“Nchi yetu hii sisi ina uhuru. Sasa mbona ina uhuru wa watu wachache?”

—Dereva wa bodaboda, kata ya Manzese, Agosti 2022

Utangulizi 

Kuanzia tarehe 22 hadi 25 Agosti 2022, vikundi mbalimbali kutoka maeneo ya Manzese na Jangwani walikutana na watafiti wawili, Michaela Collord kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham (Uingereza) na Sabatho Nyamsenda kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Tanzania), kwa ajili ya kujadili changamoto wanazozipata katika kuishi na kufanya kazi maeneo hayo.

Walijadiliana na namna wanavyopambana kuziondoa changamoto hizo. Pia walitafakari, je, ni kitu gani kingepaswa kubadilishwa katika mfumo wa upatikanaji, upangaji na uendeshaji wa maeneo ya kufanyia kazi ili wavujajasho wote waweze kujenga mfumo upya, mfumo unaoleta haki sawa kwa wote kukaa hapo na kufaidika na maeneo kwa pamoja?

Miongoni mwa makundi yaliyowakilishwa ni pamoja na wamachinga, madereva wa bodaboda na bajaji, wabeba mizigo, wapepetaji nafaka, mafundi, waokota chupa za plastiki, mafundi magari kutoka gereji bubu, wang’arisha viatu, na wakazi wa eneo la Jangwani.

Ufuatao ni muhtasari wa mazungumzo hayo. Muhtasari huu unagusa mambo kadhaa muhimu. La kwanza, unasisitiza kuhusu thamani kubwa ya kazi za wavujajasho mtaani, kazi ambazo mara nyingi hudharauliwa. Kisha, muhtasari unataja changamoto zinazowakabili watu wa tabaka la chini, na maoni ya wavujajasho walioshiriki katika majadiliano yaliyozaa muhutasari huu. Maoni hayo yanahusisha malengo yanayoigusa serikali lakini pia mawazo kuhusu jinsi ya kujipanga wenyewe kama wavujajasho ili kuwa na mshikamano imara, kujijenga kiuchumi na kuwa na msimamo mmoja wakati wa kukutana na serikali, mabosi, au mamlaka nyingine.

Muhtasari huu ilijadiliwa na kukubaliwa wakati wa kongamano kubwa lililojumuisha vikundi vyote tarehe 3 Septemba 2022. Kuchapisha muhtasari huu hapa ni sehemu mojawapo ya kueneza mitazamo ya watu hao wanaoitwa “wa [tabaka la] chini” ambao ndiyo wengi. Yaani ni sehemu ya kukuza mazungunzo zaidi, na kutafuta njia ili wavujajasho wafaidike. Wote wawe huru, siyo tu “wachache.”

Wavujajasho, “thamani” ya utu na kazi zao 

Takribani washiriki wote wa majadiliano walisisitiza jinsi wanavyodharauliwa, kunyanyaswa, na kunyang’anywa bidhaa zao wakifanya kazi mtaani. Mwokotaji chupa ndiye mtuhumiwa wa kwanza iwapo wizi utatokea katika eneo analookota chupa. Machinga amefukuzwa mara mbili, tatu, nne mpaka mtaji wake wote umekatika. Pia mafundi wa gereji bubu, mafundi wa kung’arisha viatu, na wengine hufukuzwa kutoka barabarani. Dereva wa bodaboda, akipata ajali na kwenda hospitalini, hukutana na madaktari ambao hawamjali kwa sababu ya kazi yake. Wabeba mizigo wameonewa “kama takataka.” Kuna maneno mengi zaidi ya uonevu yanayotumika dhidi ya wavujajasho: “kundi la wahuni”, “chizi”, “uchafu”, “kidudu”, “wakorofi”… na mara nyingi tena, “wezi.”

Hata hivyo, washiriki wa majadiliano walipinga mitazamo hii ya “kibaguzi”.

Cha msingi kabisa, ni suala la utu kama alivyosisitiza dereva mmoja wa bodaboda: “Yule ni binadamu na mimi ni binadamu. Sasa kwa nini hatuna thamani?”

Cha pili, washiriki walisisitiza kwamba, tofauti na wanavyochukuliwa, wanaleta huduma na tija kubwa kutokana na kazi zao. Wanahudumia wenzao mitaani. “Tupo” pamoja, alisema fundi gereji, akiongeza, “Mama lishe tupo nao. Sisi ndiyo wateja wao.” Akaendelea kuwataja “machinga, bajaji, bodaboda.” Wote wanategemeana kazini na maishani.

