HOTUBA YA MWENYEKITI WA UDASA KATIKA KUMBUKIZI YA MIAKA 20 YA PROF. CHACHAGE S. CHACHAGE

Familia ya Profesa Chachage
Ndugu Wanataaluma,
Wakereketwa wa Uhuru wa Kitaaluma
Marafiki na Wanafunzi waProfesa Chachage
Wapenda Haki Wote,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Habari za Mchana.

Tunakusanyika hapa leo tukiwa na hisia nzito kuadhimisha miaka 20 tangu kuondoka kwa mwanataaluma nguli, Profesa Chachage Seithy Chachage, ambaye maisha yake yote yalikuwa kielelezo cha utafutaji wa ukweli na utetezi wa haki za binadamu.

Profesa Chachage hakuamini katika elimu inayofungwa kwenye kuta za kumbi za mihadhara pekee; aliamini kuwa Chuo Kikuu ni taasisi inayotakiwa kujenga ujasiri wa kuhoji na kujenga hoja bila uoga.

Kwa wengi wetu ambao tumemfahamu Chachage kupitia maandiko yake, tunatambua kwamba Prof Chachage aliamini kwamba huru wa taaluma ni haki ya kipekee ya wasomi na jamii nzima. Kwamba,wanafunzi na walimu wao wana uhuru wa kufikiri na kuchambua masuala ya kitaifa na kimataifa bila kuingiliwa.

Hata hivyo, tunapomkumbuka Profesa Chachage leo, ni lazima tujiulize: Je, mazingira ya sasa ya kitaaluma nchini Tanzania yanairuhusu mbegu ya fikra huru aliyoipanda kukua?

Inasikitisha kwani siku za hivi karibuni, kumekuwa na mwelekeo wa kutishia uhuru huu kupitia ukamataji, mahojiano, na kufunguliwa mashitaka kwa wanataaluma kutokana na maoni au kauli walizotoa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma. Mifano ya hivi karibuni inatisha.

Kwa mfano, mnamo Julai 3, 2026, wahadhiri wawili wa Chuo Kikuu cha St. John walikamatwa wakiwa kazini. Mmoja alituhumiwa kwa kufundisha maudhui ya Maadili na Utawala Bora na kutoa mifano ya kashfa za Richmond na ESCROW ili kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa kuzingatia sheria. Vilevile, mwanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma naye alikamatwa, jambo linaloashiria mazingira ya hatari kwa wale wanaothubutu kuwa na mitazamo tofauti katika mambo mbalimbali yanayoendelea nchini. Kitendo cha Jeshi la Polisi la Tanzania kuwashikilia wahadhiri hawa kwa siku 17 bila kuwafikisha mahakamani ni kinyume cha sheria na ni unyanyasaji wa wazi wa uhuru wa wanataaluma kutoa maoni kwa ujumla.

Hali ya kutisha zaidi ni kugaidisha taaluma kwa lengo la kuleta hofu miongoni mwa wahadhiri wa Vyuo Vikuu. Kutokana na hali hii wanataaluma wenzetu wanaanza kujidhibiti kutoa maoni yao (self-censorship) kwa kuhofia madhara ya kisheria na kiutawala. Kitendo chochote cha kuwakamata na kuwafungulia kesi nzito wanataaluma wenzetu, na haswa kwa kutoa mifano ya kihistoria darasani, ni dhahiri kwamba tunaharibu ubora wa ufundishaji na kuwanyima wanafunzi fursa ya kujenga uwezo wa kufikiri kwa kina.

Tamko la hivi karibuni la Africa Coalition for Academic Freedom (ACAF) linaonyesha kuwa 72% ya matukio yanayofuatiliwa barani Afrika ni ukiukwaji wa uhuru wa taaluma, ikiwemo ukandamizaji wa Serikali. Tanzania isikubali kuwa sehemu ya takwimu hizi za aibu. Ili kuepusha aibu hii kwa taifa letu, UDASA tunazitaka mamlaka kuacha kuingilia uhuru wa kitaaluma.

Ndugu wanataaluma wenzangu na wageni wengine mliojumuika nasi leo, tunapaswa kurejea kwenye misingi ya Azimio la Dar es Salaam na Kampala (1990), ambayo yanasisitiza kuwa Vyuo Vikuu vinapaswa kuwa huru.

UDASA tunataka marekebisho ya Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005 ili kutambua uhuru wa taaluma kama haki ya msingi ya kisheria na siyo tafsiri ya kikatiba tu. Vyombo vya dola lazima vitofautishe kati ya shughuli halali za kitaaluma na vitendo vya jinai. Maoni yanayotolewa darasani yanapaswa kutathminiwa kitaaluma na siyo kijinai.

Ndugu watanzania wenzangu mlioko hapa na mnaotufuatilia kwa njia ya mtandao, tunapojadiliana na kumkumbuka Profesa Chachage leo, tusikubali vyuo vyetu vikuu viongozwe na hofu. Uhuru wa taaluma ni uhai wa taifa letu, na bila uhuru huo, tutazalisha wataalamu wanaoogopa kuuliza maswali magumu, jambo litakaloliangamiza Taifa letu. Kama ambavyo anatwambia John Dewey (1936): ‘Kukana uhuru katika elimu ni uhalifu dhidi ya demokrasia.’ Ni katika muktadha huo UDASA itaendelea kuwa katika msitari wa mbele kupigania uhuru wa kitaaluma.

Baada ya kusema haya, na sasa natamka kwamba majadiliano juu ya ‘Uhuru wa Kitaaluma na Mustakabali wa Vyuo Vikuu vya Afrika’ umefunguliwa rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza.

Elgidius Edgar Bwinabona Ichumbaki Mwenyekiti wa UDASA.