Wazanzibari sio Waskochi
Matokeo ya kura za maoni
huko Uskochi yameacha gumzo barani Afrika. Kuanzia Abuja hadi Arusha Waafrika
tunajiuliza kuna nini cha kujifunza. Hapo Mji Mkongwe, Zanzibar hiyo ndiyo
habari ya mjini.
Rafiki yangu mwenye
uzalendo wa Kizanzibari amenishtusha kwa kunitumia ujumbe usemao “naona umefurahi…haya
furahia” baada ya kumtumia taarifa kuhusu matokeo
hayo na kuuliza kiutani: “Vipi Zanzibar/Unguja/Pemba/Tumbatu?” Kutokana na
sababu za kihistoria – historia binafsi na ya jumla – naipenda sana Uskochi. Nimefurahi
wamepitia mchakato huu muhimu ambao inasemekana, pamoja na kushindwa katika
kura, utawaletea mabadiliko mengi yatakayoongeza
uhuru wao ndani ya Muungano.
Fundisho nililolipata
ni kuwa japo Wazanzibari sio Waskochi hata wao wana haki ya kupiga kura kama
wenzao na watakapopata fursa hiyo tusishangae maamuzi yao kisa baadhi yao/yetu
tumekuwa tukiwasemea kuwa wanataka hiki au kile. Pia yamenipa moyo kuwa sio
jambo la kushangaza kupinga muundo (dhaifu) wa Serikali Tatu kati ya eneo moja
kubwa na eneo moja dogo ilhali nasimamia hoja yangu kuwa ‘Zanzibar ni Zaidi ya Nchi’.
Haishangazi kwani Muungano wetu bado unuweza kuongeza uhuru zaidi kwa Zanzibar.
Wapo wanaoshangazwa
na Waskochi kupiga kura ya kukataa kujitenga na Uingereza. Hapa tunaongelea
sehemu ambayo imekuwa na historia ndefu ya uzalendo wa Kiskochi toka enzi za William
Wallace, yule shujaa wao maarufu ambaye Mel
Gibson alimuigiza katika filamu yake ya Braveheart,
yaani, ‘Moyojasiri’.
Filamu hiyo inaanza
na maneno mazito ya Mskochi dhidi ya Muingereza ambayo kwa tafsiri ya haraka
haraka yanasomeka hivi kwa Kiswahili: “Nitakueleza habari za William Wallace.
Wanahistoria wa Kiingereza watasema nadanganya. Lakini historia huandikwa na
wale wanaowanyonga mashujaa”. Naam, ndivyo ilivyokuwa, Wallace alinyongwa baada
ya kuongoza mapambano ya Uskochi dhidi ya Uingereza.
Kwa zaidi ya miaka
700 mpambanaji huyo amekuwa kielelezo thabiti cha uzalendo wa Kiskochi. Lakini
uzalendo huo umeshindwa kupata kura za kutosha za kuuvunja Muungano wao na
Uingereza. Kwa nini?
Profesa mmoja wa
Kinaijeria anasisitiza kuwa japo
Uingereza haikuwatisha wapiga kura kwa mtutu wa bunduki, ilitumia vitisho vya
kiuchumi. Anadai mabenki na taasisi za kifedha zilitishia kujitoa Uskochi.
Pia anasema Waskochi
walitahadharishwa kuwa nchi yao mpya itabidi ilipe sehemu ya deni la taifa na
itakumbana na visiki kwenye suala la sarafu yao. Hili, anahitimisha,
liliwatisha sana wale wapiga kura wanaokuwa hawana hakika hadi dakika ya mwisho
na ambao kwa kawaida ndio wanaobadili matokeo.
Huyo mwanazuoni
ni miongoni
mwa wale ambao wanahoji kama uchaguzi huo wa kutojitenga ulikuwa ni utashi
tu wa Waskochi walio wengi zaidi. Lakini katika maamuzi ya masuala ya kutengana
hofu huwa ina sehemu yake. Kiongozi mkuu wa Uskochi wakati wa upigaji kura huo,
Alex
Salmond, ameamua kujiuzulu ila amekubali matokeo hayo japo amesisitiza kuwa
“kampeni inaendelea na njozi yao haitakufa kamwe”.
Ugumu wa maamuzi hayo
ya Waskochi unathibitishwa na idadi ya kura. Asilimia 55 dhidi ya 45 ni ishara
kuwa wamegawanyika takribani katikati katika suala hili. Hivyo, ni vigumu na
labda haiwezekani kufanya uamuzi ambao utawapendeza Waskochi wote sasa. Hata
kura za Sudani ya Kusini hazikufikia asilimia 100!
Zanzibar je?