“Sisi watu wa hali ya chini kabisa. Sisi pia ni sehemu ya wadau ambao tunalisha mkoa wa Dar es Salaam. Ukila ugali, ujue umetokana na sisi. Umetengeneza nyumba, ujue mwanangu pale kabeba simenti. Umepiga kinywaji, mwanangu kahusika. Sisi tunalisha mkoa wa Dar es Salaam. Basi… tuangaliwe, sisi kama maskini wa chini kabisa”

—Mbeba mizigo, kata ya Manzese, Agosti 2022

Lakini wavujajasho hawahudumii eneo lao tu, hapana. Watu wote wa Dar es Salaam, wakiwemo “watu wa tabaka la juu” wanawategemea wavujajasho. Kama ilivyonukuliwa hapo juu, wabeba mizigo wanaoshusha mahindi na wanawake wanaoyapepeta wanasema, “Tunalisha mkoa wa Dar es Salaam.” Machinga pia, wanahudumia mkoa huu, na kazi ya machinga ndiyo “biashara kubwa” hata kama “watu wanasema ndogo ndogo kutokana na jinsi tunavyotazamwa na jamii.” Wang’arisha viatu wanakaa barabarani “kusaidia raia”, yaani mng’arishaji mmoja ameshashugulikia viatu hata vya mbunge. Madereva wanasema, “sisi tunatoa huduma kama walivyo watu wengine”, na “Bodaboda ndo usafiri unaweza kukupeleka sehemu yoyote ambayo daladala haiingii.” Mwishoni, kote Dar es Salaam, waokotaji wanasafisha.

Licha ya kuleta huduma hizi kubwa, wavujajasho wanaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi. Sasa tuangalie, changamoto hizi ni zipi?

Changamoto

Kila aina ya kazi ina changamoto zake mahususi. Kwa mfano, madereva wa bodaboda na bajaji walitaja mfumo wa kinyonyaji wa mikataba na kupeleka hesabu kwa mabosi, waokotaji na wanunuzi walitaja bei za chini viwandani, na kadhalika.

Hata hivyo, changamoto nyingi zinawaathiri wavujajasho wote, hata kama zina sura tofauti kulingana na aina ya kazi. “Ya kwetu, tunafanana”, akasema fundi mmoja. “Hata mama lishe, akija hapa, atalalamika hilohilo na mimi nimeliongea.”

Ufuatao ni ufafanuzi wa changamoto walizozitaja washiriki, changamoto ambazo nyingi zinaingiliana:

Kutokuwa na eneo salama la kufanya kazi na kuishi
Watu wote walizungumza juu ya athari kubwa sana ya kukaa na kufanya kazi maeneo ya wazi yanayofaa kwa biashara zao, lakini serikali haitaki kuyatambua. Yaani wote—kutoka machinga mpaka mafundi gereji na wang’arisha viatu—hufukuzwa au hutishwa kwa sababu hiyo. “Itakuwa umemrahisishia Mtanzania kutafuta kipato chake kama asubuhi anajua anaenda wapi”, akasisitiza mshiriki mmoja. “Hii kuzurura kushoto, kulia inaleta shida sana.”

Kuna athari nyingine zaidi. Madereva hawawezi kusajili umoja wao na kupata mikopo kutoka manispaa kwa sababu stendi yao haitambuliki kwa serikali za mitaa. Hata machinga ambao walifanikiwa kujenga  SACCOS imara na yenye mtaji wa shilingi milioni 600 walipoteza mtaji huo baada ya kufukuzwa kutoka  kwenye soko lao.

Masuluhisho ambayo serikali inapendekeza pia ni changamoto yenyewe. Mipango ya kuwahamisha watu eneo lingine mara nyingi haijali mahitaji ya biashara za wavujajasho, ambazo zinategemea “mkusanyiko wa watu.” Biashara hizo, kwa msingi, ni biashara za mtaani, biashara za kuhudumia watu ambao wenyewe wako mtaani. Zinapoteza maana kama serikali ikizitoa. Wamachinga walitolea mfano wa “Machinga Complex”. Serikali ilijenga ila wateja hawaingii kule, na mwishoni  machinga “hawawezi kukaa” pia. “Utawalazimisha tu.”

