NA SABATHO NYAMSENDA

@Sabatho7

 

Mwaka 2017, serikali ya Tanzania, kupitia Rais Dk. John Pombe Magufuli, ilitangaza “vita vya uchumi” vilivyolenga kukomesha uporaji wa rasilimali unaofanywa na kampuni za kimataifa. Mojawapo ya mbinu zilizotumika kupigana vita hivyo ni mabadiliko ya sheria za madini. Yalijumuisha utunzi wa sheria mpya zinazotambua na kusimika mamlaka ya kudumu ya Tanzania juu ya utajiri asilia na rasilimali zinazopatikana ndani nchini. 

Dola likapewa wajibu wa kusimamia mamlaka hayo kwa niaba ya wananchi. Bunge nalo lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya 2010. Hayo yote yaliyopelekea kufutwa kwa leseni ya kuhodhi eneo lenye madini iliyojulikana kama retention licence kwa lugha ya Kiingereza.

 

Kabla ya kufutwa kisheria mwaka 2017, retention licence ilikuwa ikitolewa kwa kampuni ambazo zinamiliki leseni ya utafutaji wa madini (prospecting licence) ambazo zimeshagundua madini lakini haziko katika nafasi ya kuanza uwekezaji mara moja. Hivyo, zilionekana kuhitaji muda kabla ya kufanya uwekezaji. Kwa maana hiyo, kampuni hizo zilipewa leseni ya kuhodhi eneo lenye madini iliyokuwa na uhai wa miaka mitano, ambayo iliweza kuhuishwa tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Uhuishwaji ulitegemea kama mwekezaji husika angetoa sababu za msingi za kumfanya aendelee kuhodhi eneo lenye madini bila kuliendeleza. Tofauti na hapo, Waziri wa Madini alitakiwa kumwandikia barua ya kumtaka achukue leseni kubwa ya uchimbaji madini (special mining licence). Leseni ya utafutaji wa madini (prospecting licence) ambayo nimeitaja hapo juu, hapo awali ilitolewa kwa kipindi cha miaka minne, na ingeweza kuhuishwa mara mbili kwa vipindi vya miaka mitatu na miwili. 

 

Hata hivyo, kampuni nyingi za madini zilikuwa zikitumia leseni hodhi za madini kama njia ya kuendeleza uhodhi, ulanguzi na uporaji wa madini nchini Tanzania. Ripoti ya taasisi ya ECDPM iitwayo The Complexities of Tackling Illicit Financial Flows in Practice: The Example of Tanzania ya mwaka 2019 inabainisha mbinu kadhaa zilizokuwa zikitumiwa na kampuni za kimataifa kupora rasilimali za Afrika. Zilifanya hivyo katika hatua za utafutaji wakati kampuni zikiwa na leseni za utafutaji pamoja na leseni za kuhodhi eneo la madini. 

Mbinu hizo ni pamoja na upandishaji wa gharama za matumizi wakati wa utafutaji wa madini. Pia hujumuisha hutorosha sampuli za madini ziliyochimba wakati wa utafiti hasa pale serikali inapokosa taarifa juu ya kiasi na kiwango cha madini kilichomo katika sampuli hizo. Yote haya ni sehemu ya sababu zilizopelekea utoroshaji wa fedha (illicit financial flow) unaosababisha ufukara mkubwa katika bara la Afrika. 

 

Kwa kuongezea, sehemu kubwa ya kampuni zilizomiliki leseni hodhi zilikuwa ni kampuni za kidalali zisizo na nia wala uwezo wa kuendeleza migodi. Lengo lao likiwa ni kuhodhi maeneo yenye madini. Zilifanya hivi ili kuyatumia kuingia ubia, kuyauza kwa kampuni zingine zenye pesa zaidi au kuchukulia mkopo ambao hauwekezwi katika mgodi husika. 

Miongoni mwa waathirika wa ulaghai huo ni wachimbaji wadogo. Hawa hawaruhusiwi kusogelea maeneo husika na serikali ambayo inakosa mapato. Hivyo, ni muhimu kwamba kampuni iingie moja kwa moja katika uzalishaji baada ya kipindi cha utafutaji wa madini kuisha. 

 

Sababu hizi ndizo zilizopelekea Bunge la Tanzania kutunga Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.7 ya 2017. Hii ilirekebisha ama kufuta vipengele mbalimbali vya Sheria ya Madini ya 2010. Vile vinavyohusu leseni ya utafiti na leseni ya kuhodhi eneo ni miongoni wa vipengele hivyo.

