Muundo wa Muungano: Serikali Tatu,
Moja, Mbili? Zote!


Zitto Kabwe


Mwalimu Azaveli Lwaitama ni mwalimu na mlezi wangu nje ya darasa.
Alipokuwa Katibu wa Umoja wa Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mimi
nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Idara ya Uchumi. Nilikuwa nashinda
kwenye Ofisi ya UDASA tukijadiliana kuhusu Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism),
Ujamaa na harakati za kulinda haki za watu. Ilikuwa ni nadra kwa mwanafunzi wa uchumi kuwa karibu na mwalimu wa lugha na mnadharia mkubwa. Wanafunzi wa uchumi
tulikuwa tunajidai na kujivuna. Tulikuwa tunajiona bora sana maana darasa letu
halikuwa linazidi watu 40 na kwa kweli wote hawamalizi. Darasa langu tulimaliza
wanafunzi 25 tu kati ya 40 tulioanza. Mwalimu Lwaitama ni mpenzi mkubwa wa Muungano kama nilivyo mimi. Tumeapa kuulinda kwa namna yeyote ile. Yeye alikuwa
mhafidhina (conservative) sana akitaka Muungano wa muundo huu aliouacha Mwalimu Nyerere. Mimi
nataka kuulinda kwa kuufanyia marekebisho makubwa sana ya kimuundo. Hatukuwa
tunakubaliana.

Wiki iliyopita Mwalimu Lwaitama kaandika kuhusu muundo wa Muungano
katika makala zake za kila wiki katika gazeti la kimombo la The Citizen.
Amebadili msimamo. Ameona sasa muundo wa Muungano ulivyo sio endelevu. Ametoa
mapendekezo niliyoyatoa siku za nyuma katika mazungumzo yetu ingawa yeye bado
anayasema kwa shingo upande. Lwaitama sasa anataka Serikali mbili
zilizonyumbuliwa. Anapendekeza Waziri Mkuu wa Muungano mwenye nguvu za za
kitendaji. Nampongeza kwa kuboresha mawazo yake. 

Hata hivyo bado Mwalimu wangu na Watanzania wengi wamejikita katika
mjadala wa Serikali ngapi. Idadi ya Serikali inaonekana kama ndio dawa ya kero
za Muungano. Ni kweli Wazanzibari wanataka uhuru zaidi na wengine hawataki
kabisa Muungano. Unawalalia. Unawanyima uhuru wa kuamua baadhi ya mambo yao na
japo halisemwi unawanyima wanasiasa wa Zanzibar mamlaka ya masuala mengine
ambayo yangewafanya wajilimbikizie madaraka.

Huku bara napo kuna watu, tena wanaongezeka kwa kasi kweli kweli,
wakitaka Tanganyika yao. Tena wengi vijana. Demografia zetu zinaonyesha kwamba
Watanganyika waliozaliwa Tanganyika ni takribani asilimia 12 tu ya Watanzania.
Asilimia 70 ya Watanzania wamezaliwa wakati Muungano umeshasherehekea miaka 15
ya kuzaliwa kwake. Lakini wanataka Tanganyika yao. Wamechoshwa na kelele za
Wazanzibari. Hawawataki Wazanzibari kujaa kwenye Bunge la Muungano wakati wapo
kiduchu sana. Wanasiasa nao, japo hawasemi waziwazi wanataka wawe na mamlaka
zaidi bila kulazimika kushauriana na wanasiasa wa Zanzibar. Linapokuja suala la
wagombea Urais ndio kabisa wanakereka kutafuta mgombea mwenza kutoka Zanzibar.
Wachambuzi wa historia za kisiasa siku wakiamua kufanya tafiti watachoka na
roho zao watakapoona aina za wagombea wenza ambao wagombea Urais huteua, hasa
kutoka sisi vyama vya upinzani.

Kimsingi idadi ya wapinga Muungano inazidi kuongezeka siku hata siku.
Ukiwauliza kwa nini hawataki Muungano wanasema aah, basi tu. Kama ni Mzanzibari
atasema Tanganyika wanatutawala. Kama ni Mtanganyika atasema Wazanzibari
wamezidi kelele, tunataka Tanganyika yetu. Sisi ‘Unionists’ (Wanamuungano) nao hatuna majibu ya
kuridhisha sana na ya kukonga nyoyo. Isipokuwa tu, Muungano huu ni wa aina yake
Afrika na Duniani. Ni alama pekee ya kuonyesha Mwafrika kupinga mipaka ya
kikoloni. Sasa hili haliwaingii kichwani ‘secessionists’ (Wanautengano) na hatuna la kuwasaidia.
Lakini ni lazima tuurekebishe Muungano huu. Ulivyo sasa utavunjika tu. Kuulinda Muungano ni kuufanyia marekebisho makubwa. Mwalimu Lwaitama kaliona hilo.
Pendekezo lake liboreshwe sasa. Sio rahisi sana.