Mbali ya kutegemea “mkusanyiko wa watu”, yaani wateja, biashara zenyewe zinategemea mchanganyiko wa biashara mbalimbali. Maana serikali kupanga  mafundi wote wakae eneo moja, machinga wote soko moja, n.k. kutakuwa changamoto pia. Kwa mfano, mafundi wa bodaboda wanasema wapo kila sehemu ili waweze kuhudumia kirahisi madereva ambao hawawezi kukaa sehemu moja.

Mwisho, watu ambao wamezoea kufanya kazi sehemu moja, kama wabeba mizigo ambao wanakaa Manzese na wamezoea Manzese, wana hofu ya kukosa kazi kama serikali itaamua kuwaondoa na kuwahamishia eneo jingine.

– Kutokuwa na kazi inayotambulika kwa serikali
Kutokuwa na eneo linalotambulika kunaendana na shida za kutokuwa na kazi inayotambulika. Washirikishi wa majadiliano wengi, siyo wamachinga tu, walisisitiza kwamba, “Kipindi cha vitambulisho [vya wamachinga], [wavujajasho] wengi walikuwa huru kidogo.” Sasa umebaki uhuru “mdogo sana” wa tabaka, yaani “nchi yetu ina huru lakini uhuru kwa wachache.” Kilio sasa ni, “tutambuliwe kama ajira rasmi.”

Kutokuwa na utawala shirikishi na wa kisheria
Wengi walilalamikia serikali kubadilisha misimamo yake kwa haraka mno bila kuwashirikisha wananchi, yaani “serikali imekuwa watu wa kuamua tu” na “wanadamu wanakuwa kama mifugo. Wanakuchukua na kusema, ‘Nenda huku! Nenda huku!” Wengine walisisitiza kwamba, “Malalamiko yetu yanaishia serikali za chini”, hasa kwenye wenyeviti wa serikali za mitaa. “Hayafiki juu.” Serikali na watu mtaani ni “sawasawa na mbingu na ardhi.”

Pia washiriki waliona kwamba serikali inakosa sheria na sera rasmi. Kwa mfano, mmachinga mmoja aliona kwamba vitambulisho vilikuwa kitu kizuri lakini mfumo wa vitambulisho haukuwa rasmi, kwani ulitokana na “tamko, siyo sheria.” Kuwa na sheria ni lazima ili wamachinga na wavujajasho wengine wabaki salama “hata kama anakuja kiongozi mwingine.” Lakini kwa sasa, “kila anayekuja, anakuja na utaratibu wake”, na mtaani wamachinga wanafukuzwa tena “kama kuku.”

“Kipindi cha vitambulisho, maana yake wengi walikua huru na biashara zao… Sasa uchumi unaonekana umekua mgumu zaidi kwa sababu mwingine leseni hana, kitambulisho hana, eneo pia hana. Anafanyaje biashara? [Ama] warudishe vitambulisho [vya] watu wa hali ya chini au wafanye maboresho ya mipango miji. Watuwekee maeneo ambayo kidogo yatakuwa rafiki na karibu na maeneo ambayo tulikuwepo sasa hivi, sio kutupeleka Chanika huko, Pugu, wapi. Inakuwa ni shida”

—Fundi wa bodaboda kutoka gereji bubu, kata ya Manzese, Agosti 2022

Vikosi vya usalama visivyowajibika
Wengi walilia askari barabarani, sungusungu, mgambo na vikosi vya usalama vingine kuwanyanyasa. Mara nyingi ni kwa sababu ya kutokuwa na eneo rasmi au kwa sababu kuna vigezo vya kufanya biashara ambavyo ni gharama kuvitimiza, yaani haviendani na uwezo wa kifedha wa wavujajasho wengi. Lakini pia, mara nyingine, askari na wengine wanatumia vibaya mamlaka yao ya kutoza faini ili kupata faida binafsi. Wengine wanavaa “kiraia” na hawana vitambulisho, maana alioshikwa nao hajui ni akina nani wanaomshika na atapelekwa wapi.

Kutokuwa na mikataba inayojali haki za wafanyakazi
Watu wengi, kwa mfano wabeba mizigo na wapepeta nafaka, hawana kabisa mikataba ya ajira hata kama wanafanya kazi kwa mabosi. Wako “kibaruani”. “Hujui ufanye nini mpaka upigiwe simu kwamba gari limekuja. Huko ndio ukimbie mbio uende kazini ufanye kazi.” Kipato pia ni “kidogo”, yaani “kinachopatikana kinaishia kwenye chakula,” na bila mikataba, “bosi anapanga bei yake.” Likizo ya ugonjwa, iwapo mtu ataugua, hakuna. Wakijisikia vibaya lazima waende kazini.

