CCM katika ncha ya Mpasuko: Jinamizi la
Urais wa Lowassa 2015

Richard Mbunda

Idara ya Sayansi ya Siasa
(UDSM)

Siasa za Tanzania ni za pekee?

Siasa za Tanzania zimekuwa
na upekee katika mambo kadha wa kadha. Ni upekee huu unazozifanya siasa za
Tanzania kutokutabirika na kuwavutia wachambuzi wengi sana. Kwa mfano, huko
duniani, umaarufu katika siasa ni chachu kubwa ya mgombea kuchaguliwa katika
uchaguzi. Lakini hapa Tanzania hali inaweza kuwa tofauti. Mwaka 1985 wakati
Mwalimu Nyerere anang’atuka, hakuna aliyetarajia kuwa Mzee Mwinyi angemrithi.
Macho ya watu yalikuwa kwa mwanadiplomasia mahiri Afrika Salim Ahmed Salim,
ambaye inasadikiwa pia alikuwa chaguo la Mwalimu Nyerere. Walakini haikuwa
hivyo.

Mwaka 1995 wakati Mzee Mwinyi anamaliza muda wake, kuna
sura kadhaa zilizobeba umaarufu mkubwa sana ndani ya Chama cha Mapinduzi. Kiumaarufu,
mtakubaliana na mimi kuwa John Samwel Malecela, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa
kipindi hicho, Edward Lowassa na Jakaya Kikwete walikuwa maarufu zaidi ya Rais
Benjamin Mkapa. Kuna baadhi ya maandiko yanamkariri Mwalimu Nyerere akisema
kuwa tusiangalie umaarufu ‘…. Kama umempenda kwa kuwa ni mtu maarufu nenda
kanywe naye chai…’ Hii inasaidia kutuonyesha kuwa watu maarufu walikuwepo,
lakini kutokana na mfumo uliokuwepo hawakuweza kuchagulika.

Upekee mwingine unatokana na nafasi ya Rais na Mwenyekiti
wa chama anayemaliza muda wake kumteua anayempendekeza kuwa mrithi wake
madarakani. Katika historia ya nchi, tangu Baba wa Taifa mwenyewe hakuna Rais
aliyeweza kumweka mgombea wa pendekezo lake madarakani. Simulizi za kisiasa
zinaonyesha kuwa Mwalimu Nyerere alishindwa kumweka Dkt. Salim A. Salim
madarakani mwaka 1985. Mzee Mwinyi naye alikosa fursa hii adhimu mwaka 1995
pale ambapo Mwalimu Nyerere kama Baba wa Taifa alipotumia nafasi yake
kuhakikisha chaguo lake, Ben Mkapa anaingia madarakani. Pamoja na uwezo,
heshima aliyojijengea na ushawishi Mzee Mkapa pia, hakuweza kushawishi
ataeuliwa mgombea aliyemtaka ili awe Rais pale alipomaliza muda wake 2005.

 Kuna sababu kuu mbili zinazoelezea hali hii ya Rais
anayemaliza muda wake kushindwa kumweka mrithi. Mosi, Rais anapomaliza muda wake
anakuwa hana mamlaka ya kidola ya kushurutisha watu. Kuna kiongozi mmoja
mwandamizi aliwahi kuniambia kuwa, mwaka mmoja kabla ya tarehe ya uchaguzi,
Rais huwa hapewi usikivu kwa asilimia mia moja. Hivyo ni vigumu kushurutisha
watu waenende kulingana na matakwa yake. Lakini la pili ni kuwa, watu tayari
wanakuwa wameshajipanga na kuunda mitandao ya ushindi. Mara nyingi Rais
anayemaliza muda wake anajaribu kukwepa mitandao hii kwa kuwa kama
isipofanikiwa anahatarisha kuingia katika mgogoro na Rais atakayemrithi.

Hata hivyo, binadamu wanatofautiana na mara nyingi
hawatabiriki. Siasa ni kamari, na wacheza kamari hawaogopi madhara bali
husukumwa na faida. Kwa kuzingatia historia ya nchi yetu, viongozi wakuu wa
nchi katika awamu zote nne unaweza kuwaweka katika makundi mawili. Kuna wale ambao
walizingatia utawala wa dola tu. Mzee Mkapa na Mzee Mwinyi wanaangukia katika kundi
hili. Kwa upande wa Mzee Mwinyi, sababu mojawapo ilikuwa ni Mwalimu kuendelea
kuwa Mwenyekiti wa chama kwa miaka kadhaa baada ya kung’atuka urais. Na hata
alipopewa kofia ya chama, bado hakuonyesha hamasa ya kukitumia chama ili kufanikisha
malengo yake. Mzee Mkapa, angetamani hata huo uenyekiti wa chama angepewa
mwingine ili yeye abaki na serikali.