Sasa tufanyeje? Serikali moja itaimeza Zanzibar. Serikali Tatu ni
gharama kuendesha na Serikali mbili zimeimeza Tanganyika na watu wanataka
Tanganyika yao na zinainyima uhuru Zanzibar na watu wanataka wawe huru zaidi.
Mfumo wa Serikali ngapi na kadhalika ni moja ya mikakati ya wanasiasa katika
kusaka vyeo. Sisemi sio halali kujadili lakini kiukweli mfumo gani wa Muungano
hautaongeza fungu la dagaa kwa mwananchi wa Kagongo au sinia la ubwabwa kwa
mwananchi wa Mkanyageni. Waingereza wana msemo ‘unataka kula keki yako na
kubaki nayo’, basi tuwe na Serikali zote.

Nimeanza na Mwalimu Azaveli Lwaitama. Naboresha hoja yake kwa kurudia
niliyowahi kuyasema huko nyuma kuhusu muundo wa Muungano. Tuwe na Dola Moja tu.
Ndio, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala sio Shirikisho la Tanzania
(kwanza litatuondoa kwenye kiti chetu kule Umoja wa Mataifa maana kwa jina letu
sisi tunakaa katikati ya Uingereza na Marekani. Katikakati ya mabwana wakubwa,
labda ndio maana wanatupa misaada sana, unajuaje?). Tuwe na Rais mmoja tu
mwenye mamlaka kamili ya Asasi za Dola – Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Uhamiaji,
Sera za Fedha na jukumu la jumla la kusimamia ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Achaguliwe na Watanzania wote wa pande zote mbili za Muungano kwa
kupata zaidi ya nusu ya kura za pande zote za Muungano. Tuachane na mambo ya
Mgombea Mwenza. Tumejaribu tumeona hana maana zaidi ya kutembea na mikasi tu.

Zanzibar  iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya Muungano. Tanganyika iwe na Waziri Mkuu Mtendaji kwa masuala yote ambayo sio ya Muungano. Hawa watateuliwa na Rais wa
Muungano kutoka chama chenye Wawakilishi wengi katika Baraza la Wawakilishi
Tanganyika na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Wote watakuwa ni Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano kwa utaratibu kwamba iwapo Rais anatoka Zanzibar, basi
Waziri Mkuu wa Tanganyika atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na wa Zanzibar
atakuwa Makamu wa Pili wa Rais. Kule kule kwenye misingi haswa ya Muungano.
Hawa wataongoza Mabaraza yao ya Mawaziri na watakuwa na nguvu ya kuteua na
kufukuza Mawaziri wanavyotaka. Hawatakuwa Wabunge katika Bunge la Muungano.

Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye Wajumbe wasiozidi 101 pamoja na
Rais wa Bunge la Muungano. Wabunge wa Muungano watatoka kwenye mikoa (au
Majimbo kama sera ya Majimbo itakubalika). Kwa utaratibu wa sasa kila mkoa
utachagua wabunge 2 mmoja mwanamke mmoja mwanaume kwenda Bunge la Muungano.
Wajumbe wa Ziada watatokana na uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata kwenye
kura za Rais wa Muungano. Idadi hii yaweza kupunguzwa na hata kuwa na Wabunge
51 tu akiwemo Rais wa Bunge la Muungano ambapo kwa mikoa ya sasa kila mkoa
utachagua Mbunge 1 na wengine watokane na uwiano. Rais wa masuala ya Muungano
atakuwa Mkuu wa Shughuli za Serikali katika Bunge la Muungano na Rais kwa mwaka
mara moja atahutubia Baraza la Taifa (Wabunge wa Bunge la Muungano na Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi kutoka kila upande wa Muungano). Wazungu wanaita
hotuba hii ‘State of the Union’ (Hali ya Taifa) na wengine huita ‘Queen’s Speech’ (Hotuba ya Malkia).

Mkuu wa nchi mmoja, Dola moja ya Jamhuri ya Muungano. Serikali  mbili na kila upande una Serikali yake yenye
mamlaka kamili ya maisha ya watu wao ya kila siku. Haya matatu pamoja na
Serikali ndogo ya Muungano. Lakini tutakuwa tumepata kila kitu labda. Wenye
kutaka Uhuru mpaka Zanzibar watapata. Wenye kutaka Tanganyika watapata na wenye
kutaka Muungano kama Dola yenye nguvu watapata.