Wavujajasho wengine, kama madereva wa bodaboda na bajaji, wana mikataba, lakini wanasisitiza kwamba “ule mkataba ulivyoandikwa, unamlinda bosi. Wewe mfanya kazi haukulindi.” Kwa mfano, dereva wa bodaboda/bajaji anaweza kumlipa bosi hesabu ya kila wiki kwa mwaka mmoja na zaidi ili amiliki chombo chake mwenyewe. Ila dereva akikaribia mwisho wa marejesho hayo, bosi anaweza “kumpokonya”  chombo na kukiuza kwa mwingine “kwa ajili ya laki moja tu.” Labda dereva kaugua na akachelewa na hesabu zake za kila wiki. Na pia, dereva hawezi kumfanya bosi arudishe pesa zilizokwishalipwa. Dereva anazipoteza tu.[1] Hata kama mikataba hayo ingesaidia kumlinda dereva pia, madereva na wavujajasho wengine hawana uwezo wa kumlipa mwanasheria au kuenda mahakamani kutetea haki zao. Hatimaye, “Mimi kama nimekudhulumu [wewe kama bosi wangu], hutapata janga. Lakini kama umenidhulumu [mimi kama mwajiriwa], jasho langu Mungu ataliona.”

Mfumo wa mikopo na kuonewa kwa taasisi za kifedha
Kupata mikopo kutoka manispaa ni changamoto, hasa kama kikundi kinashindwa kujisajili au wahusika serikalini wanaomba rushwa. Mabenki yanakataa kukopesha, lakini taasisi nyingine zinazotoa mikopo midogo midogo zinaleta “mateso”, hasa kwa wanawake. Riba kubwa zitozwazo na taasisi hizo zinaleta “hali ya ufilisi mtaani.”

Matatizo ya kiafya yanayohusiana na kazi
Kazi nyingi zinaathiri afya za wavujajasho, yaani “kuna kuumia kwenye kazi.” Wabeba mizigo hulazimishwa kubeba mizigo mizito na hatimaye hupata matatizo ya mgongo, tena bila kulindwa kimkataba: “Mimi ukinipima nina kilo 70, nabeba mzigo [wa kilo] 130, natembea kama mtoto anaanza kutembea leo.” Wapepetaji wao huvuta vumbi la mahindi bila kuvaa barakoa, na hupata Kifua Kikuu (TB) na matatizo mengine ya kupumua. Madereva hupata ajali. Waokota chupa hupata maambukizi. Wakazi wa eneo la Jangwani, ambapo janga la mafuriko liliibuka baada ya ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi ya mwendokasi na wodi ya Taasisi ya Mifupa (MOI) hospitalini Muhimbili, pia wanapata magonjwa mengi, achilia mbali vifo na upotevu wa mali usababishwao na mafuriko.

Shida za kiafya pia ni shida za kifedha, na sababu moja muhimu ya vikundi vya wavujajasho kukosa kukuza mtaji wao. Vikundi hutunza akiba kwa ajili ya kuwekeza baadaye, ila mwishoni, badala ya kuwekeza, wanatumia fedha hizo kuwasaidia wanakikundi wenye matatizo pamoja na familia zao.

Miundombinu ya kujisitiri, kuhifadhi bidhaa, n.k.
Sehemu zinazotumiwa na wavujajasho kujipatia kipato au kuishi katika maeneo ya Manzese na Jangwani hazina vyoo, na miundombinu mingine muhimu, kama mahali pa kuhifadhi bidhaa.

