Katika kipindi cha miaka takribani mitatu sasa dhana ya uzalendo (na mzalendo) imepata umaarufu sana miongoni mwa Watanzania hasa viongozi wa kisiasa. Ninadhani umaarufu wa dhana hii unaweza kuwa umekaribia ama kulingana na ule wa dhana ya ufisadi (na mafisadi) ambayo ilikuwa maarufu sana katika kipindi cha karibu muongo mmoja na nusu kabla ya dhana ya uzalendo kushika hatamu. Katika tafakari hii fupi ninaangalia nini hasa maana (ama tafsiri) ya dhana hii ya uzalendo (na mzalendo) katika muktadha mpana wa maendeleo ya watu.

Hoja yangu ya msingi ni kwamba maana ya dhana ya uzalendo imebadilika sana siku za hivi karibuni na kupewa tafsiri mbalimbali zinazojikita katika misingi ya mitazamo ya kisiasa baina ya wanasiasa na wananchi, nafasi ya kiuchumi ya makundi mbalimbali katika jamii, na vigezo vingine vya kijamii kama utaalamu na taaluma. Nitaanza kwa kuelezea japo kwa ufupi tafsiri niliyonayo ya dhana ya uzalendo. Kisha nitajaraibu kufafanua hoja yangu ya msingi.

Uzalendo unatafsiriwa kama dhana/hali ambayo mtu ama watu fulani wanakuwa na mapenzi ya dhati na taifa lake/lao na yuko/wako tayari kwa lolote ili kulitetea taifa hilo kwa dhati na bila woga wala kificho (tafsiri yangu). Hii ni tafsiri ambayo nimeifahamu kwa muda wote. Sina shaka ndiyo ambayo wengi wanaifahamu.

Pamoja na hilo, uzalendo unaweza kutafsiriwa kama dhana ya uzawa; nikimaanisha ile sifa ya kuzaliwa katika taifa fulani. Kwa mfano, tafsiri hii nimekuwa nikiisikia ikitumika sana katika maelezo yanayotolewa na viongozi juu ya ujenzi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo…. “mradi huu umebuniwa na kujengwa na wazalendo”. Tafsiri hii humaanisha mambo makubwa mawili (kwa maoni yangu): kuonesha dhana ya uzawa/asili ya wataalamu waliotekeleza mradi husika au kufanya jambo fulani kubwa la sifa; maana nyingine ni kuidhihirishia jamii na hata jumuiya ya kimataifa kuwa na sisi kama taifa tunao uwezo wa kusimamia na kufanya mambo makubwa.

Wakati nikiitazama tafsiri ya kwanza kama iliyo sahihi na kamilifu na hivyo kuitumia kama tafsiri rejea katika tafakari yangu; tafsiri ya pili ninaitazama kama ishara ya mwanzo kabisa ya kubadilika kwa dhana nzima ya uzalendo. Hii naweza kuifananisha na zile zama za uzawa na wazawa za Mzee Iddi Simba. Kadhalika, nimetumia mfano wa miradi ya maendeleo kwa makusudi kabisa nikielewa kuwa hili ni eneo ambalo dhana ya uzalendo imekuwa ikitumika sana kama nitavyofafanua hapo mbele. Baada ya kuweka msingi wa tafakari yangu sasa nitajikita katika kufafanua hoja yangu ya msingi.

Ni dhahiri kuwa dhana ya uzalendo imekuwa ikitumika katika nyanja ya siasa za Afrika (ikiwemo Tanzania) kwa muda mrefu. Nakumbuka nikiwa mtoto wa shule ya msingi, mwishoni mwa miaka ya themanini na mwanzo mwa miaka ya tisini, harakati za ukombozi kule kusini mwa Afrika zilikuwa zimepamba moto. Wakati ule tulikuwa tukisikia maneno kama mashujaa na wazalendo wa Afrika yakihusishwa na harakati zile na vinara wa harakati hizo kama Mwalimu Julius Nyerere na Nelson Mandela.