Kwa mujibu wa marekebisho hayo, leseni ya utafiti itahuishwa mara moja tu, badala ya mara mbili kama ilivyokuwa awali. Katika eneo ambalo leseni ya utafiti haiwezi kuhuishwa tena, basi eneo hilo la utafiti litarudi katika mikono ya serikali. Nayo inaweza kulitoa kwa kampuni ya ndani kwa ajili ya utafiti. Halafu kampuni za nje zenye nia ya kuendeleza utafiti zitaingia mkataba na kampuni ya ndani ambayo imepewa leseni hiyo ya utafiti.

 

Kadhalika, vifungu namba 37 na 38 vya Sheria ya Madini ya 2010 vilifutwa. Hili liliondoa kabisa uwepo wa leseni za kuhodhi eneo lenye madini. Kanuni za Madini (Mining (Mineral Rights) Regulations 2018) zilizochapishwa Januari 10, 2018 zilisisitiza kufutwa huko kwa leseni za kuhodhi maeneo na zikarudisha umiliki wa maeneo yote yaliyokuwa chini ya leseni hizo katika mikono ya serikali. 

 

Tarehe 19 Desemba 2019, Tume ya Madini ilitoa tangazo la zabuni kwa kampuni zinazohitaji leseni ya kuchimba madini katika maeneo yote ambayo yalikuwa chini ya leseni hodhi. Kampuni hizo zinazoomba zabuni zilitakiwa kuingia ubia na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Serikali (STAMICO). Ubia huu ni kwa ajili ya uchimbaji, pamoja na kuchukua jukumu la kuwaendeleza wachimbaji wadogo. 

Hata hivyo, kampuni nyingi za nje zilizokuwa zimehodhi maeneo hazikutaka kuomba leseni za uchimbaji. Badala yake zilitaka zisiathiriwe na mabadiliko ya kisheria yaliyotokea. Ama zilitaka zipewe leseni za utafiti kama mbadala wa leseni za kuhodhi maeneo. 

 

Tume ya Madini haikukubaliana na matakwa hayo. Kwa mujibu wa makala yaliyochapwa katika tovuti ya Tume ya MadiniJanuari 1, 2020, Tume ya Madini ilifanya “uchambuzi wa kina” na kujiridhisha kuwa “maeneo yote 10 yaliyokuwa na leseni hodhi yatatolewa kwa zabuni na kukaribisha kampuni za uchimbaji wa madini na watu binafsi wenye uwezo wa fedha na utaalam katika miradi ya uchimbaji wa madini na wenye nia ya kuendeleza miradi ya madini… kuomba zabuni hizo.” 

Katika makala yake iliyochapishwa mtandaoni tarehe 16 Oktoba 2018, gazeti la Mtanzania lilimnukuu mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof Idris Kikula, akifafanua zaidi kwa nini kampuni nyingi zilizomiliki leseni hodhi hazikuwa na nia ya kufanya uwekezaji: “Ukiangalia kwa undani kabisa utakuta wenye leseni walikuwa hawachimbi, mfano wa wachimbaji wa madini ya Nickel walikuwa wakiona bei imeshuka eneo hili wanaliacha na hujui zitakuja kupanda lini, hivyo eneo linakuwa chini ya mamlaka ya mtu ambaye halitumii, na haliendelezi.” Ndiyo maana Tume ya Madini ikazifuta leseni hodhi kwa mujibu wa sheria bila kutoa mbadala kwa wamiliki wa leseni. 

 

Miongoni mwa masharti yaliyowekwa katika tangazo la zabuni la Desemba 2019 ni kuwa mshindi wa zabuni alipaswa kukubaliana na sheria zote za madini na kuanza uzalishaji katika kipindi ndani ya miaka miwili ya mwanzo. Mzabuni huyo pia alitakiwa kutoa asilimia 20 hadi 30 ya hisa kwa STAMICO, ukiachilia mbali hisa asilimia 16 ambazo serikali hupewa bure kwa mujibu wa sheria mpya. Zaidi ya hayo, kampuni itakayoshinda zabuni ilitakiwa kulipa fidia kwa kampuni zilizomiliki leseni hodhi zilizofutwa kwa gharama za utafutaji wa madini ambazo kampuni hizo ziliingia. 

 

Mabadiliko haya ya sheria za madini na utekelezaji wake yameibua hujuma, tafrani na chokochoko kutoka kwa kampuni za madini, mashirika ya kimataifa na nchi za kibeberu dhidi ya serikali ya Tanzania. Baadhi ya kampuni toka ughaibuni zilitishia kupunguza mitaji yake. Zimefanya hayo yote huku zikiongoza jitihada za kuchafua taswira ya Tanzania kimataifa, hasa zikitumia mapungufu ya kisiasa ya ndani kuwa kiashiria cha uendeshaji mbaya wa kiuchumi. 

