Iko wapi Diplomasia katika “Diplomasia ya Uchumi”?

Dastan Kweka

@KwekaKweka

Kiutaratibu, sera ya mambo ya nje ya nchi ni mwendelezo wa sera ya mambo ya ndani, na huainisha kanuni na misingi ambayo huongoza dola husika katika kujenga mahusiano na nchi nyingine, kukuza ushawishi, na kutetea maslahi yake. Pia, sera ya mambo ya nje, kama zilivyo sera nyinginezo, hupaswa kubadilika ili iendane na muktadha, kwa mfano; mabadiliko – ya ndani au ya nje – katika fikra, mienendo, au mitazamo.

Nchi yetu imeshuhudia mabadiliko makubwa ya kiutawala katika kipindi cha takribani miaka mitatu, tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani. Mabadiliko ambayo siyo tu yameathiri utekelezaji wa sera ya mambo ya nje ya Taifa letu, bali yanaashiria mwelekeo mpya kabisa wa kisera. Lengo la makala haya ni kuainisha nakisi iliyopo katika utekelezaji wa sera hiyo, kwa lengo la kuonesha wapi panahitaji maboresho.

 

Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje, toleo la mwaka 2001, imesimikwa katika dhana ya “diplomasia ya uchumi” –  dhana yenye lengo la kuhakikisha kuwa, mbali na malengo mengine, mfano ya kiulinzi, shughuli za kidiplomasia zinazoendeshwa na nchi yetu zinajikita katika kuujenga na kuuimarisha uchumi wetu. Utekelezaji wa sera hii, ambayo imekuwepo kwa karibia miongo miwili sasa, ulipaswa kuimarisha misingi muhimu ya “sera ya asili” ya mambo ya nje ya Tanzania, huku ukiongozwa na kanuni kadhaa, ikiwemo ya kulinda uhuru wa Taifa, haki za binadamu, na usawa na demokrasia (Ukurasa wa 11).

Sera ya asili ya Mambo ya Nje ilikuwa na misingi yake – “fundamental principles of Tanzania`s foreign policy” – ambayo ni ile iliyokuwa katika sera ya mambo ya nje ya serikali ya awamu ya kwanza, na ilihusisha kuunga mkono juhudi za kujikomboa za watu, na mataifa yanayoonewa. Usimamizi thabiti wa msingi au kanuni hii, na nyinginezo, hasa wakati wa harakati za uhuru, na vita vya ukombozi, uliipatia Tanzania heshima kubwa Afrika, na duniani. Hata hivyo, ni wazi kuwa ingawa sera ya sasa ya mambo ya nje imeainisha haja ya kuimarisha misingi hiyo ya asili, kuna ushahidi wa wazi kuwa imeshatelekezwa. 

Kwa mfano, tumeona Tanzania ikianzishamahusiano ya kibalozi na Israeli, na kujivuniakupokea watalii kutoka nchi hiyo, huku mgogoro baina ya nchi hiyo na Mamlaka ya Palestina ukibaki kuwa kitendawili. Pia, tumeona nchi yetu ikiimarishamahusiano na nchi ya Morocco, na kupokea misaada kadhaa, huku suala la Sahara Magharibi likibaki bila ufumbuzi. Tafsiri ya dhana ya diplomasia ya uchumi, katika muktadha wa mabadiliko haya, ni kuwa, yeyote mwenye fedha, teknolojia, au kingine chochote tunachokihitaji, hata akiwa dhalimu, ni swahiba wetu. 

Hoja ya msingi kuhusu kubadilika kwa mahusiano baina ya nchi yetu na Israeli, au Morocco, siyo mabadiliko peke yake. Mabadiliko haya yangeweza kuwa muhimu, kwa mfano, kama yangejikita kwenye haja ya kubadili mbinu. Ajabu ni kuwa, tunaambiwa mabadiliko haya ni muhimu kwa sababu za kiuchumi, basi. Ni kama vile, kwa kuimarisha mahusiano na nchi hizi hali yetu kiuchumi itaboreka kabisa. Ajabu!

Mwenendo wa utekelezaji wa sera yetu ya mambo ya nje unaonesha kuwa, watawala wanadhani inawezekana, na ni sawa, kwa dola kusukuma ajenda zake katika ngazi ya kimataifa, bila kulazimika, au kulazimishwa, kuheshimu misingi na kanuni muhimu, hata zile ambazo Taifa limejiwekea lenyewe katika sheria na sera zake. Kwa mfano, mojawapo ya kanuni ya msingi  katika sera yetu ya mambo ya nje inahusu ulinzi wa uhuru, haki za binadamu, usawa na demokrasia. Bila shaka, kanuni hii ina msingi wake katika Katiba ya nchi yetu (1977). Kwa hiyo, tumeiambia dunia kuwa hii ndiyo misingi tunayoiheshimu na kuithamini. 

Ajabu ni kuwa, serikali inatarajia jamii ya kimataifa ikae kimya pale inapoonekana kukiuka misingi hii, na kutowajibika kwa namna yoyote ile, hata pale baadhi ya miili ya raia wake inapoibuka baharini, kutekwa, au kunusurika kifo katika mashambulio mbalimbali. Sikitiko ni kuwa, nchi ambayo kwa miaka mingi ilifahamika kwa kukemea uovu, uonevu na ukandamizaji uliofanywa na mataifa ya Magharibi, hasa nyakati za ukoloni, sasa imegeuka ya kukemewa kupitia (ma)azimioyatolewayo na jamii ya kimataifa, ikiwemo Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Mkemeaji amegeuka mkemewaji. 