Mwalimu Nyerere na Rais wa sasa Jakaya Kikwete ni watu
waliopenda kuzitumia kofia zote mbili. Ikumbukwe kuwa Mwalimu Nyerere aliwahi
kujiuzulu Uwaziri Mkuu mara tu baada ya Uhuru ili akakijenge chama. Mwalimu
alikitumia chama kama nguzo kuu ya maamuzi. Wakati wa mfumo wa chama kimoja
maamuzi mengi muhimu yalitoka kwenye chama, ambako alikuwa mwenyekiti. Rais
Kikwete pia, ni mtu aliyekulia kwenye chama na anajua umuhimu wa chama na siasa
ndani ya chama. Pia kwa hulka yake, Rais Kikwete ni mwanasiasa asiyekubali
kushindwa. Kwa mantiki hiyo basi, ni vigumu kusema hataweza kuelekeza mchakato
wa kumteua mrithi wake. Ana nafasi kubwa sana ya kufanya hivyo, na ni matumaini
yangu kuwa atapenda afanikiwe katika hili.

Kwa wale wanaobeza uwezo wa Rais anayemaliza muda wake
kuelekeza mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
ningependa kuwasihi wamwangalie Rais Kikwete katika jicho tofauti. Ningependa
kuwakumbusha mambo machache: mosi, mgogoro wa kurithishana madaraka Zanzibar,
ambapo Mh. Gharib Bilali aliona kuwa sasa ilikuwa zamu yake. Kikwete
alifanikiwa kumweka Dr. Shein Zanzibar. Pia, mwaka 2010 katika mchakato wa
kumchagua Spika wa Bunge, Rais Kikwete aliwashtua watu na chaguo lake. Kuna
baadhi ya wanasiasa hawajui walipigwa na kitu gani. Lakini Mh. Anne Makinda
aliibuka kuwa Spika hata sasa.

  

Mwenyekiti yupo Kambi ipi?

Swali ambalo lilikuwa rahisi miaka 10 iliyopita sasa
linaonekana gumu sana. Wachambuzi wa Kitanzania watakumbuka mtandao madhubuti
ulioundwa na Timu iliyomhusisha Edward Lowassa na wapambe wake kuhakikisha Rais
Kikwete anaingia Ikulu. Mtandao huu ulimpa Ushindi wa kishindo Rais Kikwete.
Hivyo basi, ilitarajiwa kuwa Rais Kikwete awe upande wa Lowassa kwa mantiki ya
yeye kulipa fadhila. Lakini hali haipo hivyo. Mimi nilikuwa wa kwanza
kukimbilia kitabu cha wasifu cha Rais Kikwete kilipotoka, ili nijue kitu gani
kilitokea mpaka waziri wake mkuu akajiuzulu 2008. Sikuridhika na maneno tu kuwa
‘ilikuwa ajali ya kisiasa’. Kwa bahati mbaya, sikuona lolote la maana katika
kipengele hicho kwenye kitabu hicho.

Hata hivyo, kuna viashiria vingi vinavyoonyesha kundi
hili, lililojulikana maarufu kama “Boys II Men”, limesambaratika. Waandishi wa
habari wamekuwa wakiuliza maswali na wamekuwa hawaridhishwi na majibu
wanayopewa. Aliulizwa Lowassa katika mkutano wake na Wahariri kule Dodoma, na
kwa kuwa swali lilijirudia mara nyingi likamkasirisha. Vijana wa ‘www.com’ wanamsemo
kuwa ‘kusoma hujui na picha huioni?’ Waandishi wa habari wametusaidia kurekodi
kauli zinazopingana. Wakati anatangaza nia kule Arusha, Lowassa alibainisha
kuwa alimuunga mkono Kikwete 2005 na 2015 ni zamu yake kuungwa mkono. Lakini
Rais Kikwete alipoulizwa na Mwanadiplomasia wa Marekani June 9 kama atamuunga
mkono Lowassa alisema yeye hana mgombea. Na hata kama anaye kura yake ni moja
tu. Ingawa kauli hii inalenga kuonyesha kuwa Mwenyekiti wa chama hapaswi kuwa
na mgombea au sehemu ya mtandao, lakini kwa wawili hawa inasadikiwa palikuwa na
yamini. Majibu kama haya yanaweza kutupa dondoo tu ya uhusiano wao kwa sasa.

