Natoa pongezi nyingi kwa wote wanaohusika na hii Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika, ambayo sasa inajulikana dunia nzima. Pia nawapongeza wote walioshinda na ambao hawakushinda mwaka huu. Kwani kutoshinda hakuna maana kuwa maandishi yao si mazuri.  Nyote mnachangia katika ukuzaji wa lugha hii tukufu, na ambayo asili yake ni Afrika. Kiswahili kimeteuliwa kiwe lugha ya Afrika nzima. Mimi mwenyewe napendekeza kiwe lugha ya dunia.

Nataka kukumbusha machache kuhusu umuhimu wa lugha. Katika mwaka wa elfu moja mia nane na thelathini na nne (1834), Mwingereza mmoja aliyeitwa Lord Macauley alipendekeza sera mpya ya elimu India, nchi ambayo ilitawaliwa na Uingereza kwa miaka mingi. Alisema kwamba lazima Kiingereza kiwe lugha ya elimu, badala za lugha za wenyeji, kama vile Sanskrit. Nia ya kufanya hivyo, alisema, ni kuunda tabaka kutoka kwa watawaliwa, ambalo, kwa miili yao, rangi za ngozi zao, mavazi, dini, zitabaki kuwa za Wahindi kabisa, lakini vichwa vyao, yaani mabongo yao, yatakuwa ya Mwingereza. Akaendelea kusema, tabaka hili la mwili wa Mhindi lakini bongo la Mwingereza, litasaidia kufaulisha utawala wa kikoloni India. Yaani tabaka hili litakuwa kama manyapara wa ubeberu.

Kote walikotawala duniani, Waingereza walifanya kama hivyo: walikandamiza lugha za wenyeji, na kukuza Kiingereza juu ya makaburi ya lugha za wenyeji. Wainagereza, Wafaransa na wakoloni wengine hawakutoa sera hizi kwa nia tu ya kujifurahisha.  Kiingereza na Kifaransa ni lugha za biashara ya mamilioni ya dola.

Kwa hivyo, tusifikiri kwamba Waingereza na Wafaransa watakaa kimya wakiona Kiswahili kinaweza kuwa lugha ya Afrika nzima. Watafanya kila wanaloweza kuona kwamba Kiswahili hakitachukua nafasi za lugha hizo kwa elimu ya Mwafrika. Watatumia mbinu nyingi: za pesa, au za kidiplomasia kuangamiza mpango huo. Watajaribu kuwashawishi viongozi wa sera za elimu za nchi zetu kwamba elimu ya dunia, elimu ya sayansi, elimu ya juu, inawezekana tu kwa Kiingereza. Watazishawishi serikali za Afrika kwamba ujuzi wa sayansi na teknolojia wawezekana tu kwa Kiingereza. Nataka kukumbusha kwamba wakati Kiingereza na lugha nyengine za Ulaya zilikuwa zinanyanyaswa na Kilatini, waliopendekeza kutumia Kiingereza kwa elimu na uandishi waliambiwa Kiingereza hakina majina ya dawa na sayansi, ati elimu nzuri ni ile inayosomeshwa kwa Kilatini tu.

Ni wajibu wetu sisi Waafrika kukikuza Kiswahili na lugha nyengine za Mwafrika. Tuzo hii ni mfano mmojawapo wa yale yanayowezekana kufanywa. Lakini serikali zote za bara la Afrika zinahitajiwa ziwe na sera za kukuza Kiswahili kiwe lugha ya Afrika nzima. Ahsanteni sana.

HAKIMILIKI

Ujumbe wa Ngũgĩ wa Thiong’o kwenye sherehe ya Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika, iliyofanyika Mlimani City Conference Centre, Dar es Salaam, Januari 25, 2023. Ujumbe huu ulisomwa na Abdilatif Abdalla kwenye sherehe hizo.