Mfumo wa kusajili na kujenga vikundi kama umoja, ushirika, n.k.
Licha ya kuunda vikundi—umoja, chama cha ushirika, n.k.— kwa ajili ya kuleta faida ya pamoja kwao, wavujajasho wanakumbana na vikwazo vinavyowafanya washindwe kusajili vikundi vyao au hata wakisajili wasiweze kupiga hatua katika malengo waliyojiwekea. Mathalani, waraka huu umeshataja mfano wa madereva kutosajiliwa kwa sababu ya stendi yao kutotambulika kwa serikali za mitaa. Pia vyama viwili vya wanawake, SACCOS na chama cha ushirika katika kata ya Manzese, wamelazimishwa kulipa gharama kubwa, zinazojumuisha nauli za maafisa, tozo za ukaguzi na ada kubwa za mafunzo ambazo zinashusha mtaji wao. Wameona pia kwamba taasisi za serikali zinazoratibu ushirika zinaonekana kujali mashirika tajiri—kama SACCOS za wafanyakazi wa serikali na makampuni binafsi—kuliko mashirika ya watu wa chini ambayo yana mahitaji na uwezo wa kifedha tofauti.

Kusonga mbele

Changamoto zipo nyingi, lakini pia washiriki wa majadiliano walizungumzia namna bora ya kuzitatua. Kama mshiriki mmoja alivyosema, “Watu wa [tabaka la] chini wana ideas kuliko watu wa juu.” “Maamuzi yanatakiwa yatoke kwa wananchi”, akaongeza mwingine. “Tuna mawazo makubwa.”

Hapa chini ni baadhi ya mawazo hayo.

Kuwa na mfumo shirikishi wa mipango miji unaojali mahitaji ya wafanyakazi na wakazi

Wengi waliongea kuhusu nini wangependa serikali iweke kwenye mipango miji yake, kwa mfano:

  1. Madereva walizungumza juu ya kujenga njia maalum za pikipiki na bajaji kando ya barabara kuu kama barabara za Morogoro au Bagamoyo kwa sababu ya wingi wa ajali za kutisha kwenye barabara hizi.[2]
  2. Wang’arisha viatu walitaka njia maalum kwa watembea kwa miguu.

Kila kundi lilikuwa na mapendekezo yake, lakini pia walizungumza namna ya kuboresha mfumo wa mipango miji kwa ujumla. Kwa mfano, licha ya kupanga ili mafundi wote au machinga wote wahamishwe sehemu moja ya mbali kufanya kazi zao, afadhali serikali ihushishe watu wa kila eneo—kama eneo la Manzese na eneo la Jangwani—ili waweze kupanga pamoja—mtaa kwa mtaa—jinsi bora ya kukidhi mahitaji ya watu wanaofanya kazi na wanaoishi huko.[3] “Kwa kushirikiana wenyewe, tunaelekezana,” alisema mshiriki mmoja. Inatakiwa watawala serikalini “waongee na wafanyabiashara wote… wakutane na mafundi wote wa gereji, halafu tarehe nyingine, mama lishe wote. Wakusanye maoni kila sehemu, halafu ndiyo wajue wafanyeje… Wakifuata maoni yenu, watapata faida.” Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba changamoto kubwa ya wavujajasho kutokuwa na eneo linalofaa kwa kazi zao itatuliwe.

Kuwa na sheria na sera rasmi zinazohusisha wavujajasho moja kwa moja
Badala ya serikali kuwa na “tamko” au misimamo inayobadilika kwa haraka, bora ipitishe sheria, kama “Sheria ya Machinga” inayolinda haki ya wavujajasho na pia kuboresha mipango miji.[4] Siyo kubaki na hali ya “tunaondolewa, tunarudi.” 

Uwajibikaji wa vikosi vya usalama
Lazima kuwe na mfumo imara zaidi wa kuwatambulisha na kuwajibisha vikosi vyote vya usalama, vikiwemo askari, sungusungu, n.k. Kwa mfano, lazima askari awe na kitambulisho chake kumwonesha mtu kama anatoza faini.

Mikataba na sheria zinazolinda haki za wafanyakazi
Wafanyakazi wote wawe na mkataba unaolinda haki zao, na siyo kufanya kazi kwa uamuzi wa bosi wao. Wizara ya Kazi inapaswa kuimarisha mfumo wa kulinda haki za wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kusaidia kutekeleza mikataba yao na kuhakikisha waajiri wanatimiza wajibu wao wa kimkataba kwa wafanyakazi.

Bima ya afya
Serikali ihakikishe wafanyakazi wanapata bima ili kulinda afya zao lakini pia kuwakomboa na gharama za matibabu, jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yao. 

Kujenga miundombinu
Serikali inapaswa kujenga miundombinu muhimu, hasa vyoo vya umma, katika maeneo yote.