 Mzee Kingunge alitufunua macho pia alipowaasa wawili hawa
kupatana wakati akihutubia siku Lowassa alipotangaza nia kule Arusha. Wito wake
wa kutaka wawili hao kupatana kutokana na historia yao ya kisiasa unatuonyesha
kuwa hali ya uhusiano wao sio shwari. Lakini suala la kuhasimiana katika siasa
sio jambo geni. Wananadharia za kihalisia wanasema hakuna urafiki wa kudumu
katika siasa bali masilahi ya kudumu. Hata hivyo, wito wa Mzee Kingunge una mantiki
kubwa. Kwa sababu ikiwa maswahiba hawa wa zamani sasa wanapambana kwa namna
yeyote madhara yake yatakuwa makubwa sana kwao binafsi na hata kwa chama.
Makala hii ndefu ina jaribu kubashiri (project) kinachoweza kutokea katika
mchakato huu wa uteuzi.

Siasa za Umaarufu

Umaarufu katika siasa ni silaha muhimu sana. Na
unatafsiriwa katika uwezo wa kuvuta watu katika mikutano yako, na kuwa midomoni
mwa wananchi muda wote. Umaarufu unaanza na mtu. Kwa wanasiasa wajanja zaidi,
huupamba umaarufu kwa sera za kuvutia, na ahadi zinazoendana na matakwa ya
wananchi. Mwaka 2005 Rais Kikwete alikuwa maarufu kiasi kwamba watu wakadhani
ataumaliza kabisa upinzani. Na ahadi yake ya maisha bora kwa kila mtanzania
iliwafanya wapiga kura ‘warukwe na wazimu’. Lakini mwisho wa siku ni maneno tu,
katika dhana nzima ya umaarufu.

Katika kinyang’anyiro cha mwaka huu Edward Lowassa ndio
habari ya mjini. Jina lake limekuwa midomoni mwa watu kuanzia mijini mpaka
vijijini. Prof. Kitila Mkumbo alitanabaisha katika makala yake kuwa Lowassa ana
ufuasi ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi. Ingawa wapinzani wake wamekuwa
wakibeza umaarufu wake kwa vigezo kuwa anawanunua watu, lakini uhalisia wa
madai haya una walakini. Ni vigumu kudhani kuwa Lowassa ni trilionea mkubwa
sana anayeweza kuwalipa maelfu ya wananchi wanaojitokeza kumuunga mkono kila
anapojitokeza! Na kama anaweza kufanya hilo, nitashangaa kuona vyombo husika
vikilifumbia macho hili, kwa kuwa ni kansa inayolitafuna taifa. Lakini kuna
watu wanaosifu timu yake kwa kuweza kuwaleta karibu na Lowassa watu wote hao. Na
kama madai haya ni kweli basi anastahili sifa ya kuwa mhamasishaji mzuri. Ni
vyema tukasema pia kuwa, kwa wagombea wote waliojitokeza, hakuna mwanasiasa
anayemkaribia Lowassa kwa ‘umaarufu’. Na Lowassa amekuwa akitumia umaarufu huu
kama karata yake ya turufu kuwafanya CCM wajue anakubalika. Je, CCM
watashawishika?

Siasa za Uteuzi

Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikijinadi kuwa mchakato
wake wa uteuzi wa wagombea ni wa kidemokrasia sana. Lakini kuihalisia, hasa
katika ngazi ya wagombea wa Urais kamati mbili za awali zinaweza kutoa
maelekezo. Kamati ya Usalama na Maadili ndio chombo cha kwanza kuwajadili watia
nia. Kamati hii hujadili majina haya kwa kina, kwa kumptia kila mgombea na
kisha kutoa mapendekezo kwa Mwenyekiti wa Chama. Kwa mujibu wa mmoja wa makada
maarufu wa CCM, ripoti ya Kamati ya Usalama na Maadili huwa ni ya siri.
Kiujumla, Kamati hii huundwa na sekretatiati pamoja na wakuu wa Idara mbalimbali
kama vile Uenezi, Mambo ya Nje, Oganaizesheni, Uchumi na Fedha, na Uendeshaji.
Kila mgombewa hupewa alama (grade).

