Ufafanuzi
Hili andiko ni sehemu ndogo tu ya mchango wangu kwenye mjadala mpana kuhusu ndoa za mitala. Mchango huu umejikita katika dhulma kwa kuwa kuna michango mingine mingi inayoongelea kwa kina upande mwingine. Kwa hiyo ndugu yangu msomaji, kabla hujaja na hoja za faida, uwe tu na amani kuwa hoja hizo zitazungumzwa kwa kina kwenye kongamano pendwa la mitala linaloendelea huko nchini Kenya.

Baada ya ufafanuzi huo, nianze kwa kukiri kuwa mila na tamaduni za kuoa wake wengi zilikuwepo kwa mujibu wa historia na zinaendelea kuwepo kwenye jamii zetu. Japokuwa kwa sasa ndoa hizi zinahusishwa zaidi na mafundisho ya dini ya Kiislam, ila bado zipo jamii kama zile za kusini mwa bara la Afrika ambazo zina tamaduni za ndoa za mitala hasa kwa viongozi wao licha ya kuwa wao siyo Waislam. Hata hivyo, andiko hili litajikita kwenye dhulma kwenye jamii za Waislam.

Kwa mujibu wa Uislam, ruksa ya kuoa wake wengi imetoka kwenye kitabu kitukufu, nanukuu:

Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana (Quran 4:3)

Aya hii inaonyesha dhahiri kuwa ruhusa hii ya kuoa mke zaidi ya mmoja imekuja na masharti yake hasa katika kuhakikisha kila mke anapata haki zake kikamilifu. Kwa maneno rahisi, aya hii imesema, ruksa ya kuoa mke zaidi ya mmoja ni kwa wale tu ambao wanaweza kuwa waadilifu kwa wake zao wote. Kama wewe unajua uwezo na dhamira ya kuwa muadilifu huna basi unapaswa kuoa na kubaki na mke mmoja tu.

Katika muktadha huu, kumekuwa na mijadala endelevu miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu juu ya ‘uadilifu ni nini? Japo kuwa maoni yanaendelea kutofautiana, wengi wanakubaliana kwenye yafuatayo:

  • Kutenda kwa usawa: Mume mwenye mke zaidi ya mmoja lazima ahakikishe uwepo wa usawa miongoni mwa wake zake. Usawa huu ni pamoja na kutimiza mahitaji yao ya kihisia-moyo, kimwili na kijamii kwa usawa. Isiwe huyu ni mke wa siku tano na yule wa siku mbili, huyu mke wa hadharani na mwingine wa mafichoni. Huo sio uadilifu.

  • Wajibu sawa wa kifedha: Mume mwenye mke zaidi ya mmoja ana wajibu wa kuwahudumia na kuwatunza kwa usawa wake zake na watoto wote kwenye ndoa zake. Hii ni pamoja na kuhakikisha wake na familia zote wanapata haki sawa ya makazi, mavazi, chakula, matibabu, na mahitaji mengine. Kutunza familia moja na kuacha nyingine si uadilifu.

Kwa tafsiri hii ya uadilifu matarajio ni kuwa, uwezo wa kutimiza vigezo hivyo ndivyo vilipaswa kuwapa haki ya kuwa na mke zaidi ya mmoja. Ila kwenye dunia ya leo, wanaume wengi wamekuwa mstari wa mbele kuoa mke zaidi ya mmoja, kwa sababu ni ‘haki yao’ kidini, bila wao kufuata na kutimiza ‘masharti’ (wajibu) kwa mujibu wa dini. Je, kuna haki bila wajibu?  Matokeo yake, ndoa nyingi za mitala zimegubikwa na dhulma nyingi na kuwa chanzo cha kuvuna/kufanya dhambi na mifarakano kwenye jamii hivyo kwenda kinyume na matarajio ya ndoa kwa mujibu wa dini.

Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri (Quran 30:21)

Dhulma ya Kifedha
Japokuwa kwa mujibu wa dini ya Kiislam uwezo wa mwanamke kifedha ni moja ya sifa za kuolewa, na hivyo wanaume wameshauriwa kuoa wake ‘kwa mali zao’ (wadada endeleeni kutafuta hela), siku hizi imekuwa kama ni ‘fashion’ kwa wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja, huku wakijua kwa hakika kwamba hawana uwezo wa kutimiza wajibu wao wa kuwatunza na kuwahudumia. Dhulma zaidi ni pale anapooa mwanamke mwenye kipato a.k.a ‘career woman’ kwa kujua kuwa hatahitajika kutoa huduma yoyote ya kifedha kwake na hivyo kipato chake yeye mume kutumika tu kwa mke mmoja. Hii si sifa ya uadilifu na ni dhulma.

