Chuki hizi msidhani

Hazina udini ndani,

Maana behewa hili

Lina watu kila hali

Wamo na maaskofu,

Na mashehe watukufu;

Na wasomi wa sharia,

Na wachumi wetu pia,

Kila mtu ana lwake,

Anazo sababu zake.

Wamo na watu wajinga,

Wanodhani wakitenga

Tanganyika iwe pake,

Ina Serikali yake,

Nchi haitavunjika,

Ila itaimarika.

Wangasema hawataki

Kutuletea hilaki,

Bali kwa ujinga wao

Tukaangamizwa nao,

Wao na wanoania

Wote ni wamoja pia,

Na njia ya jahanama

Imejaa nia njema.

Wamo na waso wajinga

Wanokusudia janga,

Ila wao wanadhani

Sisi ndio punguani

Kwa ulozi wa maneno

Ati “ndani ya Mwungano”,

Watulaze usingizi,

Waleta maangamizi.

Mumo humo pia wamo

Wasio na msimamo,

Wanofuata mkumbo

Kwa hili na kila jambo.

Upepo uvumiako

Ndiko nao waendako,

Kwao hiki ni kimbunga,

Ni hatari kukipinga!

Wamo walopungukiwa

Au kuchanganyikiwa,

Waliomo behewani

Bila kujua kwa nini.

Wamo behewani humo

Wenye dhiki na urumo,

Wanodhani watashiba

Tukitana na Zanziba

Wamo na wengine tena,

Watu aina aina

Kiwauliza sababu,

Hawana la kukujibu.

Wamo na watu wabaya,

Wawi, wana wa hizaya,

Ni watu wanochukia

Umoja wa Tanzania,

Sasa wamepata mwanya

Ili kutuparaganya.

WOTE, na wasonia,

Watavunja Tanzania,

WOTE, na watoumia,

Wamo wanashangilia.

Wanabomoa misingi,

Na sisi hatuwapingi,

Tubaki ni kunyamaa

Na kushikilia paa,

Jumba kitakapoomoka,

Nani atasalimika?

Wala msidhani ati

“Kwenda kwenda na wakati’

Kila mara ni halali,

Hata kwa mambo batili.

Mtayumba na wakati,

Bila dira bila dhati?

Mkondo uvutiako,

Nanyi mkokotwe kuko?

Sera mpya kila mara,

Kufuata mazingira,

Kama vitenge na kanga,

Au rangi za kinyonga?

Mawi hayawi matamu

Kwa kupendwa na kaumu,

Wala sumu kuwa uki

Kwa kupendwa na malaki

Hata yaletayo janga,

Hatuwezi kuyapinga?

Yangatukusa balaa

Ni mwiko kuyakataa?

Hata yanayobwaga zani?

Yangatwingiza vitani?

Yakishapendwa na watu,

Kupinga hatuthubutu?

Wengi wakichachamaa,

Watakalo watatwaa,

Ila si kweli kusema

Daima hutaka mema

Wengi wakishaamua

Mama yako kumuua,

Kwa kuwa wao ni wengi,

Utashiriki, hupingi?

Yako mambo ya msingi,

Yasiyotegemea wingi,

Yanotaka msimamo,

Wengi wangawa hawamo.

Ungebaki peke yako,

Kupinga ni wajibiko,

Ungafa uwe mhanga,

Huna budi kuyapinga.

Ni moja ni kama lino

La kuvunja Muungano,

La kujenga uhasama

Katika jamii nzima.

La kuiga Wasomali

Kama watu majuhali,

La kufanya Tanzania

Iwe Yugoslavia.

La kufuata Warusi

Hata katika maasi,

La kuvunja vunja Dola,

Turudie makabila.

LINGEPENDWA NA KAUMU

BADO NI JAMBO HARAMU.

Nimewambia wenzangu:

Ningebaki peke yangu,

Nitapinga’ Nitapinga

Tanganyika kujitenga!

Julius K. Nyerere (1993: 16-32) Tanzania! Tanzania! (TPH)