Kamati ya pili inayopitia majina haya ya wagombea ni Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC). Wajumbe wa Kamati hii ni pamoja na Rais
wa Jamhuri, Makamu wa Rias, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Spika, Wenyeviti wa
Jumuiya na Wajumbe 14 wa kuteuliwa. Kamati hii ina mamlaka ya kuchagua majina
matano kati ya majina ya wagombea wote ambao watapelekwa katika kamati ya Halmashauri
Kuu ya Taifa (NEC) ili yapigiwe kura. Ingawa Kamati ya Usalama na Maadili nayo
ina nafasi yake katika kutoa mapendekezo, Kamati Kuu ya Taifa ndiyo kikwazo
kikubwa cha harakati za wagombea akiwemo Edward Lowassa kuendeleza safari yake
ya matumaini.

Bundi katika Kambi ya Lowassa

Pamoja na umaarufu wake ambao umejidhihirisha katika kila
kona ya nchi alikopita kutafuta wadhamini, wachambuzi wameyasema mambo kadhaa
ambayo yanaitia dosari safari yake ya matumaini. Kati ya hayo, makubwa ni mawili.
Mosi, amekuwa akituhumiwa sana kwa ufisadi. Tangu miaka ya 1990, maswali
yamekuwa yakiulizwa kuhusu utajiri wake. Ingawa hakuna takwimu sahihi za
utajiri huo [kwa maana sijawahi kuliona jina lake katika gazeti la Forbes Africa] lakini tuhuma hizi
zimekuwa sehemu ya maisha yake ya kisiasa. Inasadikiwa kuwa, Mwalimu alimkataa
Lowassa kwa sababu ya utajiri huo ambao chanzo chake hakielezeki. Kilele cha
tuhuma ilikuwa na kashfa ya kampuni ya kufua umeme maarufu kama Richmond, mwaka
2008. Lowassa akiwa Waziri Mkuu alipinga tuhuma hizo akidai kuwa wapinzani wake
walikuwa wanautaka Uwaziri Mkuu. Hivyo basi, aliamua kujiuzulu ili tu awape
amani wapinzani hao. Wananadharia za Kihaini (Conspiracy Theorists)
walimhusisha pia ‘Mkuu wa Kaya’ katika anguko la ‘Bwana Mkubwa huyu,
wakidhahania kuwa, alikuwa ‘akimfunika’ Rais katika utendaji wake, hivyo
ilimpasa kuondoka.

Hivi karibuni Lowassa amejitahidi kujibu tuhuma hizo na
kuna kauli mbili nzito alizozitoa. Ya kwanza aliitoa kwa waandishi wa habari
Dodoma akidai kuwa, Richmond haikuhusisha pesa hata senti tano, na yeye
mwenyewe ndiye aliyezuia malipo ya aina yoyote yasifanyike kwa kampuni hiyo
mpaka pale ambapo wangekuwa wamejiridhisha. Aliendelea pia kusema kuwa
[waandishi wa ripoti hiyo ya kamati teule ya Bunge] wanapaswa kuona aibu kwa
kuwa mitambo ya Richmond ilionekana bora zaidi katika kufua umeme na
ikathibitishwa na Rais wa Marekani Barack Obama na (aliyekuwa) waziri wake Hillary
Clinton walipokuja kuzuru nchini. Kauli ya pili ameitoa hivi karibuni aliposema
mtu anayemtuhumu kwa ufisadi na ana ushahidi basi na amtaje. Ukweli  ni kuwa mpaka sasa tuhuma za ufisadi dhidi ya
mtia nia huyu hazijawahi kuthibitishwa. Kisheria, mtu huyu anapaswa kudhaniwa
kuwa si mkosaji mpaka ithibitishwe. Lakini kisiasa, vipimo tofauti vinatumika.
Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, Rais wa nchi hapaswi hata ‘kutuhumiwa’ tu. Kauli
hii ya Nyerere inaweza kuwa imepitwa na wakati, kwa kuwa kutuhumiana miaka ya
sasa imekuwa mbinu ya kisiasa. Spika wa zamani, Samwel Sitta aliiita mbinu hii
‘siasa za maji taka’. Kuthibitisha hilo, takribani watia nia wote wa CCM
wameshawahi kutuhumiwa kwa namna moja au nyingine hasa hasa katika mambo ya
ufisadi.

