Wakuu
Muhidin J. Shangwe
Imeibuka tabia, ya kuitana Wakuu
Ishakuwa kuu kadhia, hadhi kuwekana juu
Nijuze wapi lianzia, neno la wakati huu
Limeenea mitandaoni, kila mtu Mkuu!
Ujuzi sifa yao, kila jambo walijua
Mtandaoni ndo’ kwao, japo pote huyazua
Zamani na mamboleo, Wakuu wasochagua
Nabaki na moja swali, heshima au kujitutumua?
Wakuu mmetanabahi, kwamba fulani fisadi
Kigogo mpiga dili, ramli kwa ripoti ya Assadi,
Tena mwapiga zumari, Si wa kwanza wala pili,
Nazongwa kujiuliza, Wakuu ’kina nani?
Wakuu twashukuria, kwa wenu uzalendo
Habari kutupatia, japo maneno si vitendo
Nasi twaaminia, kuupenda wenu mtindo
Habari hizi nyeti, Wakuu mwazipata wapi?
Imekuwa kama desturi, kwa hizi mpya zama
Kwa ubaya na uzuri, utukufu kuuparama
Japo matendo sifuri, kutwa kucha kulalama,
Waungwana kuitana Wakuu, ni heshima au woga?
Kaditama mefika mwisho, melonga pasi ficho,
Kweli yaja mwisho,Tena haihofu tisho,
Hongeraye mvunja zungusho, Tena pasi fukisho,
Kifiwacho Kiswahili, au fikiri za Waswahili?