Jinsi ya kurudi Nyumbani ni mkusanyiko wa mashairi 50 yaliyotungwa na Esther Karin Mngodo. Kitabu hicho kimechapishwa mwaka 2021 na kusanifiwa na Enchi House. Mchoro wake wenye mvuto umechorwa na Dinah Manongi na mtiririko wa mashairi ukihaririwa na Neema Komba. Hakika huu ni utatu wa ushirikiano wa umbu.

Moja ya mashairi yaliyonigusa sana humo ni shairi la 10 lililobeba jina la kitabu. Hilo ndilo lililonipa hamasa ya kuandika mapitio haya baada ya kulisoma lote kwa rafiki yangu wa karibu ambaye naye ni umbu. Shairi hilo la 10 lina beti 10 zikisindikizwa na hitimisho linalotoa jibu la swali hili ambalo nimekuwa najiuliza: Nyumbani ni wapi?

Mwandishi anajaribu kujenga hoja kuwa miili yetu ndiyo nyumba. Hivyo, kimantiki, kurudi nyumbani ni kurudi kwenye umiliki wa hizo nyumba zetu. Ni dhahiri kuwa Biblia ina nafasi kubwa katika falsafa na sanaa ya mtunzi maana dhana hiyo na zinginezo ipo kwenye kitabu hicho ambacho nacho ni mkusanyiko wa vitabu kadhaa pia.

Alichofanya mwandishi ni kuzichakata dhana hizo anuwai na kuziweka katika mazingira yetu ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili miili yetu – yaani nyumba zetu. Mathalan, kwenye ubeti wa nane anatupa ushauri huu:

Hofu na hasira vikikupanda, tuliza moyo kwa shairi
Jizamishe kwenye beseni la kujipenda na kumbuka kila mtu aliyewahi kukuambia anakupenda.
Maneno yao yakusafishe kama maji ya Mto Nile.

Shairi lingine lililonigusa ni la “Barua kwa Bibi Titi’ kwa sababu kwa muda sasa nimekuwa natafiti kuhusu maisha ya mwanamke huyo jasiri katika historia ya Tanzania. Sidhani kuwa ni kwa bahati mbaya shairi hilo ambalo ni la 19 limetanguliwa na mashairi haya mawili – ‘Awezalo Kulisema Mwanamke Hadharani’ na ‘ Nani Kama Mama?’

Esther anaanza barua yake hiyo na “Salaam Mama” na kumalizia ubeti huo kwa kumvumishia sifa ya “Mwanamke wa shoka.” Hakika Mama naam Bibi Titi alikuwa mwanamke ‘ngangari’ aliyeweza kuyasema hadharani hata yale ambao wengine hawakuweza. Mengine bado hawawezi kuyasema hadi imebidi mwandishi ayawekee alama ya kuyakata kwenye shairi lake linalohusu wanayoweza kuyasema wanawake hadharani. Basi bila kukumalizia ladha na hamu yote naomba ruhusa yako ewe msomaji mwema kunukuu walau ubeti huu mmoja wa shairi la Bibi Titi:

Wanaume walijificha nyuma yako.
Walimwogopa mwanamke huyu asiyeogopa kuzungumza mbele yao.
Uliijenga Tanganyika.
Ulileta uhuru.
Ulisimama mbele ya wanaume kumtusi Malkia.
Ulisema, imetosha.
Ulisababisha TANU ipate ushindi.
Ulisababisha badiliko.
Na hilo lilikugharimu maisha yako yote.

Mpenzi msomaji kama hujui basi ujue mtunzi pia ana wimbo wa Titi, Bibi Titi unaoweza kuusikiliza YouTube.

Bi Esther pia ametoa mawaidha kwa ‘wana’ ambao bado hawajui ‘Jinsi ya Kumpenda Mwanamke’, hilo likiwa ni shairi la pili kwenye kitabu. Kahoji pia wadau wanaowasumbua ‘wasimbe’ kwa kuwauliza ‘Unaolewa lini?’ ambalo ni shairi la 11. Ujumbe huo unwahusu pia wanaowaghasi ‘senior bachelors’ kwa kuwaamuru: Oa Kaka Oa (OKO).

Kila shairi lipo. Ukitaka la ‘Hedhi’ lipo. La ‘Hina’ lipo. Hata la ‘Fumanizi’ lipo. Na pia ya ‘Taifa’ na ‘Uhuru’ yapo.

Sitakitendea haki kitabu hiki kama sitakipa heko kwa kuwa na shairi lenye jina ‘Akwilina’. Shairi hilo la 21 humo ni kumbukuzi ya binti huyo aliyeuliwa katika mazingira ya kutatanisha yaliyoweka doa kubwa katika historia yetu ya kisiasa. Kwa hasira shairi linahoji: “Yuko wapi Demokrasia? Katiba Mpya kutupatia? Yuko wapi Akwilina?….”

Unaweza kuugawa mkusanyiko wa mashairi haya kwenye dhima kuu nne. Upendo. Haki. Amani. Upatanisho. Hivi ukiwa navyo mwilini basi utakuwa umerudi nyumbani. Iwe ni kwenye mahusiano ya kimapenzi au kisiasa.

Kwa kiasi kikubwa kitabu hiki ni kwa ajili ya ‘Umbu’ ambalo ni jina la shairi mojawapo. Ndiyo maana mwandishi mwanzoni kabisa kwenye wakatabahu kasema ni kitabu “Kwa Jasmine Mainda-Rose”, yaani bintiye, na “Kila mwanamke asomaye.” Kama hujui maana ya umbu  tembelea tovuti yake yenye jina hilo – https://umbu.africa/.