Doa la pili ni lile la afya yake. Wachambuzi wamemuandika
Lowassa kuwa ni mdhaifu wa afya.  Kuna
baadhi ya wachambuzi wanadhani mtia nia huyu ni mdhaifu. Hata hivyo, Lowassa
amejitahidi kuonyesha uimara (u-fit) wake kwa maneno na matendo. Katika moja ya
mikutano yake na waandishi wa habari Lowassa alisisitiza yuko ‘fit’ kiafya na
akasisitiza yeye na watia nia wenzake wapimwe afya na jopo la madaktari wa
ndani nje ya nchi. Walakini, majibu haya hayajawatosheleza wengi na swali juu
ya afya ya mtia nia huyu bado lipo kwenye midomo ya Watanzania walio wengi.

Mustakabali wa Lowassa

Ni vyema tuakaanza na mtazamo chanya. Akiteuliwa Lowassa,
je, ataweza kuihakikishia CCM ushindi dhidi wa wapinzani wake? Hilo ni swali
gumu, hasa pale ambapo upinzani wamekaa kimya wakisikilizia. Hata hivyo,
Lowassa anabebwa na kura za maoni zilizoendeshwa na baadhi ya Taasisi za
utafiti nchini. Kwa mfano, kabla hata hawajatangaza nia, TWAWEZA walitoa majibu
ya maoni yao na walimtangaza Lowassa kama ndiye anayeongoza kwa kukubalika. Inasadikiwa
pia kuna utafiti ulifanyika hivi karibuni, ambao unaonyesha pia Lowassa anakubalika
zaidi kuliko Dr. Wilbrod Slaa wa UKAWA. Tafiti hizi zinatoa taswira kuwa
Lowassa ana mvuto na anachagulika. Hatujui atakubalika kwa kiasi gani kwani
atakuwa na tuhuma lukuki za kujibu kutoka kwa wapinzani wakati wa kampeni.
Anachoweza kujipa moyo ni kuwa takribani tuhuma zote zimeshatajwa. Yawezekana
wapinzani wake hawatakuwa na kashfa mpya ambayo itatikisa kampeni zake. Kwa
utabiri wangu akiwa mgombea wa CCM anaweza kupata ushindi usiozidi 70%.

Hata hivyo, pamoja na mvuto wake, Lowassa ana kibarua kigumu
kuhakikisha jina lake linapitishwa. Kauli za Mwenyekiti wa CCM akiwa katika
maazimisho ya miaka 125 ya KKKT huko Mbuyukenda, yaliyofanyika mnamo Julai 5,
2015 jijini Tanga imezidi kutia shaka kama kweli Lowassa atapenya. Bila
kujiumauma Mwenyekiti aliwataka Viongozi wa dini nchini kukemea wanasiasa
wanaopenda madaraka na wanaotumia pesa ili kununua ushindi. Mwenyekiti
alihitimisha kuwa, watu wa namna hii watalifikisha taifa pabaya. Ingawa watia
nia wengi wametumia pesa kusaka ushindi, lakini kauli hii inashabihiana na
tuhuma zilizoelekezwa kwa Lowassa na wapinzani wake katika mchakato wa uteuzi.
Kimfumo, mwenyekiti wa chama ana ‘kura ya turufu’ katika vikao vya awali vya
mchujo ambavyo havihitaji uwingi wa kura. Kama alichokiongea Mwenyekiti ndicho anachokiamini,
kuna walakini kwamba jina la mwanasiasa huyu mwenye mvuto litapita katika
kamati hizo.

Athari kwa CCM kama jina la Lowassa likikatwa

Mambo makuu matatu yanaweza kutokea kama jina la Lowassa
halitapita kwenye mchujo wa wagombea. MOSI, Lowassa mwenyewe amesema hatahama
CCM na asiyemtaka CCM aondoke yeye. Kwa kauli hii, tutegemee Lowassa kukubali
kuwa ameenguliwa katika mchakato halali wa chama na atangaze kumuunga mkono aliyependekezwa
na chama. Dhahania kuu katika mazingira haya ni kuwa viongozi wa chama wamekaa
naye wakaongea kwa kina na wakakubaliana kuwa chama kwanza maslahi binafsi yaje
baadaye. Katika hali hii, ambapo Lowassa atakuwa amewaomba wafuasi wake
kumuunga mkono mteule wa Chama kuna uwezekano chama kitafanya vizuri. Lakini
kutokana na mvuto uliofifia kwa hao wagombea wengine, CCM itapata ushindi mwembamba tu katika uchaguzi wa
huru na haki.

