi. Mweleze afumbe macho…eeh unataka kumvisha pete? Acha kabisa! Usifanye hivyo sasa; haraka haraka haina baraka. Toa kitabu ulichonunua kutoka kwenye mkoba wako kisha kiweke mezani. Mwambie kuna zawadi yake mezani na kwamba aotee ni zawadi gani. Usidhani ni mbashiri akipata; BMV ametawaliwa na vitabu kichwani.
Mwambie afumbue macho kisha achukue zawadi yake kwenye bahasha. Akifungua na kukuta kitabu chenyewe ni kile akipendacho, tarajia maneno matamu toka kinywani mwake! Usishangae, BMV huthamini vitabu kuliko chochote.
Acha siku hiyo ipite. Siku nyingine, muombe msome kitabu pamoja au akusimulie kitabu chake pendwa. Fanyeni haya ufukweni. Siku hiyo, waweza kumueleza kiu yako; kiu ya kuwa naye maishani. Usidhani maneno yako matamu yatamduwaza; ameshasoma mengi. Ameshasoma vitabuni ahadi za wanaume wanaoahadi kutoa milima na mito wakikubaliwa au wale wanaoahidi magari huku wangali makapuku wa kutupwa. Ameshavisoma visa vya wanaume vinga’ng’anizi. Au umesahau kile kisa cha Mmbu king’anganizi alichowahi kusimulia Chinua Achebe? Ngoja nikukumbushe!
Hapo kale Mmbu alimpenda sana sikio (sikio hilihili lililo mwilini mwako). Basi Mmbu akamwendea sikio na kumweleza kuhusu pendo lake kwa sauti ibembelezayo kwa huba. Mrembo sikio kusikia maneno ya Mmbu akadondoka chini kwa kicheko. Kisha akarudi pahala pake na kumwambia Mmbu kwa dharau. ‘’Wewe mbu kiumbe unayeishi kwa wiki moja kisha ukaondoshwa na kifomithili ya mkulima ang’oavyo magugu ndiyo unipose mimi! Unataka kuniacha mjane halafu anioe nani?’’
Mmbu alijaribu kumbembeleza sikio bila mafanikio. Hoja ya sikio ilikuwa ile ile: kwamba Mbu ana maisha mafupi. Basi Mbu akasema kwa huzuni..’’Hao waliokuambia kuwa nina maisha mafupi wamekuongopea, nitakuthibitishia hili’’. Basi ikawa kila siku Mmbu anakuja sikioni kwa binadamu na kumweleza sikio kwamba bado yu hai. Hata sikioni mwako bila shaka hufika kuendeleza ushawishi wake kwa mnyange sikio. Ni kwa sababu hujui lugha ya Mmbu ndiyo maana unadhani amekuja kukupigia kelele tu! Akija kwa binadamu yoyote, iwe amelala au yu macho, lazima aje kwanza kwa binti sikio kumsalimu. ‘’Ewe sikio kipenzi, tazama nipo hai, nikubalie’’ Kweli Mbu king’ang’anizi!
Kwa hiyo ukiwa na BMV, jua visa vyote hivi amekwisha visoma! Habari ya kumuota mtu ndotoni au kumuona kwenye glasi achana nayo! Maneno haya yaseme ukiwa na wasichana wengine, si BMV! Mweleze kwamba unampenda. Akikuuliza kwa nini, mweleze unapenda kila kitu chake. Usisahau kusema pia unaipenda tabia yake hasa kupenda kwake kusoma vitabu. Hapa BMV atafurahi sana. Furaha yake ni vitabu.
Akikubali, anza uhusiano wa kimapenzi. Jitahidi nawe uanze kupenda vitabu taratibu. Akikuuliza unamjua Shaaban Robert usikimbilie kusema ni shule ya sekondari; sema ni nguli wa fasihi. Akisema kuhusu Andanenga usije dhani ni jina la mzizi fulani; huyo ni malenga mashuhuri almaarufu kama ‘’Sauti ya kiza’’.
Muoe. Kama ndiyo kwanza mnaanza maisha, m-surprise kwa kumnunulia kabati jipya la vitabu. Mkijenga nyumba, usisahau study room, chumba cha kujisomea. Usishangae usiku akiwa kwenye usingizi mzito akagumia ndotoni ’’usimuuue usimuuee!’’. Hakuna haja ya kumwamsha; jua anaota ya vitabuni!
Ukirudi nyumbani halafu ukakuta bado hajapika chakula usimfokee wala kumpiga, hiyo ndiyo raha ya BMV. Nenda alipo, yaweza kuwa chumbani kajilaza na kitabu mkononi au nje kwenye bustani akisoma kitabu! Kwa BMV, vitabu ni popote! Msogelee karibu kisha soma naye hadithi, namaanisha kula naye hadithi kwa sababu huo ndiyo mlo mkuu wa BMV.
Ukiishi na BMV jua haupo peke yako. Mpo waume wawili; wewe na vitabu. Usimuonee wivu mume mwenza kwa sababu kila mmoja ana jukumu la kumfisha BMV kwenye kilele,
Kilele kilojaa raha
Kilele kiso karaha
Kilele chenye furaha
Akawa hajitambui
Hajui yupo ndotoni
Au kapaa mbinguni
Ala raha za peponi
Mrembo hajitambui
Ado Shaibu ( Komredi wa Malenga )
………………………………………………..
NOTE: Tangu kuandikwa kwa mara ya kwanza kwa makala ya ‘’Don’t Date a Girl Who Reads’’ ya Charles Warnke, makala nyingi zaidi zimeandikwa kuchukua upande wa mwandishi au upande tofauti. Niliandika post hii baada ya kusoma makala ya Jennifer Souter iitwayo ”You Just Date a Girl who Reads’’.
Kwa wale wapendao kusoma makala zaidi kuhusu mjadala huu pitieni kwenye links zifuatazo:
Why You Simply Have to Date a Girl Who Reads | Jennifer Soutar
Don’t date a girl who reads — Charles Warnke – think thank thunk
You Should Date An Illiterate Girl | Thought Catalog
Angalizo: Unaposoma links hizo kumbuka, fasihi ndiyo iliyoutawala mjadala.
Nimependa hii post japo sikumbuki ni lini niliisoma. Ni kweli vitabu humfanya mtu asiangalie mambo ya kijinga bali ya maana na makubwa. Hupanua mawazo na kujenga kujiamaini kwa namna yake.
Wow, umetupatia 💯! Mimi nimeanza kupenda vitabu nikiwa na miaka 12, na haipiti siku sijasoma. Nina study room, shelves zimejaa, nina vitabu vingine kwenye kqbati la nguo😅😅. Imebidi mume wangu anishauri ninunue tablet kwa ajili ya kusoma ili kuikoa nafasi.