Itakuwaje Wazanzibari nao wakipata fursa ya kupiga kura? Wataamua kujitenga na
Tanzania?
Jibu wanalo
Wazanzibari wenyewe. Ili tulipate hilo jawabu lazima wapate kwanza hiyo fursa.
Kile ambacho kimekuwa kinaendelea ni ‘mwamba ngoma ngozi huvutia kwake’.
Anayewamba ngoma ya kujitenga atakuambia Wazanzibari wengi hawataki Muungano.
Na anayewamba ngoma ya kutojitenga atakuambia Wazanzibari wengi wanataka Muungano.
Hata tafiti zikikubaliana tafsiri zinatofautiana.
Ile taasisi iliyokuwa
inaheshimika sana katika tafiti za kitakwimu, REDET, iliwahi kufanya tafiti mwaka 2003
& 2004 na kugundua kuwa ni asilimia 1.6 tu ndiyo walikuwa hawaupendi Muungano
na hakukuwa na tofauti kubwa kati ya Wazanzibari na Watanzania Bara kuhusu
hilo. Tofauti za msingi zilikuwa kwenye muundo wa Muungano. Hizo ndizo
zinazoendelea kuleta mgongano katika mchakato wa katiba mpya.
Ugunduzi mwingine
muhimu wa tafiti hizo, kwa mujibu wa uhakiki wa baadhi ya Wanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni kuwa asilimia ya
walioweza kutaja angalau faida moja ya Muungano kwa ujumla/wastani haikuzidi 50
nchini Tanzania. Kwa upande wa Zanzibar, wengi wao – asilimia 52 – walitoka
mkoa wa Mjini Magharibi na Tanzania Bara walitoka mikoa ya Pwani – Tanga
(78), Pwani (64), Mtwara (64) na Lindi (62) – hivyo, kupelekea wahakiki
hao kuhitimisha kuwa hii “inaashiria
kwamba ni katika ile mikoa yenye maingiliano makubwa zaidi ya kijamii na
kiuchumi baina ya watu wa pande mbili za Muungano ndio wanaofahamu zaidi faida
za Muungano.” Hivi hawa wakipiga kura
watashinda kweli?
Demokrasia ni kama upanga ukatao kuwili. Inaweza
kuleta kile kiitwacho ‘udikteta wa walio wengi’ ambapo hata
asilimia 55 inatosha kuamua nchi iendelee na kile ambacho asilimia 45 ya wenzao
haikitaki. Hebu tazama picha za baadhi ya Waskochi kutoka kwenye hiyo asilimia
45 wanavyotokwa
na machozi kwa kushindwa kujitenga. Je, kwao matokeo ya ‘referenda’ ndio ‘maridhiano’. Piga picha ni jinsi gani kura kama hiyo ikipigwa Zanzibar na
ikatokea walio wengi kutoka Mjini Magharibi wakasema hawataki kujitenga ila
wenzao wa mikoa mingine walio wengi zaidi wakasema tujitenge – ndio itakuwa ‘mwafaka’?
Cha kuzingatia ni
kuwa na mfumo unaoridhiwa na wananchi wa kufanya maamuzi magumu ambayo hata
kama matokeo yake hayatawapendeza wote angalau mchakato wa kufikia uamuzi huo
utawapendeza wengi kama sio wote. Ni dhahiri kuwa tumegawanyika kwenye suala la
muundo wa Muungano. Hakuna takwimu za taasisi au tume yoyote zinazopinga ukweli
huo. Na mgawanyiko huu unachochea mgawanyiko kuhusu uwepo wa Muungano. Kwa hali
ilivyo sasa hakuna upande wowote wa Muungano ambao haujagawanyika.
Ombeni
Sefue amekaririwa akisema hivi kuhusu suala hilo: “Hutapata maridhiano hayo
ndani ya Bunge Maalumu na hutapata maridhiano ukienda kwa wananchi.” Ni kweli.
Hatuwezi kupata ‘maridhiano hayo’ kokote sasa. Tunachoweza kupata ni maridhiano
ya namna ya kuridhiana. Kilichobaki ni kuamua namna ya kukipigia kura kile
ambacho kitawaacha wengi tu hawajaridhika japo wengine wengi tu wameridhika.
Tuamue sasa. Kama
kweli tunataka kuamua kuvunja na kuunda nchi upya tuitishe kura ya maoni huko
Zanzibar. Wazanzibari wapate fursa ya kuamua kujitenga au kubaki katika Muungano
wa Tanzania.
Baada ya hapo, kama
wameamua kubaki, tupige kura kuamua muundo wa Muungano. Tukimaliza ndiyo
tutengeneze katiba mpya. Hakika (z)itakuwa katiba mpya maana hata nchi
(z)itakuwa (z)imezaliwa upya.