Suala la kuzingatia katika mazingira haya ni mmpeperusha
bendera mteule awe ameshafanya mazungumzo na Lowassa na wameafikiana. Hata
hivyo, kuna ugumu sana wa kufikia mazingira hayo kwa sababu kuu mbili: Lowassa na kambi yake wanaamini kuwa
wanachagulika
, na wanajinadi kuwa ni chaguo la watu na ana uzoefu wa
kiuongozi. Na pia, Lowassa alimuunga mkono
Mwenyekiti wa sasa miaka kumi iliyopita na sasa anaona ni zamu yake kupeperusha
bendera wa CCM
.

Mazingira ya PILI ni yale ambapo Lowassa baada ya kukatwa
akaamua kukaa kimya kabisa. Asiseme chochote. Kikubwa anachoweza kufanya ni
kustaafu siasa maana ni mchezo uliomshinda. Hali hii inaweza kutafsiriwa na
wafuasi wake kuwa ameonewa na wakaamua kukisusia chama. Mwenyekiti wa CCM mkoa
wa Iringa alidokeza mazingira kama haya hivi karibuni akidai kuambiwa na vijana
wa mkoa huo kuwa, kama CCM ikimkata Lowassa basi vijana ‘wataizingua’ CCM. Kwa
maono yangu, hali ikiwa hivi na UKAWA wakawa wamejipanga vizuri, watatoa
upinzani mkubwa sana kwa CCM. Hali ya kuchagulika kati ya CCM na UKAWA inaweza
ikawa ni 50 kwa 50. Sababu zingine zozote zitaufanya upande wowote kushinda.

 Mazingira ya TATU ni pale ambapo Lowassa hataridhika na
mchakato wa uteuzi na akaamua kuondoka CCM.
 Kutokana na uzito wa jina lake Lowassa anaweza
kutua UKAWA au akaamua tu kwenda katika chama kimojawapo kama vile ACT-Wazalendo.
Labda tuanze na uwezekano wa yeye kwenda UKAWA. Kumekuwa na minong’ono mingi
kutoka kwa baadhi ya watu ndani ya mfumo, wakidai kuwa kuna makubaliano yasiyo
rasmi kuwa watamkaribisha Lowassa akikatwa. Labda swali la kujiuliza ni,
akitua UKAWA Lowassa anaweza kubadilisha
hali ya upinzani kuchagulika? UKAWA wanaweza kuwa na kazi nyepesi mno ya
kumnadi Lowassa
. Kukosekana kwa ushahidi wa wazi katika tuhuma za ufisadi
dhidi ya Lowassa kunampa nafasi kubwa ya kuonekana kuwa ameonewa katika
mikwaruzano ya kugombea madaraka ndani ya CCM kama mwenyewe alivyosema wakati
anajiuzulu Uwaziri Mkuu. Hali itakuwa ngumu kwa CCM kama wataamua kumnyooshea
Lowassa vidole au kuanza kufukunyua kashfa zake. CCM ndio wamemlea Lowassa
mpaka alipofika na wamekuwa wakitetea chama chao ni cha wasafi. Kumnyooshea
kidole Lowassa ni sawa na kurusha mawe kwenye nyumba yao wenyewe.

Kutokana na skendo nyingi zilizoendelea kuikumba CCM
wapinzani watakuwa wamepandisha idadi ya kura zao kwa asilimia kadhaa. Katika
uchaguzi wa mwisho walikuwa na jumla ya asilimia 38. Mwaka huu wanaweza kuwa na
angalau 40%. Kwa maono yangu, kiwango hiki kinaweza kucheza kati ya asilimia 30
– 45 kutokana tu na wagombea wa pande zote mbili, mambo mengine yakibaki kama
yalivyo. Kwa hali ilivyo basi, Lowassa ana takribani asilimia 20 – 30 [kadirio
la chini nusu ya asilimia 60 za CCM] ya wana CCM wanaomuunga mkono kwa hali
yeyote. Kama hesabu hii ikaletwa katika muktadha wa sanduku la kura, na Lowassa
akafanikiwa kuondoka na wapiga kura wake wote, UKAWA ina nafasi ya kuleta
upinzani na kuyafanya matokeo yawe 50-50 au wakafanikiwa kushinda kwa silimia
50.01 – 55. Kuna uwezekano mkubwa pia kwamba wabunge wa CCM watapungua sana, na
hivyo kuwanyima uhuru wa kutawala mhimili huo wa dola.