Historia inaonesha kuwa, suala la haki za binadamu limetumiwa mara kadhaa na mataifa yenye nguvu duniani kuingilia uhuru wa nchi nyingine, hasa zinazoendelea, na kuleta dhahama kubwa. Mfano mzuri, na unaopendwa na “viongozi” wetu, ni Libya. Jumuiya ya Kimataifa imeweka misingi ya kuingilia uhuru wa nchi nyingine, hasa pale ambapo waliopewa mamlaka wameshindwa, au hawana motisha ya kusimamia haki za watu wanaowaongoza. Na, hatua za mwanzo za kuingilia uhuru huanza kwa maazimio, yakiwa na lengo la kujenga uhalali wa hatua zaidi. Madhara ya maazimio ni kumomonyoa heshima ya nchi, na ushawishi wake, ikiwemo katika nyanja za kiuchumi. 

Wakati fulani katika historia, Tanzania ilikua Taifa masikini, lakini ambalo lilipata heshima kubwa kwa kusimamia utu na haki, na kupinga uonevu na udhalilishaji. Tulipaswa kuendelea kusimamia misingi hii, ndani na nje, huku tukiweka juhudi katika kujenga nguvu yetu ya kiuchumi. Kwa kukanyaga misingi hii, Taifa limefungua milango ya kuingiliwa, kubezwa ama kubagazwa, na kupuuzwa. 

Mwanzoni mwa miaka ya sitini, Mwalimu Nyerere alitoa muongozo maarufu wa kisera juu ya namna ya kushughulika na sera ya mambo ya nje, uliokuwa na jina la kimombo, “Argue, Don’t Shout.” Tafsiri isiyo rasmi ni, “Jenga hoja, Usipayuke.” Katika utangulizi wa muongozo huo (ukurasa wa 11), yaliandikwa yafuatayo (nanukuu);

 “Tunataka ama kushawishi watu, au kuwafanya waelewe ni kwa nini tumechagua mwelekeo fulani. Na kwa yoyote kati ya malengo haya, tunapaswa kujenga hoja, siyo kupayuka.” (Tafsiri yangu, ukurasa wa 11).

Kuna dalili za wazi kuwa, kama Taifa tumeanza “kupayuka”, badala ya kujenga hoja. Mfano mzuri ni namna ambavyo nchi imekabiliana na madukuduku ya jumuiya ya kimataifa juu ya hali ya haki za binadamu, uhuru wa kujieleza, kujumuika na kukusanyika. Hatua ya kumfukuza balozi wa Umoja wa Ulaya nchini ilifuatiwa na taarifa nyingi zenye mwenendo wa kubomoa jina, na hadhi ya nchi. Majibu yetu yakawa duni, na yasiyojitosheleza. Kimsingi, ni hatua iliyoishia kudhoofisha mahusiano, na jina la nchi. Ni mgogoro wa kidiplomasia ulioanzishwa wakati ambao nafasi ya nchi kidiplomasia ni duni kabisa.

Tatizo kubwa katika utekelezaji wa sera ya mambo ya nje, kwa sasa, ni mkanganyiko (contradictions) kati ya hatua ambazo taifa linachukua, na malengo ambayo linataka kufikia. Kwa mfano, wakati tunadai hizi ni zama za diplomasia ya uchumi, ushiriki wa Taifa letu katika diplomasia ndani ya bara letu, na hata nje, unafanyika zaidi katika ngazi “za chini”, yaani waziri, na mabalozi. Kwa uwiano, ni mara chache unahusisha Rais, Waziri Mkuu au Makamu wa Rais. 

 

Athari ya aina hii ya utendaji imekua ni kutuma ujumbe, kwa jamii ya kimataifa, kuwa nchi yetu haioni umuhimu wa kuweka mkazo katika muhusiano, na kwamba siyo ya kutegemewa, kama ilivyokuwa zamani. Na ndivyo ilivyo; nchi yetu kwa sasa inaangalia ndani zaidi(inward looking), na imeacha ombwe la uongozi katika jamii ya kimataifa, ikiwemo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Na, sababu ni kuwa kiitikadi (soma misingi, lugha isiyo na ukakasi), tumeyumba.

Mfano mwingine wa mkanganyiko unaonekana katika nia ya taifa letu kujiimarisha kama ushoroba wa biashara katika ukanda wa maziwa makuu, kwa upande mmoja, na namna ilivyokabiliana na mgogoro wa Burundi, kwa upande mwingine. Ushiriki, na juhudi za usuluhishi za Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, zimedunishwa sana na mwenendo wa mahusiano ya nchi yetu na Rwanda. Diplomasia ya uchumi, katika muktadha huu, ilipaswa kuhusisha taifa letu kujitanabahisha kuwa liko juu ya mgogoro husika.

Kuna changamoto za kimkakati pia. Kwa mfano, watawala walitangaza “vita ya kiuchumi” katika wakati ambao pia wanaonekana kuazimia kuweka mkazo katika diplomasia ya uchumi. Tatizo ni kuwa, vita ya kiuchumi inadunisha, au kufuta kabisa (negate) juhudi kiduchu za diplomasia ya uchumi. Haiwezekani kuendesha vita ya kiuchumi nyumbani, na diplomasia ya uchumi ugenini, na usitarajie madhara (hasi). Hili siyo suala la mapungufu kuhusu uzuri, au ukuu wa lengo, bali nakisi katika mbinu. 

Tanzania, chini ya serikali ya awamu ya tano, ina malengo makubwa, na yenye kutia shauku. Changamoto kuu katika kufikia malengo hayo, hasa katika nyanja ya sera ya mambo ya nje, ni mkanganyiko katika utekelezaji wa sera hiyo. Mkanganyiko huu ni mkubwa kiasi kwamba sisi tunaotazama kutoka pembeni tunashindwa kuiona diplomasia katika inayoitwa diplomasia ya uchumi.