Insha hii imetafsiriwa na Meg Arenberg kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili kwa kutumia tafsiri ya Lisa Hayden aliyetafsiri kutoka Kirusi cha maandishi asilia kwenda Kiingereza. Guzel Yakhina ni mwandishi mashuhuri kutoka Kazan, Urusi. Amewahi kushinda tuzo mbalimbali kwa maandishi yake na riwaya yake ya mwisho, Зулейха открывает глаза, imetafsiriwa na Lisa Hayden kwa Kiingereza kwa kichwa cha Zuleikha.

Ninaandika waraka huu kwa rafiki zangu, wachapishaji, wafasiri, na wasomaji katika nchi zingine. Kuandika kunahitaji uwazi wa fikra na akili tulivu kwa hiyo ni vigumu kuandika sasa, wakati hisia zinachemka. Kilicho vigumu zaidi lakini ni kuelewa yanayotokea Urusi na Ukraine. Ila kukaa kimya sasa hakukubaliki. Kwa hiyo nitajaribu angalau kuwaambia kitu.

Kwa miaka kumi na nne ya maisha yangu – utoto wangu kamili na ujana – niliishi katika uliokuwa Muungano wa Sovieti (USSR). Wakati huo itikadi ya kikomunisti ilikuwa tayari inavuta pumzi yake ya mwisho mwisho. Kama wanachama wa kikundi cha chipukizi, sisi watoto tuliamini itikadi hiyo, japo kwa shingo upande, si kwa makini. Tulichokiamini kwa dhati kilikuwa amani. Mashine ya propaganda iliyoanzishwa mwanzoni mwa zama za kisovieti ilikuwa inaendelea kufanya kazi kwa juhudi, lakini ilikuwa inatengeneza balagha ya upinzanivita zaidi kuliko balagha ya ukomunisti. “USSR ni ngome ya amani!” “Amani duniani!” Kaulimbiu hizo za kibalagha zilikuwa zimebandikwa ukutani kwenye kila chekechea na kila shule. Kila mwaka, masomo yalipoanza, kazi ya kwanza tuliyopewa katika kila darasa ilikuwa ni somo la amani. Nyimbo na mashairi kuhusu amani yalipewa nafasi katika kila tamasha la chipukizi (na tulikuwa na matamasha mengi). Njiwa weupe walichorwa kama ishara ya amani kwenye kila darasa, kwenye kila ubao, na kwenye kila daftari la mwanafunzi. Tuliamini njiwa weupe hao kwa dhati, jinsi watoto tu wanavyoweza. Imani ya amani ilikuwa sehemu ya utoto wa kisovieti isiyoondoleka. Tuliwekewa imani hiyo kwenye utambulisho wetu. Tukifikiri imani hiyo haitikisiki, kana kwamba ingedumu milele.

Nilielewa pia kuwa vita ni vya kutisha kiasi kwamba watu ambao wameshuhudia hujinyamazia. Babu yangu alikuwa mwanajeshi katika Vita vya Pili vya Dunia ila hakuwahi kutamka hata neno moja kuhusu vita hivyo: aliwalinda watoto na wajukuu wake kwa kukaa kimya.

Leo, vifaru vya Urusi vinakanyaga ardhi ya kigeni. Ni vigumu hata kuamini kinachotokea. Upinzani ndani ya nchi ni wa kina kiasi kwamba nataka kupiga mayowe. Maneno hayaji, hayana nguvu ya kutosha. Uchungu, hasira, hofu, udhaifu – vinafurika. Habari tulizopata tarehe 24 Februari 2022 ziliniponda. Dunia yangu haijapinduliwa tu, bali imeteketezwa. Sielewi kwa nini “chanjo” hiyo ya upinzanivita haikusaidia.

Ninaandika kwa niaba yangu mwenyewe, ila rafiki na wenzangu wote tuna mtazamo mmoja. Hakuna mtu hata mmoja katika jamii yangu ya karibu wala ya mbali ambaye anaunga mkono vita hivi. Mitandao ya kijamii imejaa hasira pamoja na maombi, malalamiko, na madai ya kukomesha shughuli hizi za kijeshi.

Wakati umewadia kuyasema maneno rahisi ya ukweli, na kuyarudia tena na tena. “Vita hapana!” “Amani duniani!” “Uhai wa binadamu una thamani kuliko yote!” Haya tutayarudia mpaka giza hili lipite. Tutathibitisha kawaida ya wema ili tusikumbane na kawaida ya uovu siku za usoni.

Hivi si vita vyangu. Nakataa kuvichukulia kama vyangu.