UMOJA WA WANAOTAKA TANGANYIKA:
Ni umoja wenye mashaka. Ndani yake wapo wanaotaka Tanganyika
ndani ya Muungano wa Kishirikisho wa Serikali Tatu. Lakini pia wapo ambao
hawaitaki Zanzibar, eti imewachosha.
Wote wakishapata wanachokitaka – yaani Tanganyika, umoja wao
utavunjika. Wasioitaka Zanzibar watadai Muungano uvunjike. Wanaotaka Muungano
watajikuta na Tanganyika tu.
Lakini hiyo Tanganyika ina uhakika gani itakuwa na umoja? Falme
na Uchifu wa zamani ukitaka nchi zao itakuwaje? Au mikoa/kanda kutaka kujitenga
au kujiunga na nchi jirani?
Tanzania ni nchi tuliyoijenga kwa taabu sana. Ujenzi wa miaka 50
unaweza kubomolewa kwa siku 50 tu. Nchi hujengwa na wenye moyo na umoja ni
nguvu, utengano ni udhaifu.
MADARAKA NA MUUNDO WA MUUNGANO:
Hili suala naliangalia kwa macho ya uchambuzi wa kimadaraka
(power analysis) zaidi na sio kwa mapenzi tu ya kutaka tu kitu kiwe au kwa
uchambuzi wa kimuundo (structural analysis) tu. Tatizo lilipo kimadaraka ni
kuwa kwa kiasi kikubwa Zanzibar/Wazanzibari hawataki uwiano tenge wa madaraka
ambao unatokana na Serikali ya Muungano kuwa na mambo mengi ya Muungano maana
kwao ni sawa na Tanganyika kuvaa koti la Muungano.
Tanganyika/Watanganyika, kama ambavyo nimesema awali, kwa
sasa wana umoja wa mashaka maana hivi leo kinachowaunganisha ni kutaka
Tanganyika: Humo wamo wanaotaka Serikali Tatu ili Tanganyika iwepo tu, sio kwa
sababu wanataka Muungano; pia wapo wanaotaka Muungano wa Serikali Tatu kwa
sababu wanadhani ni suluhisho la kero za Muungano na humo humo wanaotaka hivyo
kwa sababu wanaona wanaibeba Zanzibar na imekuwa mzigo; lakini pia wanaotaka
Tanganyika bila Muungano, hivyo kupata Tanganyika kwao ni hatua ya kwanza
kuelekea kuvunja Muungano. Pia kuna hili kundi jipya ambalo linadhani eti
inawezekana kuwa na Serikali Tatu bila kuwa na mfumo wa kishirikisho kana
kwamba wenzao wanaotaka Tanganyika wanaitaka iwe tu kama Serikali za Mitaa
ambazo mpaka leo zinalalamika kuwa Serikali Kuu haigatui/haipeleki madaraka
ngazi za chini.
Hili ni suala la mgawanyo wa madaraka (power) zaidi kuliko
muundo (structure). La watu zaidi ya taasisi. Ndiyo.
KUUNGANISHA SERIKALI, NCHI NA DOLA-NCHI:
Rais kaelezea vizuri kabisa kwa nini hatuwezi kuwa na
Serikali 3 kwa maana hasa ya Serikali Kuu (Central Government). Hii dhana ya
Nchi Moja, Dola Moja na Serikali Tatu ingeweza kufanya kazi tu kama maana ya
Serikali Tatu hapa ni Serikali za Mitaa Mbili (Local Goverments) na Serikali
Kuu Moja jambo, ambalo nalo haliwezekani kwa sababu Zanzibar haiwezi kukubali
kuwa na Serikali hiyo yenye hadhi ndogo kiasi hicho.
Mchakato wa ugatuzi wa madaraka i.e. kupeleka madaraka katika
ngazi za chini umeshindwa kwa sababu kwa kawaida Serikali Kuu haitaki/haikubali
kuziachia Serikali za chini madaraka. Lakini katika hizi Serikali Tatu
zinazopiganiwa sasa ukweli, kama Rais alivyouelezea vizuri sana, ni kuwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa haina nguvu/madaraka ukilinganisha na
Serikali za Washirika hasa huyo Mshirika mnayemdai ambaye atakuwa ni zaidi ya
Kaka Mkubwa, si kwa Zanzibar tu ila hata kwa Tanzania pia, yaani Tanganyika. Uchambuzi
wa madaraka (power analysis) ni muhimu sana katika suala badala ya kuleta dhana
za kidhahania na matamanio ilhali hazifanyi kazi nje ya makaratasi. Serikali
kwa Maana ya Serikali Kuu hujiendesha ikiwa na nchi na dola.
