“Katika nchi kama yetu, ambamo Waafrika ni masikini na wageni ni matajari, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi yake katika miaka themanini au mia moja ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni na wenyeji watakuwa watwana. Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri na wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana” JKN 1958 (Uhuru na Umoja)
Haya ni maneno ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoyatoa mnamo mwaka wa 1958 wakati wa vuguvugu la kupigania uhuru katika makala yake iitwayo Mali ya Taifa. Kimsingi muktadha hasa uliopelekea kuandikwa kwa makala hiyo ilikuwa ni jaribio la Waingereza kuingiza nchini mfumo wa umiliki ardhi usiokuwa na ukomo (freehold). Ikumbukwe kwamba suala hili lilipendekezwa na Tume ya Malkia ya 1953-1955 iliyofanya zoezi hili katika nchi zote tatu zilizokuwa chini ya utawala wa Mwingereza (Kenya,Tanganyika na Uganda). Kwa mtazamo wa tume hiyo ,mfumo huo ulionekana ni bora zaidi ikilinganishwa na mfumo wa umilki ardhi wa pamoja chini ya misingi ya mila na desturi za makabila mbalimbali. Kimsingi pendekezo hilo lililenga zaidi kuingiza mfumo wa soko huria katika kuratibu suala zima la mfumo wa milki ya ardhi.
Kwa mtazamo wa Mwalimu, kuruhusu mfumo wa aina hiyo sio tu kungeleta matabaka ya wenye ardhi na watwana lakini pia kwa mazingira ya nchi yetu ingekuwa chanzo cha machafuko ya kijamii. Pendekezo hilo lilikubalika kwa majirani zetu Kenya na ikawa ndiyo chanzo kikubwa kwa walalahai na walalaheri wa huko kujilimbikizia maeneo makubwa ya ardhi mpaka kufikia hatua baadhi yao kumiliki eneo lenye ukubwa kama nchi ya Rwanda! Hapa nchini baada ya kupata upinzani kutoka kwa viongozi wa kisiasa wa wakati huo wakiongozwa na Mwalimu Nyerere wazo lilizikwa rasmi miaka ya mwanzoni ya uhuru. Mwalimu kimsingi aliichukulia ardhi kama zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wote na si kundi la wachache.
Baada ya kupata uhuru, kimsingi sheria ya Kikoloni ilifanyiwa marekebisho madogo ila msingi wa sheria ulibakia pale pale. Kutokana na mapungufu katika sheria hiyo wazalishaji wadogo, wakulima kwa wafugaji na makundi mengineyo, yaliathirika sana hasa lilipokuja suala la uhakika wa miliki. Pamoja na kwamba serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu ilikuwa na nia na lengo zuri la kuwakwamua Watanzania kutoka katika lindi la umaskini katika utekelezaji kupitia Sheria ya Ardhi ya Kikoloni ya Mwaka 1923walio wengi walijikuta wakipoteza haki zao.
Uanzishwaji wa mashamba ya lililokuwa Shirika la Kilimo na Chakula (NAFCO), Ranchi za Taifa (NARCO) na upanukaji wa maeneo ya hifadhi ni mifano michache tu inayoonyesha jinsi ambayo haki za watu juu ya ardhi zilivyopokwa. Kimsingi ardhi ilipokwa kutoka mikononi mwa wananchi ama kwa maana nyingine umma na kuwekwa mikononi mwa dola sio katika wakati wa Mwalimu tu bali toka enzi za ukoloni! Kwa hiyo utaifishaji na mengineyo yaliyofuatia yalikuwa ni sehemu tu ya kile tulichokirithi toka kwa wakoloni.
Lengo la makala hii siyo kuangalia yaliyotokea hasa wakati huo wa Mwalimu, lakini hasa ni kujikita katika msingi wa mtazamo wake katika kipindi cha kupigania uhuru. Je aliyoyasema Mwalimu mnamo mwaka 1958 katika kipindi chetu yamepoteza maana ama yanasadifu yanayotokea sasa? Baada ya kukaa na sheria hiyo ya kikoloni kwa takribani miongo saba (1923-1999) serikali kwa kufuata mapendekezo ya Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Migogoro ya Ardhi ya Mwaka 1991 iliamua kutunga sheria mpya za Ardhi mnamo mwaka 1999.
Sheria ya Ardhi Namba 4 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 za mwaka 1999, pamoja na mazuri yaliyokuwamo katika sheria hizi bado msingi wake mkuu unabaki kuwa sheria ya kikoloni kwa maana ya kulimbikiza nguvu nyingi mikononi mwa dola. Ardhi inatajwa kuwa mali ya Umma lakini kivitendo ni mali ya serikali zaidi kuliko kuwa ya umma! Sheria hizi zilifanyiwa marekebisho mnamo mwaka wa 2004 ambayo kinyume kabisa na Mwalimu marekebisho hayo yanatambua ardhi tupu ambayo haijaendelezwa kuwa ina thamani na pia yanaruhusu ardhi kuuzwa kama bidhaa nyingineyo yoyote katika soko!