Benki ya Dunia ilitoa ripoti za kuonesha Tanzania ina mazingira mabovu ya kufanyia biashara; IMF ilianzisha uharamia wa kitakwimu kuonesha kuwa uchumi unaporomoka huku vyombo vya habari vya kimataifa kama gazeti The Economist la Marekani vikiongoza katika upotoshaji uliokithiri. Taasisi ya utafiti na ushauri wa kibiashara ya Verisk Maplecroft ya Uingereza iliiweka Tanzania katika nafasi ya tatu katika farahasi ya nchi zinazoongoza katika utaifa wa rasilimali (resource nationalism index), ikitanguliwa na Venezuela na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku ikizitahadharisha kampuni za kimataifa kuwa Tanzania ni nchi hatarishi kwa mitaji yao. 

 

Baadhi ya kampuni zilizokuwa na leseni hodhi za madini ziliamua kuipeleka Tanzania katika vyombo vya kimataifa. Gazeti la The Citizen la tarehe 10 Novemba 2018 liliripoti kuwa kati ya 2015 na 2018, kulikuwa na zaidi ya mashauri 13 yaliyofunguliwa na kampuni za kimataifa dhidi ya Tanzania zikidai fidia ya zaidi ya dola za Marekani milioni 185.58 (sawa na Sh. 426 bilioni). Mwaka huu (2020) pekee yameongezeka mashauri mengine matatu dhidi ya Tanzania katika mahakama za kimataifa, yote yakifunguliwa na kampuni za madini zilizokuwa zikimiliki leseni za kuhodhi maeneo yenye madini. 

 

Kampuni hizo ni Indiana Resources ya Australia, Winshear Gold Corp na Montero Mining and Exploration Ltd za nchini Canada. Kampuni hizo zinadai kuwa mageuzi ya kisera na kisheria yaliyofanywa na Tanzania, pamoja na hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa mageuzi hayo, umezipotezea uwekezaji kampuni hizo na kuzisababishia hasara. Winshear Gold Corp imeajiri kampuni ya kisheria ya Lalive ya nchini Uingereza kama wakili wake. Kadhalika, kampuni ya Litigation Capital Management Limited (LCM) ya Uingereza imekubali kulipia gharama za kuendeshea shauri la kampuni ya Indiana Resources ikitegemea kupata faida kutokana na fedha zitakazokamuliwa kutoka kwa serikali ya Tanzania. Hapa tayari kuna mtandao wa kampuni za kibepari za kimataifa zinazounganisha nguvu dhidi ya Tanzania na zina uhakika wa kuibuka na ushindi.

 

Chaka lililotumiwa na kampuni hizi kuishitaki Tanzania ni Mkataba wa Uwekezaji baina ya Tanzania na Canada (Canada-Tanzania BIT) uliosainiwa mwaka 2013. Kwa mujibu wa mkataba huo, iwapo Tanzania itatoa upendeleo wowote kwa wawekezaji wa ndani, basi moja kwa moja upendeleo huo utapaswa kwenda pia kwa kampuni za Kikanada. Pili, iwapo Tanzania itaamua kutoa unafuu wa kibiashara kwa wawekezaji kutoka nchi nyingine yoyote, moja kwa moja unafuu huo pia utatolewa kwa Kampuni za Kikanada. Tatu, Tanzania haiwezi kutaifisha miradi inayomilikiwa na kampuni za Kikanada. Kadhalika, Tanzania haiwezi kutunga sheria zinazolenga kuongeza udhibiti wa serikali kwa wawekezaji, kwani hiyo nayo itahesabika kama utaifishaji wa mlango wa nyuma (indirect expropriation).

Utaifishaji wa moja kwa moja nao umepigwa marufuku. Tanzania pia inazuiliwa kudhibiti uhamishaji wa mtaji na faida kwenda nchini Canada. Mbaya zaidi, hata pale litakapotokea vuguvugu la kijamii au jambo lolote litakaloathiri mali na faida za kampuni ya Kikanada, basi serikali Tanzania itapaswa kulipa fidia hata kama serikali sio chanzo cha hasara hiyo. 