Je, kama Lowassa hakubaliki UKAWA, nini
hatima yake?

Kuna tetesi kuwa Lowassa amekuwa akifadhili shughuli za
ACT. Ni chama kipya, lakini ilikuwa lazima kiongozi wake Zitto Kabwe azunguke
Tanzania nzima kukinadi ili kukifanya kijulikane. Na kwa ujumla, Chama hiki hakiwezi
kubezwa kwa jinsi kilivyovuta watu kwenye baadhi ya mikutano yake. Hatuwezi
kukwepa ukweli pia, kama ilivyo Kenya, yawezekana Tanzania tunafikia hali ya
watu kuwa na vyama na sisi tukawa tunafuata watu na sio vyama. Kama Lowassa
akiamua kwenda ACT hali inaweza ikawa kama ifuatavyo: ACT Wazalendo na Zitto
Kabwe tayari wameshafanya kauharibifu katika vyama vya upinzani hasa CHADEMA.
Wafuasi wa Zitto amehama nao kutoka CHADEMA. Tumeona orodha ya viongozi wa
vyama vya siasa wakijitangaza kuhama CHADEMA na CUF. Bila shaka na wanachama wa
kawaida wamehamasika pia. Lakini ujio wa Lowassa utatoa mng’ao mpya kwa  ACT-Wazalendo. Kuna uwezekano chama hiki
kikaharibu hali ya siasa nchini kwa kuvuta hisia za mashabiki wengi ambao
wataondoka UKAWA na CCM.

Kimahesabu, hali inaweza ikawa hivi: tunaweza kusema kuwa
ACT wana mtaji wa 2% kama wakisimamisha mgombea leo. Lakini mgombea akiwa na
mvuto zaidi wanaweza kufikisha 7%, ambazo watazitoa katika vyama vya upinzani.
UKAWA watabaki na 33%. Akiingia Lowassa akaja na 30% kutoka CCM basi ACT
itakuwa na idadi ya 37% ya kura zote. CCM kwa upande wao watabakiwa na 30%. Mfumo
wetu wa uchaguzi katika katiba ya sasa mshindi hupatikana kwa wingi wa kura tu (simple majority). Katika muktadha huu,
ACT na Lowassa wanaweza kuwa washindi. Hata hivyo, kuna vigezo (factors) muhimu
vya kuzingatia. Mosi, uchaguzi lazima uwe huru na wa haki. Kutakuwa na mbinu
nyingi za kutaka kuiba kura. UKAWA na ACT itabidi wawe macho ili kura
zisiibiwe. Lakini wizi wa kura utategemea vipi vyombo vya ulinzi na usalama
vimejiandaaje kuiona CCM inatoka madarakani. Wakiridhia hilo au kama
wakashindwa kulidhibiti Watanzania watarajie mabadiliko makubwa. Pili,
kukubalika kwa mgombea atakayepitishwa na CCM. Kama watapitisha mgombea
asiyeaminiwa na watia nia wengine waliobaki na asiyekuwa na uwezo wa
kuunganisha makundi  yaliyopo, tutegemee
viongozi hawa kuondoka na Lowassa. Hivyo hali ya CCM itazidi kuwa mbaya zaidi.

Hitimisho

Lowassa ni ‘jinamizi’ kwa wote wanaofikiria uchaguzi wa
2015. Jinamizi kama lilivyo katika hadithi za kale, linatisha. Inategemea tu,
Lowassa na timu yake wamejipanga vipi kwa ajili ya huo uchaguzi, na kama wana mpango
mbadala (plan) B, na C ili kuwaleta UKAWA na ACT kwenye mchezo. Lakini pia
inategemea hawa wahusika wengine kama vile CCM, UKAWA na ACT walivyojipanga kulidhibiti
au kulitumia jinamizi hili. Ni muhimu pia tukadhahania kuwa CCM inaweza
kupasuka mikononi mwa Kikwete.