Na Ado Shaibu (@AdoShaibu)
Moja tisa sita saba, kawakusanya Arusha
Wa taifa yeye baba, Azimio kufundisha
Wanafunzi kwa mahaba, wakajibu kwa bashasha
Zidumu fikira zako, hiyo ndo’ kauli yao
Tuache kuombaomba, si heshima asilani
Nje hatuna mjomba, sasa bakuli la nini?
Tuivunje hi kasumba, kawafunda hadharani
Zidumu fikra zako, Hiyo ndo’ kauli yao
Kwenu cheo ni dhamana, jiepusheni vituko
Musijivike ubwana, kutawala kwa viboko
Rushwa semeni hapana, nyie ishikeni miko
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Tumenyonywa vya kutosha, mapinduzi sasa yaja
Kupuuzwa metuchosha , jikomboa iko haja
Ukoloni umekwisha, sasa tukate mirija
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Kila alowafundisha, wakaitika tawile
Vichwa wameinamisha, mithili ya misukule
Nani angeweza bisha, akadumu zama zile?
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Lipoitwa na Kadima, walikwenda Butiama
Walilia njia nzima, wanafunzi kalalama
Nyota yetu umezima, ona jahazi lazama
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Palepale msibani, wote wakala yamini
Alowapa darasani, tayashika maishani
Tayahifadhi moyoni, toyaacha asilani
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Mwalimu wanamuenzi, midomoni jakauka
Kwenye nyumba na mabenzi, picha zake mebandika
Kwa kuonyesha mapenzi, redioni wanamweka
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Kila moja anamwenzi, hakuna aliyemwacha
Majahili wanamwenzi, hakuna aliyemwacha
Wasafi wanamuenzi, na walafi jamuacha
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Ulo ujinga wa jana, wao meukumbatia
Na yale yaliyofana, ajabu wanabomoa!
Wanafunzi mekazana, urithi kujimegea
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
Wanamuenzi mwalimu, kwenye makampuni yao,
Wanamuenzi mwalimu, kwenye makasri yao,
Wanamuenzi mwalimu, kunako migodi yao
Zidumu fikra zako, hiyo ndo’ kauli yao
© Ado Shaibu-Komredi wa Malenga