 

Mkataba huo wa uwekezaji kati ya Tanzania na Canada umeweka pia masharti kuhusu usuluhishi wa migogoro. Ukitokea mgogoro kati ya kampuni ya Kikanada na serikali ya Tanzania basi mgogoro huo utaamuliwa katika vyombo vya kimataifa na kwa kutumia kanuni na sheria za ICSID (ya Benki ya Dunia) au UNCITRAL (ya Umoja wa Mataifa). 

 

Mkataba huo wa BIT ni wa miaka 10, unatakiwa kufikia ukomo mwaka 2023 lakini utaendelea kutumika hadi pale nchi mojawapo itakapoamua kuusitisha. Hata kama Tanzania itaamua kujiondoa kwenye mkataba huo mwaka 2023, uwekezaji wote uliofanywa na kampuni za Kikanada utaendelea kulindwa na mkataba huu kwa kipindi cha miaka 10 baada ya Tanzania kuwa imejiondoa. 

 

Ifahamike kuwa masharti ya aina hiyo yapo katika mikataba mingine yote ya kulinda uwekezaji (Bilateral Investment Treaties – BITs) ambayo Tanzania imeingia na nchi za Magharibi. Ni wazi kuwa masharti ya mikataba hiyo ya BIT yamelenga kupoka mamlaka ya Tanzania kujiamulia mambo yake yenyewe na kuendelea kiuchumi. Ni mikataba inayozuia hatua zozote za kulinda soko lake la ndani ili kujenga uchumi wa viwanda au kudumisha ushirikiano baina ya nchi za Kusini (South-South cooperation). Mikataba hiyo ni miongoni mwa kanuni za kudumisha umasikini zilizosukwa kwa ustadi mkubwa na nchi zenye maendeleo ya viwanda ili ziendelee kunyonya na kukandamiza nchi maskini. 

 

Tanzania ilianza vyema pale ilipoanzisha vita vya uchumi mwaka 2017 na kutunga sheria tatu za kulinda rasilimali na utajiri asilia ili zitumike kuwanufaisha wananchi wake. Hivyo, Tanzania isikubali kuyumbishwa ili kuachana na kazi ya kulinda rasilimali zake kwa manufaa ya watu wake. Ili kuzuia uharamia unaofanywa na kampuni za kimataifa dhidi yake, basi serikali ikate mzizi wa kisheria unaozipatia nguvu kampuni za kimataifa pamoja na nchi zinapotokea. 

Mahali pa kuanzia ni kusitisha mikataba yote ya uwekezaji (BITs) ambayo Tanzania imeingia na nchi nyingine pamoja na kujiondoa kwenye mikataba ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji kama ICSID Convention na New York Convention. Sehemu kubwa ya mashauri yaliyofikishwa katika ICSID yamezipatia ushindi kampuni za nchi za Magharibi dhidi ya nchi masikini, na hivyo kuchangia kuzifilisi zaidi nchi masikini. Gharama za kuendesha mashauri katika mahakama hizo zipo juu sana, ambapo nchi masikini hulazimika kulipa kiasi cha dola 1,000 kwa saa kwa mwanasheria wa kimataifa anaeiwakilisha. 

 

Sheria ya Usuluhishi (Arbitration Act) ya 2020 ifutwe. Badala yake itungwe sheria nyingine ya usuluhishi inayotambua mamlaka ya kudumu ya Tanzania juu ya rasilimali zake na inayozuia matumizi mahakama za nje na sheria za kimataifa kushughulikia migogoro inayoibuka kati ya wawekezaji na serikali. Mahakama za ndani pamoja na sheria na kanuni za Tanzania ndivyo vitumike katika kuamua migogoro kati ya wawekezaji na serikali. 

 

Je, hatua hizi zitazikimbiza kampuni za kibeberu na kuzifanya kuondoa mitaji yake nchini? Itakuwa ni habari njema iwapo kampuni hizi zitakimbia kwa sababu ndio utakuwa mwanzo wa nchi yetu kufikiria namna ya kujitegemea kiuchumi. Lakini ukweli ni kwamba hazitakimbia. 

Miaka 10 iliyopita, Afrika Kusini ilijiondoa kwenye mikataba 20 ya BIT lakini uwekezaji toka ughaibuni ulizidi kuongezeka nchini humo. Kadhalika, Ecuador chini ya Raphael Correa na Bolivia chini ya Evo Morales zilijiondoa kwenye mikataba hiyo lakini mitaji toka ughaibuni ilizidi kupaa. Ukweli ni kwamba kampuni za kimataifa zinahitaji sana utajiri asilia na rasilimali zinazopatikana nchini mwetu kuliko ambavyo nchi yetu inavyohitaji mitaji ya kampuni hizo.

 

Sabatho Nyamsenda ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com