Tangu wakati ule nilielewa uzalendo kama hali ya kupigania haki zako na za wale unaodhani ni wenzako bila kujali tofauti (rangi, kabila, jinsia, n.k) miongoni mwenu. Hivyo, basi ieleweke kuwa matumizi yake katika siasa si jambo jipya hata kidogo bali tafsiri mpya za kisiasa ambazo zimeongezwa katika dhana ya uzalendo.  Ninadhani dhana hii siku hizi imekuwa ikitumika hasa katika mashindano ya kisiasa baina ya vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Tafsiri mpya (ya uzalendo) ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika kauli nyingi za wanasiasa hasa wa chama tawala (Chama ambacho kimetawala nchini Tanzania Tangu Uhuru kikiitwa TANU na baadaye CCM baada ya muungano kati ya TANU na ASP) ni zile zinazoashiria kuwa uzalendo na kuwa mzalendo ni pale tu mtu anapokuwa mfuasi au muungaji mkono wa sera za chama tawala. Kutokana na kushamiri kwa tafsiri hii mpya, vyama vya upinzani na wafuasi wao wamekuwa wakijengewa picha kuwa wao ni wapinga maendeleo (yanayofanywa na chama tawala) na hivo kukosa uzalendo kwa nchi yao. Wakati chama tawala kimekuwa kikijitanabaisha kama cha kizalendo (na wafuasi wake kama wazalendo), vyama vya upizani, viongozi wake na wafuasi wao wamekuwa wakionekana kukosa uzalendo eti kwa sababu wao wanapinga tu.

Baadhi ya wanasiasa wa upinzani, kwa mfano Mhe. Tundu Antiphas Lissu (MB) (mwanasiasa machachari wa upinzani na mwiba kwa chama tawala nchini) si tu wamekuwa wakishutumiwa kwa kukosa uzalendo bali hata kuhusishwa na hila za mabeberu za kuididimiza Tanzania. Kwa hali ya kawaida kitendo kama hiki (endapo tuhuma hizi ni za kweli) ni kukosa uzalendo kwa hali ya juu. Swali la msingi ambalo najiuliza hapa ni: je, uzalendo maana yake ni kuwa mfuasi wa chama tawala na kuunga mkono pasi na kudadisi, kuhoji na kutafakari yale kinachosimamia?

Uhusiano kati ya siasa za vyama vingi na tafsiri ya uzalendo hauishii kwa wanasiasa peke yao bali na kwa wafuasi na wapenzi wa vyama na viongozi wake. Ni katika muktadha huu ambapo tumeanza kushuhudia kuibuka kwa matabaka ya wazalendo na wasio wazalendo. Hii ni kufuatana na upande upi wa jamii unaunga mkono chama na mwanasiasa gani kati ya chama tawala (cha kizalendo) na vyama vya upinzani (visivyo vya kizalendo).

Kwa mfano, katika chaguzi za ubunge na madiwani zinazoendelea kutoka na wimbi la wanasiasa wa upinzani waliokuwa na nafasi za kuchaguliwa kuhamia chama tawala, zimeanza kusikika kauli za wanasiasa kutoka chama tawala wakiwatahadharisha wananchi kutowachagua wanasiasa wa upinzani. La sivyo wataadhibiwa kwa kunyimwa maendeleo. Kumbe kwa nyakati hizi unaweza kuwa mzalendo kwa sababu ya kuunga mkono chama tawala na viongozi wake na kuonekana kukosa uzalendo endapo unaunga mkono vyama na viongozi wa upinzani, na pengine kuadhibiwa kwa kukosa uzalendo.

Katika hali inayofanana kwa karibu na niliyoielezea hapo juu ni kuhusishwa kwa masuala ya kitaalamu/taaluma na dhana ya uzalendo. Ni ukweli usiopingika kuwa utaalamu ni kiungo muhimu katika kusukuma mbele gurudumu la maendelo kwani mipango ya maendeleo na utekelezaji wake vinategemea sana wataalamu katika fani/taaluma mbalimbali. Katika eneo hili tafsiri nyingine ya uzalendo imeanza kuibuka hasa pale ambapo wataalamu wanaingia katika mgongano na wanasiasa (watawala).

Jukumu na lengo la mtaalamu ni kufanya jambo kwa kuzingatia miiko na taratibu za taaluma yake. Kwa upande mwingine lengo la mwanasiasa/mtawala ni kutekeleza yale aliyoahidi ama anayodhani yanawafaa wapiga kura wake. Hivyo basi, kufanya kazi pamoja baina ya makundi haya mawili ni suala lisiloepukika.

Changamoto huja pale ambapo makundi haya mawili yanaposimamia misimamo inayokinzana: mtaalamu kusimamia taaluma yake na mwanasiasa/mtawala kusimamia sera zake. Katika hili, misimamo ya wataalamu katika miiko ya taaluma zao imeanza kutafsiriwa na watawala na wanasiasa kama hali ya kukosa uzalendo. Si jambo la kushangaza, kwa mfano, kusikia mwanasheria akishutumiwa kwa kukosa uzalendo eti kwa sababu tu anamuwakilisha mtuhumiwa wa ufisadi.