Katika makala yake ya 1958, Mwalimu ameendelea kutanabahisha wazi kuwa “wakati watu wengi watakapokubali njia ambayo itawawezesha wachache kumiliki ardhi ambayo kwa kweli ni zawadi ya Mungu kwa watu wote, watakuwa wanaukubali utumwa kwa hiari yao wenyewe.” Ni nini taathira ya mabadiliko ya sheria ya ardhi ya mwaka 2004? Je, tunaweza kusema utabiri wa Mwalimu katika hili umetimia? Je kumeibuka kundi la Watanzania matajiri wajanja wachache ambao kazi yao ni kuwanunua waungwana tuliosalia tusio na hili wala lile tukisogezwa pembezoni zaidi?
Wakati wa uongozi wa awamu ya tatu Mkuu wa kaya wa wakati huo alishangaa kuona wanakaya wakiwa hawafaidi matunda ya mageuzi ya soko huria hivyo aliamua kwenda Peru na kutafuta mwarobaini wa tatizo hilo la Watanzania kutofaidi matunda, matokeo yake ndiyo marudio ya yale ambayo Tume ya Malkia ilipendekeza lakini kwa mtazamo wa kuwa kila kipande amilikishwe mtu binafsi kwa kuwa masuala ya umiliki wa pamoja ni mambo ya Ujamaa uliokwishapitwa na wakati! Pamoja na hayo hii ndiyo njia rahisi ya kupata ardhi kwa Watanzania wajanja wachache ama wageni matajiri kwani badala ya kuongea na ukoo sasa wataongea na mtu binafsi!
Ukitembelea vijiji vya pembezoni mwa miji yetu utagundua kuwa wamilki wa awali sasa wamebakia kuwa watwana katika ardhi zao kwa kuwa walishauza ili kukidhi haja na shida zao mbalimbali. Kwa kuwa Watanzania walio wengi tegemeo lao kubwa ni ardhi machafuko ya kijamii ambayo Mwalimu aliyahofia enzi zake kuwa kama tusipokuwa makini yanaweza kutokea leo hii yamekuwa ni nyimbo za kawaida katika vyombo vya habari! Mashamba makubwa yaliyochukuliwa na serikali kwa lengo zuri la kuifaidisha jamii nzima leo hii yamebinafsishwa na mara nyingine mashamba yamebinafishwa hata pale ambapo wanavijiji waishio jirani nayo wanayahitaji wa ardhi.
Migogoro ya Arumeru, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro ni mifano tu ya jinsi ambavyo jamii imechoshwa na mgawanyo wa rasilimali unaofaidisha kundi dogo la wateule huku wana wa nchi wakitaabika kutafuta wapi pa kukamata! Wimbi la ujio wa wageni wanaotamani ardhi yetu nalo bila shaka katika miaka michache ijayo itaongezea petroli katika moto ambao kama hatutakuwa makini katika kipindi hiki utalipuka.
Tuliokuwepo sasa tumesahau kuwa kama alivyotuasa Mwalimu ardhi ni mali yetu lakini hasa ni mali ya vizazi vijavyo na hivyo basi tumekabidhiwa kama dhamani kwa ajili ya kutuwezesha sisi lakini hasa kukiandalia mazingira mazuri kizazi kitakachofuata. Bila shaka huu ulikuwa ni msingi wa kuweka msisitizo katika jamii za Kitanzania kuwa msitari wa mbele hasa kuanzia ngazi ya familia na Kijiji katika kujumuika kwa pamoja kujiletea maendeleo.
Leo hii tunamikakati mbalimbali na hivi karibuni ulizinduliwa Mkakati wa Kilimo Kwanza, je Kilimo Kwanza ni kwa ajili ya kundi gani? Kilimo Kwanza kinamlenga nani? Je, kimetambua nafasi ya hili kundi la wazalishaji wadogo hasa akina Mama ambao kimsingi ndio wanaolilisha taifa?
Hapa ikumbukwe kuwa Mwalimu alishapata kusema juu ya jinsi akina baba wa Kitanzania wanavyotumia muda wao! Nusu ya maisha yao wapo likizo huku kazi za shamba zikifanywa na akina Mama. Je, nafasi ya akina Mama imetambuliwa na Kilimo Kwanza? Ama ndiyo mikakati ya kuwezesha Watanzania matajiri wajanja wachache kunyakua maeneo makubwa ya ardhi kwa kisingizio cha Kilimo Kwanza?
Katika Azimio la Kilimo Kwanza kuna pendekezo la kufanyia marekebisho Sheria ya Ardhi ya Vijiji ili kuwezesha upatikanaji wa ardhi uwe rahisi! Urahisi huu unalenga katika nini? Vijiji kama vijiji imeshindikana kuviwezesha ili viwe msingi wa Kilimo Kwanza kwa kutumia ardhi zao, au Kilimo Kwanza kinanoga mpaka Lifanyabiashara Bepari moja likitoka Dar es Salaam na kwenda kunyakua ardhi ya wana wa Rufiji?
Nimalizie makala yangu ya kumbukizi ya Baba wa Taifa kwa kusema kuwa masahibu wanayopitia majirani zetu sio majanga ya asili ila ni kazi ya akili za binadamu. Tukiachia hulka za kibinafsi zitawale maamuzi na mienendo yetu ya kimaisha hii amani tujivuniayo sasa itayeyuka kama inavyoyeyuka sasa barafu katika Mlima wa Kilimanjaro. Tukumbuke kuwa panapofuka moshi moto hufuatia.
Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana na vizazi vya watwana havitakubali hili hivyo tutakuwa tumekiandalia kizazi kitakachofuata zawadi ya vita na machafuko kwa tamaa ya kujilimbikizia kila kipande cha ardhi.
© Bernard Baha