Watanzania ni “watu rahimu sana.” Hiyo ni sifa tuliyomiminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Ilikuwa katika mkutano wake wa kwanza na wahariri wa vyombo vya habari toka aupate Urais.

Nami sina budi kumsifia Rais wetu kuwa ni mtu rahimu sana maana naye ni Mtanzania. Kwa kuwa neno hilo limezua mjadala kuhusu maana yake, hebu basi tulidadavue. Tulio na watu wa karibu wenye majina ya Rahim na Rehema hatukupata shida kulielewa. Alipoulizwa maana yake kwenye mtandao wa kijamii, mwanahabari mmoja nguli alijibu: “Unaweza kusema mwema….”

Hivyo, pamoja na mapungufu yetu ya hapa na pale, kwa ujumla sisi ni watu wema na Rais wetu ni mwema. Lakini, kama ambavyo wadadisi tumekuwa tukisisitiza, awamu baada ya awamu ya Urais, hatuwezi kutegemea wema tu wa watu kwenye masuala ya uhuru na haki za binadamu. Kwenye haki na uhuru wa kutoa na kupata habari au taarifa ama maoni, wema siyo kipimo.

Wema siyo mizani. Uwepo usiwepo haki na uhuru vinapaswa kuwepo. Kipimo ni sheria mama.

Katiba ndiyo kipimo. Na, kama tulivyoona kwenye makala ya Uhuru Uendelee, haki hizo za msingi zimesimikwa kwenye Katiba hii hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 toleo la mwisho la mwaka 2005 yalipofanyika mabadiliko madogo ya 14 ya kikatiba. Hili siyo tena suala la kutegemea urahimu wa Rais aapaye kuilinda Katiba ikiwemo hii Ibara yake:

Ibara ya 18 ya Katiba inafutwa na kuandikwa upya kama ifuatavyo: Kila mtu: (a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; (b) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; (c) anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake; na (d) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.

Ndiyo maana wafuasi wa dhana ya Usonga, yaani Uafrika Songambele, tulipigwa na butwaa tulipomsikia jana Rais Samia akituambia, kupitia kwa wahariri wa vyombo vya habari, kuwa:

Lakini ukiacha sheria za nchi, kuna ile tu heshima na adabu ya Kiafrika ndugu zangu….

Wasonga tunajiuliza, kama tulivyojiuliza kwenye hoja za mavazi alipotolewa Bungeni mbunge mwanamke hivi karibuni, hizo “heshima na adabu za Kiafrika” zinapimwaje? Kwa urahimu wa Rais wetu? Wa Waziri wake mwenye dhamana ya sekta za habari na utamaduni? Au wa nani?

Ni kwa nini tunadadisi hayo? Kwa kuwa hakuna kipimo cha kikatiba! Labda ndiyo maana Rais alisema, “lakini ukiacha sheria za nchi…” baada ya kusema, “sheria za nchi lazima zifuatwe….”

Kama kweli tunataka kutooneana katika haya masuala, ni heri basi tuwe na mjadala na maamuzi ya kitaifa kuhusu maana hasa ya heshima na adabu ya Kiafrika. La sivyo, tafsiri itategemea Rais au Waziri ama Mkurugenzi anayehusika na masuala hayo kaamkaje. Kirahimu rahimu au kishari.

Ladha tamu ya majibu mengi rahimu ya Rais jana ilitiwa shubiri na kauli hiyo pamoja na ile ya andiko tata kuhusu virusi vya korona kooni na kujifukiza. Ni sawa na kulishwa lawalawa tamu ajabu na mama kisha mwishoni kupewa majani machungu ya mchunga. Wengine tumejikuta ikitukumbusha mkutano kama huo aliuofanya mtangulizi wake, Hayati Rais John Magufuli.

Baada ya mkutano huo uliofanyika mwezi Desemba mwaka 2015, nilijikuta nikiandika makala yenye kichwa hiki cha habari: Majibu ya Magufuli na Kazi ya Kikatiba ya Wanahabari. Kama ilivyo sasa, kilikuwa kipindi cha fungate la Urais, hivyo, ilikuwa vigumu kuandika kitu chochote cha kuhoji kikasikika. Zilikuwa zama za upofu wa matumaini. Katika hitimisho, niliandika haya:

Wahenga walinena kuwa ‘nyota njema huonekana asubuhi’ na ‘dalili ya mvua ni mawingu’. Kipindi hicho kifupi cha maswali na majibu kati ya Wanahabari na Rais kinaweza kutupa mwelekeo wa huko tuendako. Japo madai ya Katiba mpya yanazidi kusahaulika katika kipindi hiki cha mwamko wa ‘Magufulika’, tukumbuke kuwa hata hii Katiba ya Mwaka 1977 tuliyonayo inasisitiza kwamba:

“Kila mtu… anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii” – Ibara ya 18 (d)

Lakini pia Ibara ya 18 (b) ya Katiba hiyo tuirekebishayo inasema:

“Kila mtu… anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi”

Kupewa taarifa ni haki. Na kutoa habari ni kazi. Hapa hakikazi tu.

HakiKazi iendelee.

Hatimiliki

Udadisi imetumia vibonzo kwa idhini ya mchora katuni Masoud Kipanya.