Kuna simulizi nyingi za wanawake kuolewa mke wa pili na mume kugoma kujigusa kwa chochote, tena wewe mke mdogo ndiyo unatakiwa utumie pesa zako kumuenzi mume asikukimbie. Pale ambapo mke anayejitunza akiendelea kudai haki yake ya kutunzwa na kuhudumiwa, basi zogo hutokea na mara nyingine ndoa huvunjika. Watoto wanaozaliwa kwenye ndoa hizi hujikuta kwenye mtihani mkubwa hasa pale ambapo ndoa ya wazazi wao inapovunjika kwa sababu ya mume kutotimiza wajibu wake kifedha. Watoto huishiwa kulelewa na mama tu.

Ukiachia hao wanaooa wake wenye vipato, simulizi nyingi huku mtaani zinaonyesha kwa wanaume wengi uwajibikaji wa kifedha umekuwa kama zawadi kwa mke anayempenda zaidi. Hawalichukulii kama jukumu lao. Hawaoni kuwa wanawajibika kutekeleza usawa kwa wake wote kwa misingi ya dini.

Dhulma ya Hisia
Umma wa Waislamu wa leo wamebuni ‘ndoa ya siri’ ambapo mke mpya analazimika kufichwa ili mke aliyetangulia na pengine hata ndugu, jamaa na marafiki wasijue kuwa mume ameoa mke mwingine. Ili kutimiza lengo hili la usiri, mke mpya huporwa haki zake nyingi ili mume aweze kuendeleza ‘ratiba’ ya maisha yake na asigundulike kama ameoa. Mara nyingi hii hupelekea mume kuwa na mke mpya kwa muda mchache mchana tu ‘anapokuwa kazini’ au pale anapoweza kutengeneza ‘safari feki’. Hufika mahala mke wa hata achikwe na chango usiku hawezi kupiga simu kwa mumewe au suala la kuambatana na mume wake kwenye mijumuiko ya kijamii kama harusi au misiba linakuwa halipo.

Kimsingi, ndoa hizi za siri zinaendeshwa kama tu uhawara, ila kuna ‘ubani’ umepita kutengeza ‘halal girlfriend’. Uhalali wa hizi ndoa zinazopewa baraka na mashekh wetu, Mungu tu mwenyewe ndiyo anajua, ila ni dhahiri ndoa za siri zinavunja na kuondoa uwezekano wote wa mume kuwa ‘muadifu’. Maisha ya wanawake wengi katika ndoa za siri yamegubikwa na unyanyasaji mkubwa mno wa kihisia. Kuishi maisha ya kufichwa kama fuko la bangi kunaleta msongo, kujiona huna thamani na mengineyo.

Wapo wanaume wanaolalamika kuwa, ohh, mwanzo alikubali nimuoe ndoa ya siri ila siku hizi ameanza kunipiga pressure ndoa iwekwe wazi. Fukuto la nafsi ya ndoa hizi halihimiliki, it’s just a matter of time. Mbaya zaidi, baadhi ya wanaume katika ndoa hizi wameenda mbali zaidi hata kufikia kuficha watoto waliozaliwa katika ndoa za siri. Watoto wananyimwa haki zao za kulelewa na wazazi wote wawili, kikamilifu na kwa uwazi. Wengine hukosa hata haki ya kuwajua ndugu zao, au huishia kujuana siku baba akifariki, akisindikizwa na zogo na kashfa.

Dhulma ya Wajibu wa Ndoa
Kupuuza na kutotimiza mahitaji ya kimwili na kihisia ya mke yeyote inachukuliwa kuwa ni dhulma katika dini. Wake wote wanastahiki haki hizi ndani ya ndoa. Ingawa mume anaweza kuwa na wake kadhaa wa kushiriki nao katika wajibu wa ndoa, mara nyingi wao husahau kwamba wake zao wana mume mmoja tu.

Hii ina maana kuwa wakati mume anaweza kupata 25% kutoka kwa kila mke na akatimiza kwa 100% ya mahitaji yake, lazima yeye afikishe 100% ya mahitaji ya kimwili, kihisia, au kifedha kwa kila mke wake. Hapa naomba nisisitize dhana ya ‘mahitaji ya mke’, huwezi kusema, ili nifanye usawa nitakuwa natimiza wajibu wangu wa ndoa kwa kila mke wangu mara moja kwa mwezi.

Je, mara moja kwa mwezi ndio mahitaji yao? Au unawafanyia tu dhulma? Na wasipopata hiyo huduma kwako waende wapi?