Mageuzi ya mfumo wa kusimamia vyama vya ushirika
Serikali kwa ujumla na hasa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania inapaswa kufanya mageuzi ili kukidhi mahitaji ya vyama vya ushirika vya wavujajasho, ikiwemo kuangalia ulipaji wa ada, ruzuku, na tozo zingine zinazoleta changamoto kwao.

Mshikamano na umoja wa wavujasho 

Washiriki wa majadiliano walitoa mapendekezo yao na dhamira yao. Lakini pia walijadili namna ya kujijenga wenyewe, kuwa na mshikamano na umoja imara zaidi ambao utasaidia kutimiza ndoto hizo.

Wengi walikuwa wanaongea kuhusu mshikamano ambao tayari upo. Waokota chupa hawana vikundi ila wanachangia mtu akipata tatizo, hata kama siyo mwokotaji mwenzao. Kwa mfano, wameshachangia kusaidia kulipa matibabu ya dereva wa bodaboda aliyepata ajali. Wakazi wa Jangwani pia wanasaidiana. Wote wamepata matatizo na wanaishi kwa “upendo” walionao kwa wakazi wengine. Kama ambavyo imeshatajwa hapo juu, kutegemeana pia kunakuza mshikamano. Mafundi gereji wanasema “tupo” na mama lishe, machinga, bajaji, bodaboda.

Mbali ya mshikamano wa kusaidiana kwenye maisha ya kila siku, kuna uwezekano wa kuanzisha vikundi vya wafanyakazi.

Kuna changamoto nyingi zinazoukumba mchakato huu pia. Washiriki kadhaa waliona kwamba “kupata muda tu wa kujipanga kuwa na umoja [ni] changamoto.” Wengine walisema kwamba, kutokana na vipato vyao vya chini, watu “wanaogopa” kuchangia, au viongozi ni “wanafiki.” Walikuwepo washiriki ambao wameshajaribu kuanzisha vikundi vyao ila serikali ikaweka vikwazo vingi na vikashindwa kujisajili, kama ilivyotajwa hapo juu. Mwisho, washiriki wengine walikuwa na vikundi imara, lakini kutokuwa na eneo rasmi na kubomolewa na serikali kuliwasabibishia hasara kubwa. Mwakilishi kutoka mojawapo ya SACCOS za wamachinga katika kata ya Manzese anakumbuka kwamba:

“Pale miaka ya nyuma, hapo kabla hatujavunjiwa, tulikuwa na huduma hata za tigo pesa. Tulikua na huduma kama za kibenki. Unaweka hela yako kama benki… Tulikuwa na huduma nyingi nyingi. Sema basi, kuvunjiwa vunjiwa ikatokea ghafla. Watu wengi wamekimbia na mabegi. [Awali] SACCOS ilikuwa na mtaji wa karibu na milioni mia sita pale… Tulikuwa Tunakopesha mpaka milioni arobaini, milioni sitini, milioni mia. Sasa hivi [baada ya kuvunjiwa], tumeporomoka. Tuna mtaji wa milioni kumi, kumi na tano.”

Hata kama vinakabiliwa na changamoto nyingi, vipo vikundi vya wavujajasho vinavyoendelea kupambana, ikiwemo SACCOS hiyo ya wamachinga. Vyote bado viko njiani, ila vina uzoefu mkubwa, na wanaweza kusaidia kuelimisha na kuhamasisha wavujajasho wenzao.

Kwa mfano, kuna kikundi cha wabeba mizigo. Kilianzishwa mwaka 2006 na kwa sasa kina wanachama 49. “Wachache wataelewa mwanzoni,” alishauri mwanakikundi mmoja, akiongeza, “wengine watakuja baadaye”. “Kuanzisha kikundi ni rahisi, lakini pia vigumu. Watu hawana uelewa wa kuanzisha katiba, mfuko….” Kikundi hicho kilivuka hatua hizo za awali. Sasa kina mifuko mbalimbali ikiwemo mfuko wa wanachama kwa ajili ya maendeleo na mfuko wa kusaidiana kama mtu ana tatizo fulani. Pia kikundi kinasaidia kama kuna sintofahamu baina ya makuli na mabosi yao, “kama [bosi] anatubana, tunafanya kazi ya elfu 10 na anatulipa elfu 2.” Ni kweli kwamba bado wanakikundi hawajatimiza malengo mengi hasa kiuchumi. Yaani ni “kikundi kikongwe kidogo, lakini kichanga kimaendeleo.” Wanatamani kuwekeza kwa pamoja, kununua vifaa vya kikundi, na hivyo kufanya biashara kwa pamoja, “lakini hatujapata nafasi.” Hata hivyo, wamesonga mbele, na wana ufahamu mkubwa wanoweza kuleta kuwasaidia makuli au wavujajasho wengine ambao wanaanzisha vikundi vyao.

