“Katika shilingi bilioni 306 zilizokuwa na zilizopaswa
kuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kuna fedha za Umma. Serikali inasema
hazikuwa 306 bilioni bali 202 bilioni! Hii sio hoja ya msingi. Hoja ya msingi
ni kwamba hata zingekuwa bilioni moja, bado ndani yake kuna fedha za umma na
ilipaswa utekelezaji wa hukumu ya kupunguza kiwango cha tozo ya uwekezaji
kufanyika ili kujua kiasi cha fedha za umma. Tapeli Harbinder Singh Seth
alilipwa hizo zilizokuwemo katika akaunti na akaendelea kulipwa bakaa na TANESCO
kiasi kwamba shirika hili linalofilisika linamlipa kila siku bwana huyu
shilingi milioni 400. Kila siku inayokwenda kwa mungu tunamlipa mtu ambaye
hajawekeza hata senti tano nchini mwetu. Alikuja na briefcase tu. Kule Kigoma
kuna neno jipya siku hizi, linaitwa umazwazwa. Ni kama ujuha hivi. Huu ni
umazwazwa ambao wananchi hawapaswi kuukubali. Watu watatu tu ambao ni raia wa
kigeni walichora wizi huu kwa miaka mitatu. Mtu mmoja anaitwa Bwana Baharuddin
kutoka Malaysia, Bwana Issa Ruwaih kutoka Oman na Bwana Singh kutoka Kenya na
anaishi Afrika Kusini. Walidanganya nyaraka za kuuziana makampuni, bwana
Baharuddin akauza hisa za IPTL kutoka Mechmar kwenda kwa Bwana Issa wa kampuni
ya PiperLink na Bwana Issa naye akauza hisa hizo zikiwa zimezuiwa na Mahakama
kwa Bwana Seth wa kampuni PAP. Mabwana hawa wanajua Watanzania ni
mazwazwa na hawafanyi uchunguzi wa kina, yaani ‘due diligence’ kwani hata
kwenye EPA fedha ziliibiwa kwa kutofanya due diligence na kwa kutumia kitu
kinaitwa ‘deed of assignment’. Mabwana hawa wanajua kuwa Watanzania wenye ofisi
za umma wana njaa na watawahonga kidogo tu na kupitisha kila kitu. Ndivyo
ilivyofanyika. Kama viongozi wetu wangefanya ‘due diligence’ kwenye manunuzi ya
makampuni haya kama Sheria ya Kodi ya Mapato inavyowataka, tusingekuwa na
skandali ya Tegeta Escrow. Mfumo uliganzishwa kwa rushwa. Ukitazama miamala ya
malipo kutoka akaunti ya Bwana Seth katika akaunti ya StanBic utaona fedha
zimekwenda benki za UAE na baadaye Oman na Malaysia. Fedha hizo zilikwenda
kuwalipa mabwana Baharuddin na Issa. Serikali lazima ichukue hatua mara moja
kuhakikisha fedha zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zinarudi, uamuzi
wa mahakama ya kimataifa unatekelezwa na fedha za umma zinarejeshwa TANESCO na
zile za binafsi zinalipwa kwa wamiliki halali. Tanzania haiwezi kuwa nchi ya
kubariki utapeli wa kimataifa na kuchafua sura ya nchi yetu mbele ya jamii ya
kimataifa. Baraza la Taifa yaani Bunge, kupitia wawakilishi wa wananchi, tayari
wameamua na kupitisha maazimio. Kilichobakia ni maazimio hayo kutekelezwa na
Serikali. Hakuna mjadala katika maazimio ya Bunge, maana katika maazimio hayo
Serikali nayo imo; ilishiriki kikamilifu katika kuyandaa na hatimaye kupitishwa
na Bunge. Hakuna namna ya kukwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kwa ukamilifu wake;
nasema hakuna, ni utekelezaji tu” – http://zittokabwe.wordpress.com/2014/12/31/speech-by-zitto-kabwe-mtwara-31-12-14/