Kanuni za kuunda Dola Moja (Unitary State) ziko wazi kama
ambavyo kuunda Dola Shirikisho (Federal State) zilivyo. Ukiwa na nchi moja
kubwa inaungana na nchi ndogo Dola Shirikishi na Dola Moja zinawezekana tu kwa
kuipa nafasi ya upendeleo nchi ndogo. Hali inakuwa tofauti unapokuwa na nchi
nyingi, ndogo na kubwa, zinazoungana ambapo mgawanyo wa madaraka na rasilimali
unakuwa na uwiano mpana (stretched). Hapo unaweza kuamua kuwa na Dola
Shirikishi la nchi kadhaa au Dola Moja inayoamua kujiendesha kwa majimbo
kadhaa. Hili la pili linawezekana kama Tanzania Bara itakubali kujivunjavunja
na kuwa na majimbo makubwa kama manne yatayoungana na Zanzibar (kama
Wazanzibari watakubali) na hivyo kutokuwa na Kaka Mkubwa anayeitwa Tanganyika.
Hatari yake ni kuwa hayo Majimbo 5 yenye uwiano mpana wa madaraka ya kisiasa na
kiuchumi yanaweza yakavunja nchi kama utaifa wa Tanzania hiyo hautaweza
kujengwa na badala yake watu wakawa wanajenga utaifa wa hayo majimbo yao. Lile
la kwanza litawezekana wenzetu wa Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Sudani Kusini wakikubali tuungane. Ila naona ni kama
vile tuna haraka sana na kusahau kuwa Serikali Mbili ni mpito tu wa kuelekea
kwenye Umoja Mkubwa.
Tusifanyie mzaha suala la kupangua nchi, dola, na dola-nchi
iliyojengwa – inahitaji uhakika sio majaribio tu.
WARIOBA (1994):
Kama Zanzibar ikikubaliwa kuwa na
madaraka zaidi katika mambo kama uraia, ulinzi na usalama, mambo ya nje na
uhusiano wa mataifa, viwanda, biashara, hali ya hatari, posta na simu, kodi na mabenki,
Tanganyika nayo itapewa madaraka hayo hayo … Matokeo yake Serikali za
Tanganyika na Zanzibar zitakuwa na nguvu sana na Serikali ya Muungano itakuwa
dhaifu kabisa. Mambo yanayobaki yatafanya Muungano uwe dhaifu kuliko
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ilivyokuwa. (Warioba (1994: 17) Tanzania: Hatima ya Muungano)
http://www.checheafrika.org/kutoka-makavani-kwa-nini-muundo-wa-shirikisho-utaua-muungano/
WARIOBA (2011):
Wakati wote kwa mwananchi wa kawaida, kumekuwa hakuna
matatizo ya Muungano. Matatizo yanatoka kwenye midomo ya viongozi.
Shughuli za wananchi wa kawaida haziangalii orodha ya mambo
ya Muungano, bali haki yao kama raia. Wanajiona ni raia katika shughuli zao za
kibiashara au nyingine. Mwananchi wa kawaida anaona anayo haki ya kufanya
biashara mahali popote. Wananchi wamezoa hivyo. Msiwafikishe mahali wakajiona
kuwa kwenda Zanzibar au kuja Bara inabidi wafuate taratibu za kwenda Kenya au
Uganda.
Tunayo matatizo ya madaraka, kwamba unazo Serikali mbili kwa
hiyo yale yaliyomo kwenye orodha ya Muungano ni kuonyesha Serikali hii ina
madaraka gani. Wanagombania madaraka.
Kama suala ni mafuta au mengine tuzungumze. Inategemea
mnavyokubaliana, tusije kuongeza au kupunguza kwenye orodha mambo ambayo
yatakuja kuwatenganisha wananchi. Kama kwa mfano, kuna watu wanafikiri
kuimarisha Muungano ni kuwa na serikali tatu, unaimarishaje?
Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu
hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho
wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote.
Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na
wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya
nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi?
Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika
na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa.
Lakini tukivunja Muungano madhara yake ni makubwa sana kwa
pande zote mbili. Mimi naamini wale wanaotaka serikali tatu wanajua nia yao ni
kuvunja Muungano na huu ndio ukweli. Ukianzisha serikali tatu, maana yake
unavunja Muungano.
WARIOBA (2014):
Hiyo haina maana kwamba kila mmoja wetu ameacha imani yake,
itikadi yake na msimamo wake. Kuna mambo ambayo kila mmoja wetu amebaki na
imani yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini
muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini Muundo wa Serikali Mbili, tupo
tunaoamini Serikali Tatu na tupo tunaoamini Muungano wa Mkataba.
http://www.wavuti.com/2014/03/hotuba-ya-rasimu-ya-katiba-mpya.html