Vikundi vingine vimeshapata nafasi kuwekeza kwa pamoja, kwa mfano, Umoja wa Wanawake wa Manzese. Kama walivyotuelezea, walianza kama umoja wa vikundi vya akiba na mikopo (VICOBA) vya wanawake, na sasa wamejisajili rasmi kama chama cha ushirika. Walianza umoja wao kuepuka taasisi za fedha ambazo zilikuwa zinawatoza riba kubwa kuchukua mali zao. Sasa wamefika mbali zaidi. Wana biashara kadhaa, kama baa, biashara ya kutengeneza sabuni, na biashara ya upishi.

Kikundi kingine cha wanawake wana SACCOS yao, na wanasaidia wanakikundi na mikopo na misaada mbalimbali. Vikundi vyote viwili vimekutana na changamoto vikifanya kazi na taasisi za ushirika, changamoto zinazotajwa hapa juu. Lakini wanakikundi wao walianza kuongea kuhusu uwezo wao wa “kujipanga vizuri kama watu mtaani” na  kuungana pamoja kama “vyama vya ushiriki kata ya Manzese” ili kusaidiana na kuanza kubadilisha mfumo wa ushirika huo ambao siyo rafiki kwao.

Vikundi hivi vyote vinatarajia kujiendeleza na kujiimarisha zaidi. Wana mengi ya kujifunza kutoka kwa kila mmoja wao, na pia kubadilishana uzoefu na wavujajasho ambao bado hawajajiunga katika umoja. Miongoni mwao, waokota chupa waliongea kuhusu namna umoja unavyoweza kusaidia kuongeza malipo kutoka viwandani. Wang’arisha viatu waliona kwamba, “bila kikundi, hakuna mtaji”, na pia umoja “siyo mafundi tu” ila umoja huu unaweza kuunganisha wafanyakazi wa aina mbalimbali kutoka kata ya Manzese na maeneo mengine.

Hitimisho

Hayo ndiyo “mawazo makubwa”, na makubwa kabisa ukilinganisha na mitazamo ya wanaowaona wavujajasho kama “wezi”, “takataka”, au wasio na “thamani.”  Washiriki wa majadiliano walitoa maoni na maono yao kuhusu mipango miji shirikishi inayotakiwa, mipango yao ya kujiimarisha wenyewe, na kwa ujumla, matumaini yao ya mustakabali mbadala.

Hayo yalikuwa majadiliano tu, na hayaishi hapa. Mapambano ya wavujajasho yanaendelea.

***

[1] Ukipitia mikataba ya madereva, unaona kwamba kuna vifungu vinavyofafanua ni kiasi gani dereva anamlipa bosi na kwa muda gani kabla ya kukimiliki chombo mwenyewe, lakini hakuna chochote kuhusu wajibu wa bosi kwa dereva ikiwa dereva atashindwa kukamilisha kiasi kamili kwa wakati, hata kama tayari ameshalipa sehemu kubwa. Kweli, kimkataba bosi anaweza “kupokonya” chombo tu.

[2] Njia maalum za pikipiki na bajaji zipo miji mingine, kama Cotonou, nchini Benin. 

[3] Mfumo wa aina hii ulikuwepo Durban, Afrika Kusini, na bado upo miji mingine, kama kule Brazil. 

[4] Baada ya kampeni iliyoendeshwa na wamachinga wenyewe, serikali ya India ilipitisha, cha kwanza, Sera rasmi ya machinga (2004) na baadaye Sheria ya Machinga (2014).

Muktadha/Usuli

Michaela aliandika makala haya, lakini yanatokana na mradi wa pamoja wa utafiti na mijadala inayoendelea na Sabatho Nyamsenda. Tina Mfanga naye alitoa msaada muhimu sana. Kujitolea kwake kwa muda mrefu katika uanaharakati na kujipanga huko Manzese na Jangwani kunamaanisha kuwa ana uhusiano mkubwa katika maeneo hayo. Hivyo, aliweza kuyakutanisha makundi mbalimbali yaliyoshiriki majadiliano ambayo makala haya yanayanukuu.