Dhulma ya Mahaba
Kupendwa na kuonyeshwa mapenzi ni haki ya mke. Kwa mujibu wa dini, ‘mbora miongoni mwenu ni yule aliye mbora kwa mke wake’  Bahati mbaya ndoa nyingi zimekuwa ndoa za mazoea na wake kukosa haki za kupewa na kuonyeshwa mahaba.

Wanaume wengi huamini wao ndio wana haki ya kuonyeshwa mahaba na wake zao na sio vinginevyo. Na mara nyingi mahaba hayo machache waliyonayo kama kuwa na muda mzuri na mke wake, kumuongelesha kauli nzuri, kumdekeza, kumsikiliza, kumpa vijizawadi, kumsifia n.k., huhamishiwa yote kwa mke mpya pale anapoolewa. Hii dhulma ya mahaba imekuwa chanzo kikuu cha hisia za chuki, wivu na mifarakano baina ya wake.

Jamii ni kama imeshazoea kuwa wake wenza lazima wagombane na kufarakana. Lakini jamii hii hii haitaki kukubali kuwa chanzo ni nini. Ni mume kujipa haki ya kuoa wake wengi bila kuwa na uwezo, dhamira na mipango ya kuwatendea uadilifu wake zake.

Dhulma ya Uchamungu
Japokuwa Uchamungu wa mtu unatakiwa ujengwe na imani yake kwenye maandiko na Muumba wake, ukweli ni kwamba matendo ya walio karibu yetu hujenga au hufifisha imani zetu. Kukosekana kwa uadilifu wa wanaume kwenye ndoa nyingi kumesababisha dhulma kama nilivyogusia hapo juu. Kitu ambacho waume wengi hawajui au hawataki kukubali ni kuwa dhulma hizi zinateteresha sana imani na Uchamungu wa wake zao. Huku mtaani unaambiwa ukitaka kukufuru, kufanya shirki na fitna omba mumeo aongeze mke, hakuna dhambi hautafanya. Dhulma zimezidi kiasi kwamba wanawake wengi wanaona Muumba wao anawaonea kuwaruhusu wanaume waoe mke zaidi ya mmoja, kwa wale ambao bado imani zipo basi hukesha kwenye miswala kuiomba subra. Imefika mahala, wema, busara na hekma za ndoa hizi haonekani tena, bali wake wanaona wameshushiwa jehanamu hapa hapa duniani.

Dhulma hizi za kwenye mitala hazifanywi tu na mume kwenda kwa mke, bali pale mume anapokosa uadilifu na kushindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu, husababisha aidha mke au ndugu kupora haki za mke mwingine. Kwa mfano, mke mwenye ushawishi aidha kwa ukubwa wake au upya wake, huweza kuweka vigingi vya nini kifanyike au kisifanyike kwa mke mwenzio. Anaweza kuyazua yaliyokuwepo na yasiyokuwepo ili mwenzie adhulumike n.k. Tumefika mahala wake wanajiapiza kuwa ‘nitamtoa yule’ unabaki kushangaa kuwa wajibu wa mume hapa uko wapi?

Ndugu hasa wa mume huwa pia na kikawaida cha kuchagua upande. Hufanya hivyo hasa pale ambapo mgawanyiko umeshatokea kwa kukosekana uadilifu. Kutengwa, kuchukiwa na kusemwa humfanya mke kukosa furaha kwenye ndoa na maisha yake.

Hitimisho
Nihitimishe kwa kusema, ingawa ndoa za mitala zinaruhusiwa katika dini, ni muhimu kujua kuwa hazijalazimishwa, na waislamu wengi huchagua ndoa za mke mmoja kujipunguzia dhima ya kudhulumu haki za mke na watoto. Uamuzi wa kuwa na wake wengi unapaswa kufanywa kwa uangalifu na wajibu mkubwa, kwa kuzingatia ustawi na haki kwa pande zote zinazohusika. Kama ndoa hizi zinafanywa na mujibu wa imani ya dini basi zitekelezwa kwa mujibu wa imani ya dini pia, na sio kutumia dini kwenye kuoa tu, ila kuishi ni kimjini mjini. Wengi wanao oa ndoa hizi husema hufanya hivyo kwa kujiepusha na dhambi ya zinaa, ni vizuri pia kuzijua na kuziepuka dhambi utakazozipata kwa kukiuka wajibu mkuu wa kuwa muadifu. Kuepuka dhambi moja kusikutengenezee dhambi elfu moja. La muhimu zaidi, ni kukumbuka kuwa ‘mbora miongoni mwenu, ni yule aliye mbora kwa wake zake’ watendeeni mema wake zenu.