Katika nyanja ya uchumi pia pamekuwepo na matumizi (ninayodiriki kuyaita mapya) ya dhana hii ya uzalendo. Hivi karibuni kumekuwa na msukumo mkubwa wa wananchi kulipa kodi na kujenga mazoea/tabia ya kupenda kufanya hivyo. Hili ni jambo la msingi kabisa na la kuungwa mkono ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya watu. Ulipaji kodi ni kigezo kikubwa kwa sasa cha kupima uzalendo wa watu kwa nchi yao. Katika hili kuna mtazamo ambao umeibuka kuwa kulikuwa na ukwepaji wa kodi uliokithiri hapo nyuma hasa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa katika sekta binafsi. Pia katika hili kumeibuka na kasumba ya kuwaona watuhumiwa wa ukwepaji kodi hasa matajiri kama watu wasio na uzalendo na nchi yao.

Pamoja na kwamba ni vigumu kwa mwananchi kukwepa kabisa kulipa kodi swali la msingi hapa ni: je, wananchi wengi ambao wako katika mfumo usio rasmi wa kuichumi (na hivyo kutolipa kodi moja kwa moja, kwa mfano, kodi ya mapato) nao si wazalendo? Ikumbukwe kwamba kuwepo katika mfumo usio rasmi wa uchumi nako kunahusishwa na dhana hii kwa zile lugha za “unyonge na umaskini” kwa upande mmoja na “utajiri na ushetani” kwa upande mwingine kana kwamba kuwa mnyonge ama maskini ni sifa mojawapo ya mtu kuonekana mzalendo na utajiri na mafanikio kinyume chake. Jambo la msingi hapa ni mazingira anayowekewa mwananchi ili apate hamasa ya kulipa kodi na kukidhi kigezo kimojawapo cha uzalendo.

Swali lingine ninalojiuliza ni: je, wananchi wanaona kazi ya kodi katika maisha yao ya kila siku? Hili ni swali muhimu sana. Lina umuhimu wa kujibiwa hasa na wananchi wenyewe endapo tunataka wengi wawe wazalendo (kwa kulipa kodi na si kwa kuwa maskini na wanyonge).

Jamii ya Kitanzania ninaitazama katika muktadha wa matabaka makubwa mawili: tabaka la wenye kipato cha kati na kikubwa (wenye nacho) na tabaka la wenye kipato kidogo (wasio nacho). Kama ambavyo nimetangulia kusema hapo juu; dhana ya uzalendo inajitokeza pia katika taswira ya matabaka haya makubwa mawili miongoni mwa jamii ambapo wenye kipato kikubwa wameanza kuonekana kama watu wasio wazalendo. Ninasema hivi kwa sababu hali ya unyonge na umasikini inaendelea kupewa uhalali (kisiasa) kama hali ambayo inakubalika machoni pa watawala.

Hali ya kuwa na ukwasi inaanza kuhusishwa na ufisadi, ukwepaji kodi, ubeberu (ama kutumiwa na mabeberu) na mambo kama hayo ambayo kwa kweli ni vigumu kuyatenganisha na dhana ya kukosa uzalendo (hasa katika muktadha inamotumika sasa). Kumbe basi, unyonge na umasikini vinaweza chukuliwa (na baadhi) kama uzalendo, usisi (tulio wengi) dhidi ya wao wachache wasio wazalendo. Hii inatokana na ukweli kwamba wanyonge na masikini (wazalendo) ndio wanaoonekana kupendwa na watawala kuliko hali ilivyo kwa wenye kipato (wasio wazalendo machoni mwa baadhi yetu).

Kuweza kujibu swali la uzalendo ni nini na nani ni mzalendo inaweza kuwa changamoto kwa wengi wetu hivi sasa. Maana na tafsiri ya uzalendo na mzalendo vimebadilika sana siku za hivi karibuni. Binafsi nadiriki kusema kwamba dhana ya uzalendo imepoteza maana yake kwa kiasi kikubwa na inatumika kisiasa zaidi (hasa na wanasiasa wa chama tawala) kufanikisha/kuhalalisha matakwa yao na kuwanyamazisha wale ambao wanadhani ni wapinzani wao.

Uzalendo kwa sasa unatumika kama karatasi ya litimasi ya kupima wale wanaounga mkono watawala/wanasiasa hasa wa chama tawala na wale wanaokaidi. Tafsiri ya uzalendo kwa sasa kumbe ni kushangilia na kuimba mapambio ya watawala. Kumbe si lazima itafsiriwe katika msingi wa kuipenda nchi yako na kuipigania pale inapobidi hata ikimaanisha kwa kuwanyooshea kidole watawala pale unapodhani hawaenendi katika namna ambayo italeta faida kwa watu na taifa lao.